Oct 27, 2017 02:43 UTC
  • Ijumaa tarehe 27 Oktoba 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 7 Safar 1439 Hijria sawa na oktoba 27, 2017.

Miaka 1389 iliyopita inayosadifiana na tarehe 7 Safar mwaka wa 50 Hijria kwa kwa kujibu wa baadhi ya mapokezi, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as) mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia Madina. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake. Mjukuu huyo wa Mtume aliuawa shahidi kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufiyan.

Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita nchi ya Norway ilivunja muungano wake na Sweden na kujitangazia uhuru. Kabla ya karne ya 14 Norway ilikuwa nchi yenye ushawishi na moja ya madola vamizi. Hata hivyo mnamo mwaka 1380 ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Denmark na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo kwa muda wa karne 4.

Bendera ya Norway

Miaka 107 iliyopita katika siku kama leo, baada ya Japan kupigana vita na nchi mbili za China na Russia kwa miaka kadhaa na kupata ushindi katika vita hivyo, iliunganisha rasmi ardhi ya Korea na ardhi yake. Korea iliendelea kuwa chini ya udhibiti wa Japan hadi mwaka 1945 wakati Japan iliposhindwa katika Vita vya Pili vya Dunia.

Na tarehe 7 Safar miaka 28 iliyopita alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sayyid Shahabuddin Mar-ashi Najafi mmoja wa Marajii na viongozi wa juu wa Kiislamu hapa nchini, akiwa na umri wa miaka 96. Alimu huyo alisoma elimu za fiqihi, usul fiqihi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani, teolojia na misingi ya kimaadili katika vyuo vikuu vya kidini katika miji ya Kadhmein na Najaf, Iraq. Miongoni wma athari kubwa zilizoachwa na Ayatullah Mar-ashi Najafi ni maktaba kubwa ya vitabu iliyoko mjini Qum, ambayo inahesabiwa kuwa ya aina yake. Mwanazuoni huyo pia daima alikuwa muungaji mkono mkubwa wa Imam Ruhullah Khomeini na harakati ya Mapunduzi ya Kiislamu ya wananchi wa Iran.

Ayatullahil Udhma Sayyid Shahabuddin Mar-ashi Najafi