Jan 01, 2026 02:45 UTC
  • Leo katika historia
    Leo katika historia

Leo ni Alkhamisi tarehe 11 Rajab 1447 Hijria sawa na tarehe Mosi Januari mwaka 2026.

Leo ni tarehe Mosi Januari inayosadifiana na kuanza mwaka mpya wa 2026 Miladia.

Mpangilio wa miezi ya mwaka wa Kirumi unaoanza Januari hadi Disemba ulianza kutumiwa katika kipindi cha Mfalme Numa Pompilius wa Roma yapata miaka 700 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa Masih (as).

Kwa msingi huo tarehe 31 Disemba huwa siku ya mwisho ya mwaka wa Miladia na usiku wa kuamkia tarehe Mosi Januari huanza sherehe za kupokea mwaka mpya katika jamii za Wakristo na nchi nyingi za Afrika, America, Ulaya, Australia na hata Asia.

Tunawatakia heri ya mwaka mpya watu wote wanaoadhimisha mwaka huu. 

Miaka 1176 iliyopita mwafaka na leo, alizaliwa mtaalamu wa fasihi, lugha na mfasiri wa Qur'ani Tukufu, Abubakar Muhammad, maarufu kwa jina la Ibn al Anbari. Msomi huyo alizaliwa huko Baghdad nchini Iraq.

Alijifunza elimu ya Hadithi baada ya kukamilisha masomo yake ya lugha na sayansi za Qur'ani tukufu. Ibn al Anbari alikuwa na uwezo wa hali ya juu wa kuhifadhi na kushika vitu kichwani mwake.

Alikuwa mtu mwema na mchamungu na mbali na kujishughulisha na kufundisha na kulea vizazi vya maulamaa, mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na vitabu vya "Adabul Kaatib" na "Dhamaairul Qur'an." Alifariki dunia mwaka 328 Hijiria akiwa na umri wa miaka 57. 

Miaka 876 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia mjini Damascus, Syria mwanahistoria mkubwa na mtaalamu wa Hadithi Ibn Asakir.

Alisoma elimu za Qur'ani, hadithi, fiq'hi na usulu fiq'hi kwa wasomi wakubwa wa mjini Damascus. Baada ya hapo Ibn Asakir alianza safari ndefu yenye lengo la kukamilisha masomo yake na kupata elimu katika vituo vya kielimu vya Baghdad, Kufa, Mosul, Neishabur, Marv, Isfahan na Hamedan.

Msomi huyo ameandika vitabu 134 kikiwemo kile cha "Tarikh Dimishqi." 

Miaka 222 iliyopita sawa na tarehe Mosi Januari mwaka 1804 nchi ya Haiti ilijitangazia uhuru ikiwa nchi ya kwanza kufanya hivyo katika eneo la Amerika ya Latini.

Uhuru wa Haiti ulipatikana kufuatia mapambano na harakati kubwa ya watumwa weusi wa nchi hiyo dhidi ya vitendo vya utumwa vya Ufaransa na kisha baadaye kuanzisha mapambano dhidi ya jeshi la Ufaransa. Ufaransa ilianza kuikoloni Haiti mwaka 1677.

Baada ya kujipatia uhuru, Haiti ilikumbwa na machafuko ya ndani. 

Siku kama ya leo miaka 132 iliyopita Heinrich Rudolf Hertz mwanafizikia  na mwanahisabati wa Ujerumani aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 37.

Alizaliwa Hamburg nchini Ujerumani mwaka 1857. Alikuwa na mapenzi makubwa na fizikia na umakenika tangu akiwa kijana mdogo. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana akajiendeleza kimasomo katika uwanja huo. 

Miaka 70 iliyopita katika siku kama ya leo nchi ya Sudan ilipata uhuru kutoka kwa Misri na Uingereza.

Mwaka 1899 Uingereza na Misri zilitiliana saini mkataba wa kuitawala kwa pamoja Sudan. Katikati mwa karne ya 20 lilianza vuguvugu la kupigania uhuru nchini Sudan na mwaka 1956 Misri na Uingereza zikalazimika kuutambua uhuru wa nchi hiyo.

Sudan inapakana na nchi za Sudan Kusini, Misri, Libya, Chad, Kenya, Uganda, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. 

Tarehe Mosi Januari mwaka 1959 miaka 67 iliyopita mapinduzi ya Cuba yalipata ushindi na dikteta Fulgencio Batista akaikimbia nchi hiyo.

Ushindi wa mapinduzi hayo yaliyoongozwa na Fidel Castro uliiweka Marekani katika mazingira magumu baada ya kushindwa vibaraka wake nchini Cuba. 

Miaka 66 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Kiafrika ya Cameroon ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa.

Kwa miaka mingi nchi hiyo ilikuwa chini ya ukoloni wa nchi za Ulaya ikiwemo Ujerumani ambayo iliikalia kwa mabavu Cameroon kuanzia mwaka 1884.  Baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia Ufaransa na Uingereza ziligawana baina yao ardhi ya Cameroon. Hata hivyo haukupita muda kabla ya kuanza mapambano ya kupigania uhuru nchini humo.

Hatimaye mapambano ya kupigania uhuru nchini Cameroon yalizaa matunda katika siku kama ya leo baada ya nchi hiyo iliyoko magharibi mwa Afrika kujipatia uhuru. 

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, inayosadifiana na tarehe Mosi Januari 1993, yalianza kutekelezwa makubaliano ya Maastricht, eneo lililoko kusini mwa Uholanzi yaliyokuwa na lengo la kuondoa mipaka ya kiuchumi kati ya nchi 12 za Ulaya.

Mkataba wa muungano wa Ulaya ulitiwa saini tarehe 10 Disemba mwaka 1991 na viongozi wa nchi 12 wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya katika mji mashuhuri wa Maastricht. Baadaye Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya ilibadilishwa na kuwa Umoja wa Ulaya.

Utekelezwaji wa makubaliano ya Maastricht ulikuwa hatua kubwa katika mchakato wa kuungana zaidi wanachama wa Umoja wa Ulaya japo kuwa umoja huo ulikabiliwa na matatizo mengi katika miaka iliyofuatia.