Mar 07, 2019 17:10 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (143)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

 Kipindi chetu cha juma lililopita kiliendelea kuzungumzia maudhui ya hofu na matarajio na tulisema kuwa, kumuogopa Mwenyezi Mungu ni daraja miongoni mwa daraja za imani na cheo miongoni mwa vyeo vya maulama. Aidha tulielezea madhara ya kuchupa mipaka katika kumuogopa Mwenyezi Mungu ambapo tulisema kuwa, moja ya madhara ya kuchupa mipaka katika hofu na kumuogopa Mwenyezi Mungu na ambayo humzuia mwanadamu kufikia ukamilifu na saada ni kuikataa na kuipa mgongo dunia. Tulieleza pia kwamba, Uislamu umekataza na kupiga marafuku suala la mtu kujikunja na kuweka kando kila kitu na badala yake kukaa tu na kumuabudu Mwenyezi Mungu bali mbali na kufanya ibada mtu anapaswa kuwa na muda wa kutafuta maisha na riziki ya halali na kuburudika na neema halali za dunia. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 143 ya mfululizo huu kitajadili sula la “kuwafurahisha Waumini”. Karibuni.

Moja ya mambo ambayo katika Uislamu yanahesabiwa kuwa ni ibada kubwa na ambayo yameelezwa katika hadithi kwa sura tofauti ni ادخال سرور فی قلوب المومنین yaani kutia furaha katika nyoyo za Waumini au kuwafurahisha waumini.

Marhumu Muhammad bin Ya’qub al-Kulayni mwandishi wa Kitabu mashuhuri cha hadithi cha Usul al-Kafi amenukuu riwaya kutoka kwa Imam Ali bin Hussein al-Sajjad AS inayosema: Amali inayopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu ni kutia furaha katika nyoyo za Waumini.

Imam Kadhim AS amesema: Kila mwenye kumfurahisha Muumini kwanza amemfurahisha Mwenyezi Mungu, pili amemfurahisha Mtume SAW na tatu ametufurahisha sisi.

 

Aidha Mtume SAW amenukuliwa akisema:

مَنْ سَرَّ مُؤْمِناً فَقَدْ سَرَّنِی وَ مَنْ سَرَّنِی فَقَدْ سَرَّ اللَّه

 

Yaani mwenye kumfurahisha Muumini amenifurahisha mimi, na mwenye kunifurahisha mimi amemfurahisha Mwenyezi Mungu.

 

Kadhalika Imam Muhammad Baqir  AS amenukuliwa akisema:

 

مَا عُبِدَ اللَّهُ بِشَی ءٍ أَحَبَّ إِلَی اللَّهِ مِنْ إِدْخَالِ السُّرُورِ عَلَی الْمُؤْمِن

Kwa maana kwamba: Hajaabudiwa Mwenyezi Mungu kwa kitu kinachopendwa na mbele ya Mola Muumba kama kumfurahisha Muumini.

Kwa hakika hadithi tulizotangulia kuzisoma zinaonyesha ni jinsi suala la kumfurahisha Muumini lilivyopewa umuhimu katika dini tukufu ya Uislamu.

Miongoni mwa thamani za kimaadili ambazo zimekokotezwa na kutiliwa mkazo mno katika Uislamu ni suala la kuwafurahisha Waumini na waja wa Mwenyezi Mungu.  Kitendo hiki kinafuatiwa na kuwafurahisha Mitume, Maimanu na hatimaye ni kupata radhi za Mwenyezi Mungu Jalla jalali. Hii ni kutokana na kuwa, wakati mtu anapokuwa pamoja na wengine katika furaha, ghamu na huzuni zao huziteka nyoyo zao na wakati huo huwa karibu na Mwenyezi Mungu.

Qur'ani Tukufu

Imam Ja’afar bin Muhammad al-Swadiq AS amenukuliwa akisema kuwa: Endapo mmoja kati yenu atamfurahisha ndugu yake Muumini, asidhani kwamba, amemruhaisha yeye tu. Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, ametufurahisha sisi na ninaapa kwa Allah kwamba, furaha hii imeingia pia katika moyo wa Bwana Mtume SAW.

