Spoti, Feb 23
https://parstoday.ir/sw/news/event-i136950-spoti_feb_23
Huu ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyoshuhudiwa ndani ya siku saba zilizopita kitaifa, kieneo na kimataifa.
(last modified 2026-02-23T08:13:53+00:00 )
Feb 23, 2026 08:13 UTC
  • Spoti, Feb 23

Huu ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyoshuhudiwa ndani ya siku saba zilizopita kitaifa, kieneo na kimataifa.

Soka AFC: Teractor ya Iran yang'ara

Klabu ya soka ya Teractor ya Iran ilikamilisha awamu yao ya Ligi ya Mabingwa ya Asia ya AFC kwa msimu wa 2025/26, kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Al Gharafa ya Qatar Jumanne iliyopita.  Watengeza trekta wa Iran ambao tayari wamefuzu, waliibana Al Gharafa ya Qatar katika kipindi cha pili na kuzima matumaini yao ya kusonga mbele, huku bao la Hosseinzadeh la dakika ya 81 likikamilisha pambano hilo baada ya Mahdi Hashemnezhad kufungua ukurasa wa mabao mapema kunako dakika ya 20 ya mchezo. Kwa mujibu wa tovuti ya AFC, kumaliza kwa Tractor katika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ukanda wa Magharibi kunamaanisha kuchuana na Shabab Al-Ahli ya Umoja wa Falme za Kiarabu katika Raundi ya 16.

Teractor uwanjani Doha

 

Wakati huo huo, klabu ya Sepahan SC ya Iran ilipoteza dhidi ya Al Ahli ya Qatar na kuondolewa kwenye michuano hiyo ya AFC Champions League 2025/26™. Al Ahli SC ya Qatar iliwashinda Foolad Mobarakeh Sepahan SC ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bao 1-0 katika muda wa ziada siku ya Jumatano, na kujikatia nafasi katika robo fainali ya ligi hiyo.

Na kutia msumari moto kwenye kidonda, klabu ya Al Hussein ya Jordan walitoka nyuma na kuishinda Esteghlal ya Iran kwa mabao 3-2 katika mchezo wa pili wa Raundi ya 16 ya Ligi ya Mabingwa ya AFC 2025/26 siku ya Jumanne. Kikosi hicho cha Jordan kilisonga mbele kwa jumla ya mabao 4-2 na kitakutana na ama klabu ya Iran au Al Ahli ya Qatar katika robo fainali.

Rais wa Iran awaenzi wanariadha walemavu

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amewatunuku na kuwaenzi wanariadha 489 wa Paralimpiki na Viziwi wa Jamhuri ya Kiislamu katika hafla iliyofanyika Jumamosi katika Ukumbi wa Mkutano wa Tehran. Kwa mara ya kwanza, sherehe tofauti iliandaliwa ili kuwatambua wanariadha kutoka taaluma za michezo ya Paralimpiki, wanamichezo viziwi na wenye matatizo ya kuona. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Ahmad Donyamali, Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran, na Ghafour Karegari, Rais wa Kamati ya Kitaifa ya Paralimpiki ya Iran. Jumla ya mabingwa na washindi wa medali 489 wa michezo ya paralimpiki, vipofu na viziwi, walitambuliwa na kuenziwa kwenye sherehe hizo. Wanariadha hao wa Iran walitunukiwa medali mbali mbali katika mashindano tofauti ya kimataifa mwaka uliopita. Sherehe hiyo lilikuwa tukio la kwanza lililoandaliwa makhususi kuwaenzi washindi wa medali kutoka taaluma za michezo ya paralimpiki wa Iran.

Rais wa Iran na wanariadha wa Paralimpiki wa Jamhuri ya Kiislamu

 

Huku hayo yakiarifiwa, timu ya taifa ya mpira wa kikapu ya Iran iliikandamiza Qatar vikapu 71-58 katika mechi ya kirafiki wakati wa kambi ya mazoezi huko Doha.  Iran ambayo imesafiri hadi Qatar kuweka kambi ya maandalizi kabla ya dirisha la pili la mechi za kufuzu Kombe la Dunia la FIBA, ilicheza mchezo wao wa kwanza wa kupasha misuli moto dhidi ya timu ya taifa ya Qatar Jumamosi. Ikishahitimisha kambi ya mazoezi huko Qatar, timu basketboli ya Iran itasafiri hadi Lebanon kushindana katika michezo miwili katika dirisha la pili la kufuzu Kombe la Dunia.

Timu ya taifa ya mpira wa kikapu ya Iran 

 

Mechi yao ya kwanza ya dirisha hili itafanyika Februari 26 dhidi ya Jordan, ikifuatiwa na mchezo wao wa pili dhidi ya Syria mnamo Machi 1.

