Alkhamisi, 04 Aprili, 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe 28 ya mwezi Rajab 1440 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 4 Aprili 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1380 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, msafara wa Imam Hussein bin Ali (as), ulianza safari yake kutoka mjini Madina. Hatua hiyo ilitanguliwa na kuaga dunia Muawiya bin Abi Sufiyan hapo tarehe 15 ya mwezi huo huo wa Rajab na kuchukua mahala pake mwanaye, Yazid bin Muawiya. Yazidi alimtaka mtawala wa Madina kumlazimisha Imam Hussein atoe baia kwake na endapo angekataa, basi amuue. Hata hivyo kwa kuzingatia kuwa, Imam Hussein alikuwa akifahamu vyema kuwa Yazidi ni muovu na fasiki, alikataa kutoa baia hiyo na hivyo akaamua kuondoka mjini Madina kuelekea Makka, akiwa na watu wa familia ya Mtume na idadi kadhaa ya wafuasi wake. ***

Katika siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, sawa na tarehe 28 Rajab mwaka 1337 Hijria, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Muhammad Kadhim Tabatabai Yazdi maarufu kwa jina la Allamah Yazdi, msomi mashuhuri wa Kiirani. Allamah Yazdi alijipatia elimu yake ya kidini nchini Iran na huko Najaf nchini Iraq, kutoka kwa maulamaa kadhaa mashuhuri akiwemo Mirza Shirazi na kufikia daraja ya Ijtihad. Msomi huyo aliandika vitabu vingi, kikiwemo kitabu cha 'al U'rwatul Wuthqa. ***

Katika siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, nchi ya Senegal inayopatikana magharibi mwa Afrika ilipata uhuru. Senegal ilikuwa chini ya ushawishi na ukoloni wa Wareno kuanzia karne ya 15 Miladia na kuanzia karne ya 17 pia Wafaransa nao walianza kuiba maliasili na utajiri wa nchi hiyo. Senegal iko katika pwani ya bahari ya Atlantic ikipakana na Mauritania, Mali na Guinea Bissau. ***
Miaka 51 iliyopita katika siku kama ya leo Martin Luther King kiongozi wa mapambano ya raia weusi wa Marekani aliuawa kwa kupigwa risasi na mtu mmoja au watu kadhaa wasiojulikana. Martin Luther alizaliwa mwaka 1929 katika mji wa Atlanta huko Marekani. Alipata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Boston na baadae akaanza kuongoza harakati ya ukombozi ya Wamarekani weusi dhidi ya ubaguzi wa rangi waliokuwa wakifanyiwa raia weusi nchini Marekani. Katika kipindi hicho, raia weusi wa Marekani waliasisi harakati ya nchi nzima ya kupinga ubaguzi wa rangi na vilevile katika kulalamikia sheria iliyokuwa ikiitambua jamii ya wazungu kama watu wa daraja ya juu huko Marekani. Kwa mujibu wa baadhi ya ushahidi ni kuwa shirika la ujasusi la Marekani CIA lilihusika katika mauaji hayo. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, Zulfiqar Ali Bhutto, Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan alinyongwa. Bhutto ambaye alikuwa mwasisi wa Chama cha Wananchi alikuwa Rais wa Pakistan mwaka 1971. Mwaka 1977 Jenerali Muhammad Dhiaul Haq alifanya mapinduzi na kumuondoa madarakani Bhutto akimtuhumu kwa kufanya mauaji na kuisaliti Pakistan. Hatimaye tarehe 4 Aprili mwaka 1979 Zulfiqar Ali Bhutto alinyongwa, licha ya viongozi wa baadhi ya nchi duniani kutaka asamehewe. ***