Mar 07, 2019 16:55 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (142)

Natumai hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni kutegea sikio sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungumzia suala la hofu na matarajio.

Tulisema kuwa, hofu na matarajio ni aina mbili muhimu za tablighi na ufikishaji ujumbe katika dini zote za mbinguni, na Mitume wa Mwenyezi Mungu walikuwa wakitumia mbinu hizi katika kulea watu na kadhalika katika kulea nafsi zao. Tulikunukulieni hadithi kutoka kwa Imam Ja’afar bin Muhammad al-Swadiq AS inayosema: “Muumini hawezi kuwa muumini mpaka atakapokuwa mwenye hofu na mwenye matarajio, na hawezi kuwa mwenye hofu na matarajio mpaka atakapokifanyia kazi kile anachokiogopa au kile ambacho ana matarajio nacho.

Kadhalika tulibainisha kwamba, hofu na matarajio ni katika sifa za waumini na wacha Mungu. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 142 kinatendelea na maudhui hii ya hofu na matarajio. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi. Karibuni.

Image Caption

 

Kwa hakika kumuogopa Mwenyezi Mungu ni daraja miongoni mwa daraja za imani na cheo miongoni mwa vyeo vya maulama. Imekuja katika Aya ya 28 ya Surat Faatir kwamba:

 إِنَّمَا یخْشَی اللّه مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ

 

Kwa hakika wanaomcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni.

Kwa mujibu wa Aya hii na kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, wanazuoni na wasomi wa Mwenyezi Mungu ndio ambao hudiriki adhama ya Mola Muumba kuliko watu wengine na hutambua kwamba, kuzembea kidogo tu kutekeleza jukumu miongoni mwa majukumu na masuuliya yao mkabala na Allah SWT ni dhambi kubwa isiyostahiki msamaha.

Kwa hakika wanaomcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni.

Imenukuliwa kutoka kwa Imam Ja’afar bin Muhammad al-Swadiq AS ya kwamba amesema: Muumini yupo katika hofu mbili, dhambi ya huko nyuma ambayo hafahamu Mwenyezi Mungu atamfanya nini, na umri uliobakia ambao hajui  ataangamia na amali zake au la. Hivyo basi daima yumo katika hofu na woga na huu woga ndio ambao humrekebisha.

Kupitia hadithi hii tunafahamu kwamba, kumuogopa Allah humsaidia mja Muumini ajirekebishe na hivyo kumfanya awe ni mwenye kutenda amali njema. Aidha katika hadithi nyingine Imam Ja’afar Swadiq AS amenukuliwa akisema kuwa:  Msomi na alimu zaidi miongoni mwenu ni yule ambaye anamuogopa zaidi Mwenyezi Mungu kuliko wengine.

Katika hadithi hii Imam Swadiq AS anataka kutufundisha kwamba, alimu na msomi zaidi miongoni mwa watu ni yule anayemuogopa Allah na kumcha. Kwani mja anayemuogopa Allah ndiye ambaye amediriki na kufahamu adhama ya Mwenyezi Mungu na kupitia kumuogopa Mola Muumba, hujiepusha na maasi na makatazao yake na badala yake hujikita zaidi katika kutenda amali njema na matendo yanayomfurahisha na kumridhisha Mwenyezi Mungu.

 

Wapenzi wasikilizaji kuna nukta muhimu ya kuzingatia hapa, nayo ni kwamba, licha ya thamani zote zilizopo katika kumuogopa Mwenyezi Mungu, lakini mja anapaswa kuwa makini ili hofu na woga huu usifikie hatua ya kuwa kizuizi cha mtu kupata ustawi na maendeleo.

