Feb 19, 2019 14:15 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (139)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia na kujadili maudhui ya ujinga na ujahili ambao ni moja ya sababu za kutoshukuru na kukufuru neema za Allah. Tulisema kuwa, akili ni neema kubwa zaidi miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu ambazo Mola Muumba amemtunuku na kumruzuku mwanadamu. Aidha tulibainisha kwamba, jahili au mjinga ni mtu ambaye anajiona msomi katika kitu ambacho hana elimu nacho na anatosheka na rai na mtazamo wake tu, na hayuko tayari kuchukua na kuikubali mitazamo ya wengine. Kadhalika tuliashiria kuwa, katika Uislamu na katika Kitabu Kitakatifu cha Qur’ani ujinga na ujahili unatajwa kuwa sifa mbaya na isiyofaa na Waumini wanatakiwa wajipambe na elimu na maarifa na hivyo kujiweka mbali na madhara haribifu ya ujinga na ujahili. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 139 ya mfululizo huu kitaendelea na maudhui ya ujahiili lakini kuhusu ishara za ujahili na ujinga. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Hadithi ya Uongofu

Radhi ud-Deen Ali ibn Musa mashuhuri kwa jina la Sayyid Ibn Tawus, alimu na arif mkubwa wa Kiislamu amenukuliwa akisema kuwa, kaeni na wenye akili mtanasibishwa nao hata kama nyinyi si miongoni mwao; na msikae na wajinga, mtanasibishwa nao hata kama nyinyi si katika wao.

Inanukuliwa kuwa, siku moja Mtume wa Allah Issa Masia AS alikuwa akizungumza na kundi la masahaba zake. Mmoja wa masahaba zake akamuuliza: Ewe Mtume wa Allah! Wewe kwa idhini ya Mwenyezi Mungu unaweza kuhuisha wafu, unaweza kuwaponya wagonjwa na kuwafanya vipofu waone. Wewe umeweza kuwaponya watu ambao walikumbwa na maradhi hayakuwa na tiba kama mbalanga.

Umewaponya hata watu waliokuwa wamepooza, kiasi kwamba, wakaweza kusimama kutoka katika vitanda vyao na kutembea kwa miguu yao wenyewe. Hivi kuna maradhi ambayo huwezi kumfanya mtu apone?

Nabii Issa (AS) akajibu kwa kusema: Ndio mimi sijaweza kuwaponya watu wajinga na sijafanikiwa kufanya kitu ili wapone. Sahaba yule wa Nabii Issa AS akauliza kwa mshangao: Kwani ujinga ni katika maradhi? Na kama ni ugonjwa dalili na ishara zake ni zipi?

Nabii Issa akajibu kwa kusema:

Kwa hakika jahili au mjinga si mtu mwenye hali ya wastani na ya kati na kati na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana huchupa mipaka au kuzembea kupita kiasi katika mambo na kazi anazozifanya.

Ujinga

 Imam Ali bin Abi Twalib AS anaashiria jambo hili kwa kusema: Jahili daima ima huchupa mipaka auu huzembea kupita kiasi.

Kwa mfano mtu mjinga na jahili, hana mpaka katika utani na mzaha na huchupa mipaka katika utani wake na hujidogosha na kujidhalilisha. Na ndio maana Imam Ali bin Abi Twalib AS anawatahadharisha watu na kuwataka wajiepushe na utani na mzaha mwingi ili wasije wakatuhumiwa kwa ujahili, na hivyo izza na hesima yao ikaondoka. Imam Ali AS anasema: Kila mtu mwenye kufanya utani na mzaha sana, huhesabiwa kuwa ni mjinga.

Miongoni mwa ishara nyingine za ujinga na ujahili ni mtu kutonufaika na elimu na akili yake. Kuna watu wengi ambao kidhahiri ni wasomi na wenye elimu, lakini hawanufaiki na akili na elimu yao na ni mfano wa wazi wa ujahili.

Imam Ali bin Abi Twalib AS, ni wasomi wengi kiasi gani ambao, ujinga wao umewaua ilihali elimu yao ipo pamoja nao lakini haiwasaidii. Kwa mtazamo wa Imam Ali AS ni kuwa, moja kati ya ishara na dalili muhimu kabisa za ujinga ni kuwa na uadui na watu. Anasema: Mwanzo wa ujinga ni kuwafanyia watu uadui.

Hii ni kutokana na kuwa, Uislamu ni dini ya amani na urafiki na mtu ambaye anawafanyia watu wengine uadui ni jahili na mjinga wa maamrisho ya dini hiyo ambapo anajidhuru mwenyewe na vilevile jamii.

Ni kwa kuzingatia uhakika huu ndio maana Bwana Mtume SAW anasema:  Vitu vitatu kama mtu hatakuwa navyo si katika mimi. Mtume akaulizwa, ni vitu gani hivyo? Akasema: Subira ambayo kupitia kwayo anaondoa ujahili, tabia njema ambayo kupitia kwao anaitumia kuishi miongoni mwa watu, na utakasifu na uchaji-Mungu ambao unamzuia na hali ya kuasi amri na maamrisho ya Mwenyezi Mungu.

Kwa hakika, alimu na mwenye akili ni mtu ambaye anasoma alama za nyakati na ambaye anafanya kila jambo kulingana na zaman a wakati wake. Kila mtu kkatika maisha hujiwa na fursa ambapo wakati mwingine kutokanan na ujahili wake na kuutokuwa na ufahamu na uelewa, huziacha fursa hizo zimpite.

Ujinga na ujahili

Miongoni mwa ishara nyingine za ujinga kwa mtu tunaweza kuashiria suala la kukataa kupokea ushauri. Kwa hakika mtu mjinga na jahili hazuiwi na katazo lolote na si mwenye kukubali ushauri. Kadiri mjinga atakavyousiwa na kupewa ushauri, hupuuza yote hayo na kufanya lile alitakalo yeye. Hii ni kutokana na kuwa, mjinga huhisi kwamba, yeye tu ndiye mwenye udiriki na ufahamu sahihi wa mambo.

Kwa zama zetu hizi mfano wa mawahabi na matakfiri ambao huwakuurusisha wasiokuwa wao na hujiona kwamba, wao ndio wanaoifahamu zaidi dini ya Uislamu kuliko watu wengine, katika hali ambayo kutokana na ujahili walionao wamekuuwa wakitoa fatuwa za kumwagwa bure bilashi damu za Waislamu wengine wasio na hatia yoyote, na katu mawaidha na nasaha za mtu yyopyote yule hazina athari kkwao.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo unakomea hapa tukutane tena juma lijalo.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

 

 

Tags