Jumamosi 11 Novemba, 2017
Leo ni Jumamosi tarehe 22 Safar 1439 Hijria sawa na tarehe 11 Novemba 2017.
Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, aliaga dunia Yasser Arafat Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kiongozi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) katika hospitali moja mjini Paris, Ufaransa. Alizaliwa mwaka 1929 na kuanza harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Israel akiwa katika rika la ujana. Mwaka 1946, Yasser Arafat alielekea nchini Misri kwa ajili ya masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Cairo na miaka mitano baadaye alihitimu masomo katika taaluma ya Usanifu Majengo. Mwaka 1965 alirejea Palestina na kuasisi Harakati ya Fat-h ili kupambana na utawala wa Tel Aviv. Miaka minne baadaye alichukua hatamu za kuongoza PLO hadi alipoaga dunia.
Miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo, Angola ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno. Wakoloni wa Kireno kwa mara ya kwanza waliingia katika ardhi ya Angola mwaka 1483 Miladia. Wakati huo, ardhi ya Angola ilikuwa sehemu ya ufalme wa Kongo, Zaire ya zamani.
Katika siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, virusi vinavyosababisha maradhi hatari ya kupooza viungo vya miili ya watoto yaani Polio viligunduliwa. Virusi hivyo vilipewa jina la virusi vinavyolemaza watoto kwa sababu ya kuwashambulia zaidi watoto wadogo na kuwapoozesha viungo vyao vya mwili. Baadaye kidogo mwanasayansi Dakta Jonas Salk aliyegundua virusi vya Polio alifanikiwa pia kugundua chanjo yake.
Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, Vita vya Kwanza vya Dunia vilifikia kikomo baada ya kutiwa saini mkataba wa kuacha vita hivyo. Vita vya Kwanza vya Dunia vilipiganwa kuanzia mwaka 1914 hadi 1918 kati ya nchi waitifaki yaani serikali za Russia, Uingereza, Ufaransa na Italia kwa upande mmoja, na nchi za Ujerumani, Bulgaria, Utawala wa Othmania na ufalme wa Austria na Hungary kwa upande wa pili. Watu zaidi ya milioni 15 waliuawa katika vita hivyo na wengine milioni 20 kujeruhiwa. Vilevile vilisababisha hasara inayokadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 150 kwa nchi zilizopigana vita hivyo.
Na miaka 810 iliyopita aliaga dunia Ibn Nuqta alimu na mtaalamu wa hadithi wa Baghdad. Alikuwa na hamu ya kujifunza elimu ya hadithi akiwa bado mdogo na alisafiri katika maneo na nchi nyingi kama Misri, Khorasani, na Sham kwa ajili ya kusikia hadithi za Mtume (saw). Msomi huyo wa Kiislamu amekusanya hadithi nyingi na kulea wanafunzi wengi katika taaluma hiyo. Miongoni mwa wanafunzi wake ni Ibn Asaakir. Ameandika vitabu kadhaa katika taaluma hiyo kikiwemo kile cha al Istidrak.