Kwa hakika mimi namuogopa Allah

Moja ya madhara ya kuchupa mipaka katika hofu na kumuogopa Mwenyezi Mungu na ambayo humzuia mwanadamu kufikia ukamilifu na saada ni kuikataa na kuipa mgongo dunia. Uislamu umekataza na kupiga marufuku suala la mtu kujikunja na kuweka kando kila kitu na badala yake kukaa tu na kumuabudu Mwenyezi Mungu. Hili ni jambo ambalo haliruhusiwi katika Uislamu, kwani mbali na kufanya ibada mtu anapaswa kuwa na muda wa kutafuta maisha na riziki ya halali na kuburudika na neema halali za hapa dunia.

 Inanukuliwa kwamba, siku moja mke wa Othman bin Madh’un mmoja wa masahaba wa Mtume SAW ambaye alikuwa mcha Mungu na mwenye kujipinda mno kwa ajili ya ibada alimuendea Mtume akiwa na mashtaka dhidi ya mumewe huyo. Alipofika kwa Mtume alisema:

Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mume wangu Othman masiku mengi anafunga Saumu na nyakati za usiku anakesha tu akifanya ibada. Baada ya Mtume kusikia mashtaka hayo, alikasirika mno kiasi kwamba, alisimama hapo hapo na kuelekea nyumbani kwa Othman. Alipofika alimwambia: Ewe Othman! Mwenyezi Mungu hakinituma na kuniteua mimi ili nije kuwa mtu wa kujikhini na kuipa mgongo dunia, bali alituma ili nije kuwafikishia watu dini iliyonyooka, nyepesi na ya kati na kati.

Moja ya madhara mengine ya hofu ni kukata tamaa. Imam Ali bin Abi Twalib AS anaitaja hali ya kukata tamaa kwamba, ni muuaji wa mtu na kusema:

"أعظم البلاء انقطاع الرجاء"

Balaa kubwa kabisa ni kukata tamaa.

 

Balaa kubwa kabisa ni kukata tamaa.

Pamoja na hayo katika matumaini pia mtu anapaswa kumzingatia na kumtanguliza Mwenyezi Mungu na ajichunge asije akachupa mipaka. Hii ni kutokana na kuwa, kama hali ya matumaini itavuka mpaka na kufikia katika kiwango kisicho cha kawaida na hali hiyo ya matumaini isiwe na hali ya hofu juu ya Mwenyezi Mungu, humfanya na kumfikisha mtu katika fikra, mawazo na ndoto za kibatili.

 

Kuna watu wanaposikia kwamba, Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa Rehma na Mwenye Kurehemu hulitumia hili kukwepa kirahisi kutekeleza majukumu yao na huacha kutenda amali njema. Waja wa aina hii hughafilika kwamba, rehma na huruma ya Mwenyezi Mungu ina masharti kama ambavyo imekuja katika Qur’an kwamba, sharti la kunufaika na rehma ya Mwenyezi Mungu ni imani na kufanya amali njema.

Ni jambo lililo wazi kwamba, hatupaswi kuwa kama wale wenye matumaini ya kukirimiwa akhera na Mwenyezi Mungu hali ya kuwa hawafanyi amali njema na hata watapoteleza na kutenda dhambi hawafanyi toba na kuomba maghufira kikwelikweli na kutorejea tena kutenda dhambi. Au tusiwe kama wale ambao wana matarajio ya kupata msamaha wa Mwenyezi Mungu hali ya kuwa wanapoteleza na kufanya dhambi na maasi hawatubu na kushikamana na toba. Kufanya hivi ni mithili ya mkulima ambaye amelima shamba lake lakini hajapanda mbegu, je ni akili na mantiki kusubiri kuja kuvuna. Bila shaka kufanya hivyo ni kutotumia akili ipasavyo.

Waumini wakweli ni wale wenye matumaini na radhi za Mwenyezi Mungu na pepo yake na wakati huo huo ni wenye kujipinda kwa ajili ya kufanya ibada na kutenda amali njema na ambao wanajiepusha na kila amali ambayo inamuudhi na kumghadhibisha Mwenyezi Mungu.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu cha Hadithi ya Uongofu kwa juma hili umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh….

Na Salum Bendera