Alkhamisi, tarehe 11 Julai, 2019
leo ni Alkhamisi tarehe 8 Dhulqaada 1440 Hijria sawa na tarehe 11 Julai 2019.
Siku kama ya leo miaka 1092 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Iraq Ibn Zubair, mwandishi mashuhuri wa Kiislamu wa wakati huo. Katika ujana wake Ibn Zubair alisoma kwa baba yake elimu muhimu tofauti za wakati huo. Baada ya baba yake kufariki dunia aliutumia utajiri wa baba yake huyo katika njia ya kutafuta elimu, kuasisi maktaba na kuwasaidia wanafunzi wa kidini waliokuwa na hali ngumu ya kimaisha. Mbali na uhodari mkubwa katika uandishi, Ibn Zubair alikuwa na kipawa pia cha kuandika upya baadhi ya vitabu vya wasomi wengine na kuvieneza.
Siku kama ya leo miaka 1061 iliyopita, alifariki dunia Abu Hamid Swaghani, mtaalamu wa nujumu na hesabati wa Iran. Abu Hamid alizaliwa mjini Khurasan, kaskazini mashariki mwa Iran, na baadaye kuhamia mjini Baghdad Iraq. Msomi huyo alihesabika kuwa mmoja wa wasomi wakubwa katika uga wa elimu ya nujumu na hisabati wa zama zake sanjari na kuasisi kituo cha unajimu mjini Baghdad. Msomi huyo ameacha vitabu vingi katika fani ya nujumu.
Katika siku kama ya leo miaka 1055 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Ali bin Omar Dar Qutni, mwandishi na mtaalamu wa sheria za Kiislamu. Dar Qutni alifanya safari nchini Misri na Sham na kupata elimu kwa wasomi wakubwa wa zama hizo. Msomi huyo alikuwa hodari katika tafsiri ya Qur’ani Tukufu, fiq’hi, mashairi na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na vitabu vya ‘al-Sunan’, ‘Sunan Dar Qutni’ na ‘al-Mukhtalif Walmu’talif.’
Siku kama ya leo miaka 775 iliyopita, mji wa Baitul Muqaddas ulikombolewa na Waislamu wakati wa Vita vya Msalaba. Vita vya Msalaba vilianza mwishoni mwa karne ya 11 Miladia na watu wa Ulaya waliwatwisha Waislamu vita hivyo. Watu wa msalaba walianzisha vita hivyo kidhahiri wakiwa na lengo la kuteka Baitul Muqaddas, ingawa shabaha halisi ya wapiganaji hao ilikuwa ni kudhibiti ardhi kubwa za Waislamu na kuwanyonya na kuwakoloni wafuasi wa dini hiyo. Katika vita hivyo wafuasi wa kanisa walichora alama za msalaba kwenye mabega na mavazi yao, na kwa sababu hiyo vita hivyo vimekuwa maarufu kwa jina la Vita vya Msalaba.
Miaka 462 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Sebastian Cabot mvumbuzi na mwanabaharia wa Kiitalia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 81. Tangu awali alikuwa akifanya safari na baba yake aliyekuwa mwanabaharia na kwa msingi huo akafanikiwa kujifunza mambo mengi yanayohusiana na ubaharia.
Miaka 98 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Mongolia ilijitangazia uhuru. Mongolia ina historia kongwe mno. Changiz Khan Moghol alianza kuziteka ardhi za nchi hiyo mwanzoni mwa karne ya 13 na kusonga mbele hadi Ulaya ya mashariki. Mongolia iligawanyika katika sehemu mbili yaani Mongolia ya nje na ya ndani baada kusambaratika utawala wa kifalme wa Wamogholi. Mongolia ya ndani iliijumuisha China, na Mongolia ya Nje ikawekwa chini ya udhibiti wa China mwishoni mwa karne ya 17.
Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, Waislamu zaidi ya elfu nane wa mji wa Srebrenica mashariki mwa Bosnia Herzegovina waliuawa kwa umati. Mauaji hayo yalifanywa na Waserbia wenye misimamo mikali. Maafa hayo yalikuwa mauaji makubwa zaidi ya halaiki kuwahi kutokea barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Wanamgambo wa Kiserbia wakiungwa mkono na serikali ya Belgrade, waliuvamia mji wa Srebrenica licha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulitangaza eneo hilo kuwa la amani mwaka 1993 na kutumwa askari wa umoja huo katika mji huo. Waislamu wa mji wa Srebrenica walijaribu kuondoka katika mji huo, lakini watenda jinai wa Kiserbia waliwauwa wanaume na watoto wao wa kiume na kuwaruhusu wanawake kuondoka katika mji huo. Wakati wa mauaji hayo ya kimbari, wanajeshi wa kulinda amani wa Uholanzi waliokuweko katika eneo hilo hawakuchukua hatua yoyote ya kuwahami Waislamu hao wa Srebrenica.