AFCON: Mvutano wa Senegal na Morocco waendelea

Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) limelaani hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Morocco dhidi ya mashabiki 18 wa Senegal waliopatikana na hatia ya kufanya vurugu kufuatia fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON. Rais wa kamati ya mawasiliano ya FSF, Bacary Cisse, amesema uamuzi huo umeleta mshangao na huzuni kubwa. “Tumesikitika na kushangazwa sana na hukumu hiyo,” alinukuliwa akisema na kuongeza kuwa, “Uamuzi huu usioeleweka umeibua hasira kali.” Mahakama ya Morocco iliwahukumu mashabiki 19 wa soka kifungo cha mwaka mmoja jela kwa vitendo vya kihuni walivyovionesha wakati wa mchezo wa fainali ya AFCON 2025 kati ya Morocco na Senegal, ambapo walijaribu kuvamia uwanja. Baada ya kikao cha mahakama kilichodumu kwa zaidi ya masaa matano, Jaji aliyekuwa akiongoza kesi hiyo aliamua kuwa mashabiki hao, raia 18 wa Senegal na mmoja wa Ufaransa, walikuwa na hatia ya zaidi ya mashtaka sita, yakiwemo ya kuharibu miundombinu ya uwanja wa michezo na kufanya vurugu wakati wa tukio la michezo. Kwa mujibu wa Wakili Naima El Guellaf, mashabiki 11 wamehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na kutozwa faini ya dola 550. Wanne wengine wamehukumiwa kifungo cha miezi sita na faini ya dola 218.

Fainali ya AFCON 2025 iliyopigwa Januari 2026

 

Na wanne waliobaki wamehukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela na faini ya dola 130. Ripoti zinasema, mmoja wa washtakiwa alizimia baada ya kusomewa hukumu. Washtakiwa hao walikamatwa mwezi uliopita baada ya mashabiki wenye hasira kujaribu kuvamia uwanja wakipinga penalti ya dakika za mwisho iliyotolewa kwa wenyeji Morocco katika fainali hiyo, ambayo Senegal iliibuka mshindi kwa bao moja sufuri. Mashabiki hao walizuiliwa rumande kwa zaidi ya mwezi mmoja wakisubiri hukumu. Katika kikao cha kesi hiyo kilichohudhuriwa na wanadiplomasia wa Senegal na Ufaransa pamoja na ndugu wa baadhi ya washtakiwa, mawakili walidai kwamba mahakama haikuwa na ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani mashabiki hao. Mwendesha mashtaka wa serikali aliiomba mahakama itoe adhabu ya juu zaidi dhidi ya mashabiki hao, akisema walivuruga utaratibu wa mechi hiyo. Alidai kwamba uharibifu uliotokea unakadiriwa kupindukia dola 476,719.

Katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, tunaarifiwa kuwa, Eberechi Eze ameimarisha tena matarajio ya Arsenal ya kutwaa ubingwa katika Ligi Kuu ya EPL kwa kuwa mwiba kwenye koo la Tottenham tena. Miezi mitatu baada ya kufunga hat-trick dhidi ya Spurs, kiungo huyo wa kati wa Uingereza alifunga mabao mengine mawili wakati Arsenal ikivuna ushindi wa mabao 4-1 ugenini Jumapili katika debi la London Kaskazini. Viktor Gyokeres pia alifunga mabao mawili na kuziba kabisa matumaini ya Spurs kwenye ngoma hiyo. Arsenal wanasalia kileleni wa EPL wakiwa na alama 61, wakifuatiwa na Machester City yenye ponti 56. Liverpool ilipata ushindi kwa mbinde wa bao 1-0 Nottingham Forest na kufikisha alama 45 wakiwa katika nafasi ya 6 jedwalini, alama sawa na Man U na Chelsea zilizoko katika nafasi ya nne na tano kwa usanjari huo. Orodha ya tatu bora kwa sasa inafungwa na Aston Villa wenye ponti 51. Binafsi kilichonivutia zaidi kwenye EPL, ni kwamba Ligi hiyo Kuu ya kandanda ya Uingereza imetangaza itasimamisha mechi ili kuwaruhusu wachezaji Waislamu kufungua saumu wakati huu wa Ramadhani. Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Uingereza, kabla ya kila mechi itaangaliwa iwapo kuna mchezaji yeyote aliyefunga, na akipatikana au watapatikana, basi mchezo utasimamishwa kwa muda mfupi wakati wa futari ili kuwawezesha kufungua saumu zao.

