Feb 19, 2019 14:25 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (140)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Kipindi chetu cha wiki iliyopita kilizungumzia na kujadili maudhui ya ujahili lakini kikijikita zaidi juu ya ishara za ujahili na ujinga, ili kumfahamu mtu mjinga kunako mwenye akili.  Tulisema kuwa, kiburi na kujiona ni katika ishara za wazi za watu wajinga na majahili. Watu wenye akili ni mithili ya mti wenye mzigo mkubwa ambao kadiri unavyotoa matunda na mavuno basi ndivyo unavyozidi kuinama na matawi yake kuning'inia. Lakini mtu jahili au mjinga, ni mwenye kiburi na kujikweza na huona kwamba, kunyenyekea na kuwa na tawadhui ni mambo ambayo hayalingani au kwenda sambamba na hadhi na heshima yake. Aidha tulibainisha kwamba, miongoni mwa ishara nyingine za ujinga na ujahili ni mtu kutonufaika na elimu na akili yake. Sehemu hii ya 140 ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu juma hili, itazungumzia matumaini na kukata tamaa. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Katika Uislamu matumaini na matarajio au rajua ni jambo ambalo lina nafasi ya hali ya juu; kiasi kwamba, katika hadithi na riwaya za Maasumina (AS), linatajwa kuwa ni "rehma ya Mwenyezi Mungu."

Mtume (SAW) amenukuliwa akisema: Rajua na tumaini ni rehma kwa ajili ya umma wangu; na lau rajua na tumaini visingelikuweko, basi hakuna mama ambaye angemnyonyesha mwanawe na hakuna mtunza bustani ambaye angepanda mche.

Aidha imenukuliwa kuwa, Nabii Issa AS siku moja alikuwa amekaa mahala akimtazama mzee mmoja aliyekuwa akichimba ardhi kwa sururu na beleshi. Nabii Issa AS akamuomba Mwenyezi Mungu kwa kusema: Ewe Mola mlezi" mpokonye matumaini na matarajio. Mara ghafla mzee yule akaweka kando beleshi la sururu na akalala na kujinyoosha. Baada ya muda kidogo, Nabii Issa akamuuomba tena Mwenyezi Mungu kwa kusema, Ewe Mola, mrejeshee rajua na matumaini. Mzee yule mara akasimama kisha akaanza tena kuchimba ardhi. Nabii Issa akamsogelea yule mzee na kumuuliza: Nimeona hali mbili kwako. Mara ya kwanza nimekuona ukiweka kando beleshi na kuamua kulala; na katika hatua ya pili nimekuona umeamka na kuendelea na kazi hii. Sababu ni nini hasa?

Mzee yule akajibu kwa kusema: Mara ya kwanza nilifikiria kwamba, nimekuwa mzee na sina uwezo tena hivyo kwa nini najisumbua na kujipa taabu kiasi hiki. Hivyo nikaweka kando beleshi na hivyo nikalala chini.

Hata hivyo haukupita muda ikanijia fikra katika akili yangu kwamba, pengine huenda nikaishi kwa miaka mingi. Mwanadamu madhali yu hai anapaswa kufanya hima na juhudi kwa ajili ya familia yake; hivyo nikaamka na kuchukua beleshi na kuanza kufanya kazi yangu.

Kwa mujibu wa aya na hadithi ni kwamba, baada ya shirki na kumshirikisha Mwenyezi Mungu hakuna dhambi ambayo ni kubwa zaidi ya kukata tamaa na Mwenyezi Mungu. Mja aliyetenda dhambi, madhali angali si mwenye kukata tamaa na rehma na msamaha wa Mwenyezi Mungu, basi yumkini akafanya toba na kuomba maghufira na akasamehewa na Mola Muumba.

Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu.

Lakini mtu ambaye amekata tamaa katu hawezi kusamehewa, kwa sababu hana matumaini ya msamaha na maghufira ya Mwenyezi Mungu hivyo hawezi kufanya toba na kuomba maghufira. Aidha kukata tamaa na rehma na maghufira ya Mwenyezi Mungu humfanya mhusika awe na uthubutu wa kufanya dhambi zaidi. Mja wa aina hii hufanya hivyo kutokana na kujiambia mwenyewe kwamba: Mimi vyovyote itakavyokuwa nitaadhibiwa tu kutokana na madhambi yangu, basi kwa nini nisiburudike na kustadhi na ladha za dhambi nyingine. Kwa mtazamo huu finyu alionao, mhusika hufanya dhambi kwa urahisi; na kwa haraka mno hutumbikkia katika korongo la maangamizi kutokana na kuogelea katika dhambi.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu ni kuwa, muumini hawezi kupata kheri ya dunia na akhera isipokuwa kama atakuwa na dhana nzuri na matumaini na fadhila za Mwenyezi Mungu, akajipamba kwa tabia njema na akajiepusha na kuwasengenya waumini.

Watu wengi hupoteza rajua na matumaini yao pale wanapokumbwa na matatizo.  Aya ya 49 yay Surat Fussilat inasema:

Mwanaadamu hachoki kuomba dua za kheri, na inapompata shari, mara huvunjika moyo akakata tamaa.

Kwa hakika hali ya kukata tamaa na kutokuwa na matumaini haipendwi na Mwenyezi Mungu. Hii ni kutokana na kuwa, hali hiyo inamzuia mtu na kumfanya asifanye harakati.

Imam Ali bin Abi Twalib AS anaitambua balaa kubwa kabisa na madhara kwamba, yanapatikana katika hali ya mwanadamu kukata tamaa. Anasema: Balaa kubwa kabisa ni kukata tamaa.

Katika masuala ya kidini na kimaanawi pia, kuwa na matumaini ni jambo lenye nafasi mno. Katika harakati za maisha, watu ambao huweza kuyashinda matatizo yaliyowakabili ni wale wenye matumaini na Mwenyezi Mungu. Mtu mwenye matumaini na asiyekata tamaa daima huhakikisha kwamba, kazi aliyokusudia kuifanya, anaifanya na hivyo kupiga hatua katika njia ya ukamilifu wa kimaanawi.

Amirul Muumina Ali bin Abi Twalib AS anasema kuwa: Watu wenye matumaini zaidi ni wale ambao wanapoona mapungufu katika kazi zao hutaamali na kutafakari na kisha kufanya juhudi kwa ajili ya kuondoa mapungufu.

Moja ya matunda muhimu ya kuwa na rajua na matumaini, ni dua na kumuomba Mwenyezi Mungu. Ukweli wa mambo ni kuwa, mtu ambaye hana matumaini na Mwenyezi Mungu na ambaye amekata tamaa na rehma na fadhila za Mwenyezi Mungu hawezi kuomba dua.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umemalizika hivyo sina budi kukomea hapa kwa leo.

Hadi tutakapokutana tena juma lijalo, ninakuageni nikimuomba Allah atujaalie daima tuwe ni wenye kuwa na matumaini naye na atuepushe na hali ya kukata tamaa.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

Tags