Ijumaa tarehe 4 Oktoba 2019
Leo ni tarehe 5 Safar 1441 Hijria sawa Oktoba 4 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 1380 iliyopita Ruqayyah binti mdogo wa Imam Hussein bin Ali (as) alikufa shahidi akiwa huko Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyya. Ruqayyah ambaye pia anajulikana kwa jina la Fatima binti Hussein (as) alikuwa binti wa mwisho wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) kutoka kwa mkewe, Ummu Is’haq binti Twalha. Wanahistoria wanasema mtoto huyo alikuwa na umri wa miaka 3, 4 au 7. Mtoto huyo alikuwa akimpenda sana Imam Hussein na aliandamana naye pamoja na familia yake katika medani ya Karbala. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, ndugu na masahaba wa Imam, Ruqayya alikamatwa mateka na askari wa Yazid akiwa pamoja na watu wengine wa Nyumba ya Mtume na kupelekwa Sham. Huko alikuwa akilia mchana usiku. Wahistoria wanasema mtawala Yazidi aliamuru kichwa cha Imam Hussein kipelekwe na kutupwa mbele ya binti huyo mdogo ambaye alilia na kuzimia kisha akakata roho.

Siku kama ya leo miaka 189 iliyopita, Ubelgiji ilijitangazia uhuru wake. Mwanzoni mwa karne ya 18 Ubelgiji ilikuwa chini ya udhibiti wa Austria, huku ikidhibitiwa na Ufaransa mwishoni mwa karne hiyo hiyo. Hata hivyo baada ya Napoleon Bonaparte kushindwa na madola ya Ulaya, mwaka 1815 Ubelgiji na Uholanzi ziliunda muungano. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa muda mrefu kufuatia Wabelgiji wa Kikatoliki kuanzisha uasi dhidi ya Waholanzi wa Kiprotestanti na hivyo kuamua kujitangazia uhuru wao katika siku kama ya leo.
Katika siku kama ya leo miaka 91 iliyopita tabibu Alexander Fleming alivumbua dawa ya penicillin. Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu nchini Uingereza, alizaliwa tarehe Sita Agosti mwaka 1881 katika familia ya wakulima mjini Lochfield farm, magharibi mwa Scotland. Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria wa maambukizi kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasi wasi mkubwa. Miaka 10 baada ya kumalizika vita, sawa na tarehe Nne Oktoba mwaka 1928 Miladia, Fleming alifanikiwa kuvumbua dawa ya penicillin, ambayo huua vijidudu vya maambukizi kwenye kidonda.
Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita satalaiti ya kwanza ilirushwa angani na msomi wa Urusi ya zamani na kwa utaratibu huo zama za udhibiti wa anga zikawa zimeanza. Satalaiti hiyo iliyopewa jina la Sputniki 1 ilizunguka dunia mara 1400 kwa siku 92 na kwa mara ya kwanza ikafikisha ujumbe wa radio kutoka angani kuelekea ardhini.
Na siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, Serikali ya Kuwait haikutoa idhini ya Imam Khomein kuishi nchini humo na hivyo kulazimika kuelekea nchini Ufaransa. Hatua ya Imam kuelekea Paris, ilikuwa sababu ya kuharakisha mwenendo wa mafanikio ya Mapinduzi nchini Iran, kinyume kabisa na matarajio ya dikteta Saddamwa Iraq na Mohammad Reza Pahlavi, mfalme kibaraka wa wakati huo wa Iran ambao waliamini kwamba kwa kumbaidisha Imam Khomein (MA) wangekuwa wameua harakati zake za kimapinduzi. Akiwa mjini Paris, Imam aliishi katika kijiji kilichoitwa Neauphle-le-Château, kilometa 50 kutoka mji huo, ambapo aliendeleza harakati zake za kimapinduzi kupitia barua na kanda za sauti kwa wanamapinduzi nchini Iran.
