Hadithi ya Uongofu (144)
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.
Kipindi chetu cha juma lililopita kilijadili maudhui ya kuwafurahisha Waumini, umuhimu wake na jinsi suala hilo lilivyosisitizwa katika Uislamu. Tulibainisha kwamba, moja ya mambo ambayo katika Uislamu yanahesabiwa kuwa ni ibada kubwa na ambalo limeelezwa katika hadithi kwa sura tofauti ni kutia furaha katika nyoyo za Waumini au kuwafurahisha Waumini. Tulikunukulieni hadithi kadhaa zinazobainisha umuhimu wa kuwafurahisha Waumini ikiwemo ile ya kutoka kwa Imam Ali bin Hussein al-Sajjad AS inayosema: Amali inayopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu ni kutia furaha katika nyoyo za Waumini. Na ile ya Imam Muhammad Baqir AS inayosema: Hajaabudiwa Mwenyezi Mungu kwa kitu kinachopendwa mbele ya Mola Muumba kama kutia furaha katika nyoyo za Waumini. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 144 ya mfululizo huu kitazungumzi maudhui ya urafiki na upendo. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.
Wapenzi wasikilizaji, Uislamu ni dini ya rehma, upendo, usawa, urafiki na udugu. Kuna aya na hadithi nyingi zinazobainisha na kutilia mkazo juu ya ulazima wa kuweko huba, upendo na urafiki baina ya Waumini. Kimsingi ni kuwa moja ya sifa za kipekee za Waumini ni kwamba, wao ni watu wa urafiki, udugu na kupendana. Aidha Mwenyezi Mungu SWT ameisimamisha dini yake tukufu ya Uislamu katika nguvu ya huba na upendo.
Na akauweka ufunguo wa saada na ufanisi wa mwanadamu duniani na akhera katika urafiki, upendo na huba. Kwa hakika, urafiki na upendo huu una umuhimu kiasi kwamba, Mtume SAW amenukuliwa akisema kuwa: Msingi wa akili baada ya imani juu ya Mwenyezi Mungu ni kufanya urafiki na kuwa na upendo na huba na watu.
Kupitia hadithi hii tunafahamu kwamba, kufanya urafiki na watu ni ishara ya mtu kuwa na akili na wakati huo huo, ni ishara ya kuwa na imani juu ya Mwenyezi Mungu, Mola Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo.
Uislamu ukiwa na lengo la kuhakikisha kwamba, mwanadamu anafikia ukamilifu, umembainishia njia ya wazi na inayoeleweka bayana. Moja ya mambo bora kabisa ambayo yanamfanya mtu afikie ukamilifu ni huba na upendo.
Suala la huba na upendo lina taathira katika kufanikisha mipango ya Uislamu kiasi kwamba, Imam Muhammad Baqir AS anaona kuwa, dini ya Uislamu haina kitu kingine bighairi ya mahaba na upendo. Anasema katika hadithi yenye alama ya swali na udadisi, Je dini ni kitu kingine ghairi ya upendo?. Mtume SAW amenukuliwa akisema: Watu wa umma wangu watabakia katika saada na ufanisi madhali ni marafiki, wanapeana zawadi na ni wenye kuchunga amana (baina yao).
Hata hivyo lililo la msingi katika suala zima la urafiki na upendo ni urafiki na upendo wa dhati na sio urafiki wa kiamaslahi, wa kuchezana shere, wa mmoja kutaka kunufaika tu na mwenzake lakini hakuna huba na upendo baina yake na mwenzake. Urafiki wa kweli na wenye nia ya dhati humfanya anayeshikamana nao kuwa mtu wa peponi. Hii ni kutokana na kuwa, Mwenyezi Mungu anapenda kuwaona watu wakiwa marafiki.
Kuna hadithi zinazobainisha kwamba, kufanya urafiki na watu ni kitendo kitokacho kwa Mwenyezi Mungu na kinachopendwa na Mola Muumba, ilihali kuwafanyia watu uadui ni jambo litokalo kwa shetani mlaaniwa.
