Oct 30, 2018 02:34 UTC
  • Jumanne, Oktoba 30, 2018

Leo ni Jumanne tarehe 20 Mfunguo Tano Safar 1440 Hijria sawa na Oktoba 30, mwaka 2018 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) Imam Hussein bin Ali (AS) na watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume ambao waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria. Majlisi ya siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume na masahaba zake watiifu ambao walijisabilia roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika ardhi ya Karbala. Katika siku hii ya Arubaini pia msafara wa mateka wa Ahlibaiti wa Mtume uliokuwa umepelekwa Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiya uliwasili Karbala ukiwa na kichwa cha Imam Hussein na kukutana hapo na sahaba wa Mtume, Jabir bin Abdillah al Ansari na wafuasi wengine wa Imam waliokwenda hapo kufanya ziara. Siku hiyo Kichwa cha Imam Hussein kilizikwa pamoja na mwili wake.

Siku kama ya leo miaka 108 iliyopita, aliaga dunia Henry Dunant mwasisi wa taasisi ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu. Dunant alizaliwa mwaka 1828 Miladia huko Geneva Uswisi na baadaye akaanzisha kituo cha kuwahudumia watu waliojeruhiwa katika vita ambao hawakuwa na sehemu nzuri ya kupatia huduma. Henry Dunant alianzisha shirika la Msalaba Mwekundu kwa lengo la kuokoa maisha ya majeruhi wa kivita. Mwaka 1901, Dunant alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel kutokana na hatua yake hiyo ya kibinadamu na aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 82.

Tarehe 8 Aban miaka 38 iliyopita aliuawa shahidi Muhammad Hussein Fahmideh, kijana shujaa wa Kiirani kwenye vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Shahidi Fahmideh alielekea kwenye medani ya vita akiwa na umri wa miaka 13 tu, ikiwa imepita miezi michache baada ya kuanza kwa vita hivyo. Shahidi Fahmideh alijitolea mhanga kwa kujifunga kiunoni maguruneti na kujilaza mahala kilipokuwa kikipita kifaru cha adui na kuwatia kiwewe na hatimaye kuwalazimisha wavamizi kukimbia. Hatua hiyo ilipongezwa na Imam Khomeini ambaye alimtaja kijana huyo kuwa ni kiongozi na kigezo cha kuigwa.

Muhammad Hussein Fahmideh

Miaka 27 iliyopita yaani tarehe 30 mwezi Oktoba mwaka 1991, ulianza mkutano eti wa amani ya Mashariki ya Kati, kati ya utawala unaoikalia Quds kwa mabavu na Misri, Jordan, Syria, Lebanon na Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO, huko Madrid mji mkuu wa Uhispania kwa upatanishi wa Marekani. Katika mkutano huo na mikutano mingine kama hiyo ambayo iliitishwa kwa lengo la kufikiwa mapatano kati ya Waarabu na Israel, utawala wa Kizayuni ulisisitiza juu ya suala la amani mkabala wa amani, huku serikali za Kiarabu zikizungumzia kurejeshewa kwanza ardhi zao mkabala na kupatikana amani na kutaka kuondoka Israel katika ardhi zote za Waarabu inazozikalia kwa mabavu.

Siku kama ya leo 11 iliyopita Qaisar Aminpur malenga mahiri na mwanamapinduzi wa Kiirani alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu. Qaisar alizaliwa mwaka 1338 hijria shamsiya karibu na Dezful mji ulioko kusini mwa Iran. Aminpur alielekea Tehran baada ya kuhitimu masomo yake ya shule ya msingi na upili na kufanikiwa kutunukiwa shahada yake ya udaktari katika taaluma ya lugha na fasihi ya Kifarsi. Qaisar Aminpur aliandika mashairi yanayohusiana na mapinduzi mwanzoni mwa ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kushiriki katika kuasisi taasisi mbalimbali za masuala ya fasihi na sanaa. 

Qaisar Aminpur

 

Tags