Huku hayo yakijiri, meneja wa timu ya Manchester City, Pep Guardiola, amejibu maoni ya mmiliki wa Manchester United, Sir Jim Ratcliffe kuhusu uhamiaji, akisema kwamba kuna haja ya "kukumbatia tamaduni zingine ili kuifanya jamii iwe bora." Shirika la habari la Uingereza PA Media limeripoti kwamba Ratcliffe, mmiliki wa hisa za waliowachache wa Manchester United, alizua utata karibuni baada ya kudai kwamba Uingereza "imekoloniwa na wahamiaji". Ratcliffe amelazimika kuomba msamaha baada ya matamshi yake kutajwa kuwa ni "ubaguzi wa rangi". Hata hivyo kocha wa Manchester City anaamini kuwa suala zima la jinsi nchi (za Magharibi) zinavyowashughulikia wahamiaji bado ni "tatizo kubwa". "Tatizo duniani kote ni kwamba tunawatambua wahamiaji au watu wanaotoka nchi nyingine kama chanzo cha matatizo ambayo nchi zetu zinapitia, na hili ni tatizo kubwa sana," amesema Pep Guardiola na kuongeza: "Kila mtu anataka maisha bora na mustakabali bora kwa ajili yake mwenyewe, familia yake, na marafiki zake. Wakati mwingine fursa zinapatikana mahali ulipozaliwa, na wakati mwingine mahali unapoweza kwenda."

Meneja wa timu ya Manchester City, Pep Guardiola

 

Kocha huyo Mhispania ameeleza kuwa: "Watu wengi hukimbia nchi zao kwa sababu ya matatizo, si kwa sababu wanataka kuondoka. Kadiri tunavyokumbatia tamaduni nyingine - kwa dhati na kwa undani - ndivyo tutakavyokuwa jamii bora." Chama cha Soka cha Uingereza hakitamshtaki Ratcliffe kutokana na matamshi yake, ambayo yalilaaniwa vikali na shakhsia wengin kote duniani, akiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, na wafuasi wa klabu hiyo.

Kwengineko, Afisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Karim Boimanda, ameeleza sababu za kuhamishwa kwa mchezo wa Dabi ya Kariakoo uliopangwa kupigwa Machi 01, 2026. Kwa mujibu wa Boimanda, dabi hiyo kati ya Yanga SC (wenyeji) dhidi ya Simba SC sasa itapigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex badala ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kama ilivyopangwa awali. Boimanda amesema uamuzi huo umefanywa kwa kuzingatia kuwa Machi Mosi, 2026, Uwanja wa Benjamin Mkapa utakuwa na matumizi mengine — ukitarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya Kimataifa ya Qur’an yatakayoshirikisha mabara yote ya dunia, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hussein Mwinyi. Uamuzi huo umeibua hisia mseto miongoni mwa mashabiki wa watani hao wa jadi.

Na kwenye ndondi, mwanamasumbwi Ryan Garcia ameshinda taji la WBC uzito wa welterweight kwa uamuzi wa pamoja, dhidi ya Mario Barrios. Garcia alimchakaza Barrios katika sekunde za kwanza Jumamosi usiku huko Las Vegas, Nevada, na kudhibiti pambano hilo kwa michanganyiko mikali. Mwanadondi huyo wa miaka 27 aliendelea kuwa mvumilivu baada ya kuangushwa mapema na akageuka kuwa mhafidhina zaidi mwishoni mwa pambano akiwa na uongozi mkubwa. Baada ya ushindi huo, Garcia amesema, ni ndoto ambayo amekuwa nayo tangu akiwa na umri wa miaka saba.

Bukayo Saka (katikati)

 

Na nikuache ukiyatafakari haya, mchezaji kinda wa Arsenal, Bukayo Saka ameingia katika orodha ya mabilione na wachezaji wanaolipwa donge nono katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Saka, 24, karibuni alisaini mktaba utakaombakisha Emirates hadi 2031, na sasa atakuwa analipwa pauni 300,000 kila wiki, kutoka 195,000 katika mkataba uliopita. Kabla ya Saka kusaini mkataba mpya, mchezaji wa Gunners aliyekuwa akilipwa kiasi kikubwa cha mshahara kwa wiki alikuwa Kai Havertz ambaye anapokea kiasi cha Pauni 280,000 kwa wiki. Earling Halaand wa Man City anasalia kileleni mwa orodha hiyo kwenye EPL kwa kulipwa pauni 525,000, akifuatiwa na Mohammad Salah wa Liverpool anayelipwa pauni laki 4 kwa wiki.

……………….TAMATI….……….