Moja sifa njema na aali za Waumini ni kwamba, ni wenye kufanya urafiki baina yao na wenye kupendana, na ambao nyumba zao daima haziishi wageni. Kwa maana kwamba, ni wenye kutembeleana. Urafiki una umuhimu mkubwa kiasi kwamba, Imam Ja’afar Swadiq AS anautaja kuwa ni aina fulani ya udugu.
Anasema:
الصدیق اقرب الاقارب
Rafiki ni ndugu wa karibu kabisa.
Kwa hakika urafiki, huba na upendo ni mambo matamu kiasi kwamba, huyafanya machungu yote ya maisha kuwa matamu na kupitia huba na upendo na urafiki, mapungufu mengi, magumu na mtatizo ya mtu binafsi na ya kijamii huwezekana kupatiwa ufumbuzi kupitia kushikamana na urafiki na upendo n ahata kusahau machungu aliyokumbana nayo mtu.
Linalopaswa kufahamika vyema ni kuwa, kitovu kikuu cha huba, upendo na urafiki ni Mwenyezi Mungu mwenye huruma. Mwenyezi Mungu amewaletea wanadamu Kitabu Kitukufu cha Qur’an kupitia kwa Mtume Muhammad SAW kikianza na huba na upendo pale anaposema:
بسم الله الرحمن الرحیم
Yaani kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu.
Aidha katika aya ya 63 ya Surat al-Anfal Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume Wake kwamba:
وَأَلَّفَ بَینَ قُلوبِهِم ۚ لَو أَنفَقتَ ما فِی الأَرضِ جَمیعًا ما أَلَّفتَ بَینَ قُلوبِهِم وَلٰکِنَّ اللَّهَ أَلَّفَ بَینَهُم ۚ إِنَّهُ عَزیزٌ حَکیمٌ
Na akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungelitoa vyote vilivyomo duniani usingeliweza kuziunga (unganisha) nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye waunganisha. Hakika Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Katika hadithi kumeashiriwa namna ya kuanzisha upendo na urafiki huu. Kwa mfano Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema: Kila mtu huanzisha urafiki na upendo na mtu mfano wake (yaani mwenye mielekeo kama yake).
Kwa upande wake Imam Ja’afar Swadiq AS siku moja alimwambia Omar bin Yazid aliyekuwa mmoja wa wanafunzi wake: Kila kitu hupata utulivu kwa kitu kingine. Muumini naye hupata utulivu kupitia kwa ndugu yake Muumini. Kama ambavyo ndege hupata utulivu kwa ndege mfano wake, je hujaona na kupata tajiriba ya kitu kama hiki?
Utulivu ambao mtu anaupata kutoka kwa rafiki au kwa mtu ambaye ana huba na upendo kwake, hauishii katika ulimwengu huu wa dunia tu, bali huwa na msaada pia katika ulimwengu wa Akhera.
Jabir bin Abdillah al-Ansari swahaba mwema wa Bwana Mtume SAW siku moja alimhutubu rafiki yake Attiyah bi Aufi kwa kumwambia: Ewe Atiyyah nimesikia kutoka kwa kipenzi changu Mtume Muhammad SAW akisema kwamba:
Kila mwenye kuwapenda watu wa kaumu fulani atafufuliwa nao na kila mwenye kupenda kitendo fulani cha watu, basi ni mshirika wa amali yao hiyo…Mpende kipenzi cha watu wa kizazi cha Mtume madhali angali anawapenda; na mchukie adui wa Kizazi cha Mtume madhali anawafanyia uadui; hata kama atakuwa ni mwenye kufunga sana na kukesha usiku akifanya ibada. Amialiana kwa ulaini na kipenzi cha Muhammad na kizazi chake; kwani kama atateleza upande mmoja kutokana na dhambi zake, basi, katika upande mwingine atabakia imara kutokana na mapenzi yake kwa watu wa nyumba ya Mtume. Kimsingi ni kuwa, marejeo na mafikio ya vipenzi wa Muhammad na aali zake ni peponi na mafikio ya maadui zao ni motoni.
Muda wa kipindi chetu cha Hadithi ya Uongofu kwa leo, umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…