Jumanne tarehe 20 Agosti 2019
Leo ni Jumanne tarehe 18 Dhulhija 1440 Hijria sawa na 20 Agosti mwaka 2019.
Siku kama hii ya leo miaka 1430 iliyopita Mtume Muhammad (SAW) akiwa katika safari yake ya mwisho ya Hija, kwa amri ya Mwenyezi Mungu alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib AS kuwa kiongozi wa Waislamu wote baada yake. Hatua hiyo ya Mtume Mtukufu ilifanyika katika eneo linalojulikana kwa jina la Ghadir Khum katika makutano ya njia ya Makka na Madina. Siku hiyo Mtume SAW alitoa hotuba mbele ya hadhara kubwa ya Waislamu kisha akashika mkono wa Ali bin Abi Twalib na kusema: "Kila mtu ambaye mimi ni kiongozi wake basi huyu Ali pia ni kiongozi wake. Mwenyezi Mungu ampende atakayempenda, na amfanyie uadui atakayemfanyia uadui." Mtume SAW pia aliwausia Waislamu kushikamana na Qur'ani na Ahlubaiti wake na akasema viwili hivyo havitatengana hadi vitakapomkuta yeye katika Hodhi ya Kauthar, Siku ya Kiyama.

Siku kama ya leo miaka 768 iliyopita, alifariki dunia Nasiruddin Tusi, mwanafalsafa, mtaalamu wa hesabati na nujumu na msomi mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Tus, kaskazini mashariki mwa Iran. Nasiruddin Tusi aliishi katika kipindi cha Hulagu Khan Mongol na aliasisi kituo kikubwa na cha kwanza cha sayansi ya nujumu huko Maraghe kaskazini magharibi mwa Iran. Nasiruddin Tusi ameandika vitabu zaidi ya 80 kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi. Vitabu muhimu zaidi vya msomi huyo ni pamoja na ‘Asasul-Iqtibaas’, ‘Akhlaaq Naaswiri’, ‘Awsaful-Ashraaf’ na ‘Sharhul Ishaarat.

Tarehe 18 Dhulhija miaka 226 iliyopita alizaliwa faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Murtadha Ansari katika mji Dezful nchini Iran na baada ya kupata elimu ya msingi kwa baba yake alielekea katika miji mitakatifu ya Karbala na Najaf huko Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Miaka kadhaa baadaye Sheikh Ansari alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni na walimu mashuhuri wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Rasaail na Makaasib ambavyo vingali vinatumiwa hadi sasa kufundishia katika vyuo vikuu vya kidini.

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, yaani Agosti 20 mwaka 1998 Marekani ilizishambulia kwa makombora ya masafa marefu nchi za Sudan na Afghanistan. Serikali ya Washington ilidai kwamba, watu walioshiriki katika kulipua kwa mabomu balozi za Marekani mjini Dar es Salaam, Tanzania na Nairobi, Kenya wiki mbili kabla, walikuwa na uhusiano na nchi hizo. Washington pia ilidai kuwa ilikishambulia kwa mabomu kiwanda cha kuzalisha madawa cha ash-Shifaa nchini Sudan kwa sababu eti kilikuwa kikitengeneza mada za kemikali. Hata hivyo weledi wa masuala ya kisiasa walisema kwamba, sababu ya Marekani kufanya mashambulio ya mabomu dhidi ya Sudan na Afghanistan ilikuwa ni kujaribu kufunika fedheha ya kimaadili iliyokuwa ikimkabili Rais wa nchi hiyo Bill Clinton. Kwa sababu hiyo mashambulizi hayo yaliamsha hasira za fikra za walio wengi na serikali nyingi duniani dhidi ya siasa za kutumia mabavu na kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani.
Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita Marekani ilikiri kwamba ilifanya makosa kuishambulia ndege ya abiri ya Iran hapo tarehe 3 Julai mwaka 1988. Siku hiyo ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege ya Iran iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas kusini mwa Iran na kuelekea Dubai Umoja wa Falme za Kiarabu ilishambuliwa kwa makombora mawili kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi. Manowari ya kijeshi ya Marekani USS Vincennes ilifyatua makombora hayo na kuuaa shahidi watu 298 waliokuwemo. Shambulio hilo lilionyesha wazi unyama wa serikali ya Marekani na ukatili wake hata kwa wanawake na watoto wadogo waliokuwemo ndani ya ndege hiyo. Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho kilichoonekana na serikali ya Washington kuwa eti ni cha kishujaa.
