Nov 25, 2017 02:49 UTC
  • Jumamosi, Novemba 25, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 6 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1439 Hijria sawa na tarehe 25 Novemba 2017 Miladia.

Miaka 835 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Jalaluddin Muhammad Balkhi maarufu kwa jina la Molavi, mshairi mkubwa wa Iran katika mji wa Balkh ambao ni moja kati ya miji ya Iran ya wakati huo. Molavi alihesabiwa kuwa mshairi mkubwa na maarufu zaidi katika karne ya 9 Hijria Shamsia na miongoni mwa wanafikra na wachamungu wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Baada ya muda Molavi alihamia katika mji wa Konya akiandamana na baba yake. Baadaye alielekea Syria kwa ajili ya masomo ya juu. Miongoni mwa vitabu muhimu zaidi vya Maulawi ni Mathnawi Maanavi, Fihi ma Fihi, Maktubat Maulana na Rabaiyat. Malenga huyo mkubwa wa Kiirani alifariki dunia mwaka 672 Hijria Shamsia. ***

Jalaluddin Muhammad Balkhi maarufu kwa jina la Molavi,

Siku kama ya leo miaka 137 iliyopita sawa na Novemba 25 mwaka 1880, kijidudu maradhi kinachosababisha maradhi ya Malaria kiligunduliwa na Charles Luis Alphonse Laveran, tabibu mashuhuri wa Kifaransa. Ugunduzi huo wa kijidudu maradhi cha malaria ulitayarisha uwanja mzuri wa kukabiliana na kuangamiza maradhi hayo. Mnamo mwaka 1907 Dakta Alphonse Laveran alitunukiwa Tuzo ya Nobeli kutokana na utafiti wake katika masuala ya tiba. ***

Charles Luis Alphonse Laveran

Katika siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, yaani tarehe 4 Azar mwaka 1329 Hijiria Shamsia, Tume ya Mafuta ya Bunge la Taifa la Iran, ilipinga mkataba ziada wa mafuta kati ya Iran na Uingereza. Mkataba huo ulikuwa na lengo la kuimarisha nafasi ya Uingereza na kuzidisha uwezo wa nchi hiyo kuchimba mafuta huko kusini mwa Iran. Vile vile mkataba huo uliotayarishwa katika kilele cha ushindani wa Marekani na Uingereza wa kupora utajiri wa mafuta wa Iran, ulitambuliwa kuwa ni tishio kwa maslahi ya taifa. ***

Kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran na kufanywa kuwa mali ya taifa

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Zaire ya zamani, Jenerali Mobutu Sese Seko alitwaa madaraka ya nchi kupitia mapinduzi ya umwagaji damu. Mobutu alizaliwa mwaka 1930 nchini Congo na mwaka 1950 alijiunga na harakati ya ukombozi ya Patrice Lumumba. Baada ya uhuru wa Congo, Jenerali Mobutu alishika uongozi wa jeshi la nchi hiyo na mwaka 1960 alikuwa Waziri Mkuu akiwa na umri wa miaka 30. Tarehe 25 Novemba mwaka 1965 Mobutu alipindua serikali na kushika hatamu za nchi hiyo aliyeitawala kidikteta. Tarehe 16 Mei 1997 Mobutu alilazimika kukimbia nchi hiyo na kwenda Morocco ambako alifia huko na kuacha nyuma faili jesi la ukatili na mauaji. ***

Jenerali Mobutu Sese Seko

Na miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Suriname ambayo kijiografia ipo katika Amerika ya Kusini ilijitangazia rasmi uhuru wake toka kwa Uholanzi. Mwanzoni mwa karne ya 16 nchi hiyo ilikuwa chini ya utawala wa Uingereza. Mwaka 1954 Suriname ilijipatia utawala wa ndani na miaka 21 baadaye ikajipatia uhuru kamili. Nchi hiyo inapakana na Brazil na Guyana na iko katika pwani ya Bahari ya Atlantic. ***

Bendera ya Suriname

 

Tags