Kwa hakika ادخال سرور فی قلوب المومنین yaani kutia furaha katika nyoyo za Waumini au kuwafurahisha waumini inajumuisha kila kitendo ambacho huwa sababu ya kupatiwa ufumbuzi matatizo ya watu na kuwafurahisha. Kama vile kuwapatia watu chakula, kuwasaidia masikini, kumtatulia mtu shida yake, kumfikisha mtu alipokusudia kwenda baada ya kukwama njiani, kumkopesha mtu na mambo mengine mfano wa hayo ambayo humuondoa mtu katika hali ya ghamu na huzuni na kumfurahisha. Thawabu ya amali kama hizi sio tu huwa sababu ya kheri na baraka, bali amali hizi huwa na faida kubwa kwa aliyezifanya huko akhera.

Katika baadhi ya hadithi, kumfurahisha Muumini au kutia furaha katika nyoyo za Waumini kunatajwa kuwa ibada bora kabisa baada wa ibada ya Swala. Hata hivyo makusudio ya kumfurahisha Muumini ni kumfurahisha na vitu ambavyo kimsingi ni halali na havina dhambi na maasi ndani yake.

Bwana wa Mashahidi Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS anasema:

 أَفْضَلُ الْأَعْمَالِ بَعْدَ الصَّلَاةِ إِدْخَالُ السُّرُورِ فِی قَلْبِ الْمُؤْمِنِ بِمَا لَا إِثْمَ فِیه

 

Amali bora kabisa baada ya Swala ni kutia furaha katika moyo wa Muumini kwa mambo ambayo hayana dhambi ndani yake.

 

Wapenzi wasikilizaji, jamii yenye nishati ni jamii ambayo ina ustawi na uhai na watu wa jamii hiyo hakuna wakati ambao wanafanya juhudi za kufanya uharibifu, kufanya matendo ambayo ni uvurugaji mambo, yasiyo na mipango, mizozo, mapigano na mambo mengine yanayoleta hali ya ukosefu wa utulivu katika jamii, bali daima hufanya hima na idili kwa ajili ya kuleta utulivu kwa ajili yao na kwa ajili ya watu wengine katika jamii wanayoishi. Katika jamii yenye furaha, wanajamii huwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu. Kwa hakika mwanadamu kulingana na fitra na maumbile yake siku zote ni mwenye kutafuta furaha, na Uislamu umeunga mkono na kuidhinisha furaha hii. Hata hivyo, kuleta furaha kwa wengine haina maana tu ya kuwafanya watu  hao wacheke.

Hadithi ya Uongofu

Inasimuliwa kwamba, siku moja Imam Ali bin Abi Twalib AS akiwa pamoja na maswahaba zake walipita katika eneo moja. Mara akatokea Bwana mmoja na kunyakua joho la Imam Ali AS na kisha akakimbia. Baadhi ya watu waliokuwa pamoja na Imam Ali AS wakamkimbiza Bwana yule mpaka wakamkamata na kisha wakamleta mbele ya Imam pamoja na joho alilonyakua. Imam Ali AS akamuashiria bwana yule na kuuliza: Ni nani huyu? Wakamjibu  Bwana huyu ni muigizaji na mchekeshaji ambaye huwafurahisha wakazi wa mji wa Madina kwa vitendo vyake vya uchekeshaji. Imam Ali AS akasema: Mwambieni, Mwenyezi Mungu ana siku ambapo katika siku hiyo watu wa kazi na vitendo vya uchekeshaji na kazi batili na zisizo na maana watafahamu kwamba, mikono yao iko mitupu (hawana kitu).

Kupitia kisa hiki tunafahamu kwamba, kuwafurahisha Waumini hakuna maana ya kuwachekesha watu kwa mbinu na njia za kibatili na zisizo sahihi. Bali makusudio ni kila amali na kitendo ambacho kinampa furaha ya kweli Muumini. 

Katika hali ya kawaida, wakati mtu anapokuwa na furaha, uso wake huwa na bashasha na tabasamu na kudhihiri furaha hii kuna thamani mno kiasi kwamba, Imam Hussein AS amenukuliwa akinukuu hadithi kutoka kwa Bwana Mtume SAW inayosema:

أَفْضَلُ الْأَعْمَالِ بَعْدَ الصَّلَاةِ إِدْخَالُ السُّرُورِ فِی قَلْبِ الْمُؤْمِنِ بِمَا لَا إِثْمَ فِیه

Amali bora kabisa baada ya Swala ni kutia furaha katika moyo wa Muumini kwa mambo ambayo hayana dhambi ndani yake.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu cha Hadithi ya Uongofu umefikia tamati kwa leo, basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo ninakuageni nikukutakieni furaha na bashasha maishani.

Wassalaamu Alaykumu Warahmatullahi Wabarakaatuh…..

Na Salum Bendera