Jumatatu tarehe 23 Aprili 2018
Leo ni Jumatatu tarehe 6 Shaaban 1439 Hijria sawa na tarehe 23 Aprili, 2018.
Siku kama ya leo ya tarehe 3 mwezi ordibehesht katika kalenda ya mwaka wa Kiirani ni siku ya kumuenzi Sheikh Bahauddin Muhammad Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, wmanazoni mkubwa wa taaluma mbalimbali za Kiislamu. Sheikh Bahai ambaye alikuwa ametabahari katika elimu nyingi kama fiqhi, nujumu, hadithi, tafsiri ya Qur'ani na hesabati alifariki dunia katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alizaliwa mwaka 953 Hijria katika mji wa Baalabak huko Lebanon katika familia ya Kiirani. Baba yake alikuwa miongoni mwa mashekhe wakubwa wa zama hizo. Sheikh Bahai ameandika vitabu zaidi ya mia moja ikiwa ni pamoja na Tashrihul Aflak, Kashkul na Hablul Matin.

Katika siku kama ya leo miaka 402 iliyopita, alizaliwa William Shakespeare, mshairi na mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza wa Uingereza. Shakespeare alianza kazi zake za usanii sambamba na kushiriki katika michezo ya kuigiza. Alipata umashuhuri mkubwa katika fani hiyo. Kazi zake za kisanii zilikuwa mchanganyiko wa sanaa iliyoakisi majonzi na vichekesho.

Miaka 160 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa mwanafizikia Max Plank wa Ujerumani ambaye pia alikuwa mtaalamu wa hisabati aliyebuni nadharia ya kwanta katika elimu ya fizikia. Mwaka 1918 Max Plank alitunukiwa tuzo ya fizikia ya Nobel kwa kugundua nadharia ya kwanta. Plank ambaye alikuwa mpinzani mkubwa wa dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolph Hitler, alifanya utafiti mkubwa katika nyanja za mwendojoto (sayansi ya uhusiano wa joto na kazi za mitambo), fizikia nadharia, joto, mnururisho na nuru na kuandika vitabu kadhaa katika medani hiyo.

Katika siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Aprili 1992, alifariki dunia Satyajit Ray mwandishi na mtengeneza filamu mashuhuri wa India. Satyajit Ray alizaliwa mwaka 1921, na filamu zake za kijamii ziligusa zaidi hisia za jamii ya wananchi wa nchi hiyo, na kupelekea kupendwa zaidi na wananchi wa India.

Na tarehe 23 Aprili miaka 23 iliyopita Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliitangaza siku hii ya kuwa Siku ya Kimataifa ya Kitabu na Haki za Mwandishi. Lengo la kutangazwa siku hiyo ni kuonesha umuhimu wa kitabu na haki za waandishi wa vitabu, kuhamasisha watu kusoma vitabu, kuwapongeza watu wanaoandika vitabu kwa ajili ya kukuza na kustawisha utamaduni wa jamii ya mwanadamu na vilevile kuunga mkono na kusaidia ustawi wa sekta ya kusambaza vitabu. Utamaduni wa kusoma vitabu umeshamiri zaidi katika dunia ya sasa hususan miongoni mwa tabaka la vijana kutokana na kusambaa zaidi vitabu vya elektroniki kupitia mitandao ya intaneti.
