Feb 11, 2020 04:40 UTC
  • Jumanne, tarehe 11 Februari, 2020

Leo ni Jumanne tarehe 16 Jamadithani 1441 Hijria sawa na 11 Februari 2020.

Siku kama ya leo miaka 2680 iliyopita mfalme wa kwanza wa Japan maarufu kwa jina la Jimmu alishika madaraka ya nchi. Kwa utaratibu huo mfumo wa kale zaidi na uliobakia kwa kipindi kirefu wa kifalme dunia ambao unaendelea hadi sasa, ulianzishwa. Wafalme wa Japan huwa na cheo cha heshima tu na Waziri Mkuu ndiye kiongozi wa masuala ya nchi.

Japan

Miaka 1020 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Ibn Darraj Qastalli mshairi na mwandishi mwashuhuri wa Andalusia. Ibn Darraj alizaliwa mwaka 347 Hijiria na alikuwa miongoni mwa washairi wakubwa wa Andalusia huko kusini mwa Uhispania ya leo. Pia alikuwa na nafasi muhimu katika kukuza mashairi ya Kiarabu mwishoni mwa karne ya 4 na mwanzoni mwa karne ya 5 Hijiria. Ibn Darraj ndiye aliyeleta mtindo mpya wa mashairi ya Kiarabu huko Andalusia na mashairi yake mbali na kuwa na thamani ya kifasihi na kisanaa pia yanahesabiwa kuwa chanzo cha kuaminika kinachoonyesha matukio ya wakati huo ya Uhispania.

Tarehe 11 Februari miaka 41 iliyopita Iran ilikuwa katika siku ya kihistoria itakayokumbukwa siku zote. Siku hiyo wananchi waliokuwa wakipiga takbira na kutoa nara za kimapinduzi chini ya uongozi wa Ayatullah Ruhullah Khomeini walihitimisha kipindi cha giza totoro katika historia ya Iran kwa kuung'oa madarakani utawala wa kidikteta wa Shah Pahlavi. Wananchi wanamapinduzi wa Iran, wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee na watu wa matabaka yote walisimama kidete wakipambana na mizinga na vifaru vya jeshi la Shah na kujisabilia kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu. Mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran yalienea nchini kote huku wafuasi wa Imam Ruhullah Khomeini wakiwa katika juhudi za kumaliza kabisa mabaki ya utawala wa kidhalimu wa kifalme. Wakati ilipotangazwa habari kwamba vifaru vya majeshi ya Shah vilikuwa njiani kuelekea Tehran kwa ajili ya kukandamiza harakati za mapinduzi zilizokuwa zinaelekea kileleni, wananchi wa miji mbalimbali walijitokeza na kupambana na majeshi hayo huku wakifunga njia na kuzuia misafara ya vifaru hivyo. Baadhi ya makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Shah waliuawa na wananchi katika mapambano hayo na kulilazimisha jeshi kutopendelea upande wowote. Siku hiyo pia wananchi wanamapinduzi walitwaa Shirika la Redio na Televisheni la Iran kutoka kwenye udhibiti wa jeshi. Muda mfupi baadaye lilitolewa tangazo katika redio ya taifa likitangaza kwamba "Hii ni Sauti ya Mapinduzi ya Kiislamu". Sauti hiyo ilitangaza ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuporomoka utawala wa kidhalimu wa kifalme uliotawala Iran kwa kipindi cha miaka 2500.

پیروزی شکوهمند انقلاب اسلامی ایران

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita Mzee Nelson Mandela kiongozi wa harakati za kupambana na ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini aliachiwa huru baada ya kufungwa jela kwa kipindi cha miaka 27. Mandela alikamatwa mwaka 1963 na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa sababu ya mapambano yake dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini. Mwaka 1991 alifikia makubaliano na makaburu wa nchi hiyo juu ya jinsi ya kukomesha utawala wa ubaguzi wa rangi na miaka kadhaa baadaye yaani mwaka 1994 alichaguliwa kuwa rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini.

Nelson Mandela

Siku kama ya leo miaka 9 iliyopita Hosni Mubarak aliyekuwa amejitangaza Rais wa maisha wa Misri aliondolewa madarakani kwa mapinduzi ya wananchi. Mubarak ambaye awali alikua makamu wa Rais Anwar Saadat wa Misri alishika madaraka ya nchi mwaka 1981 baada ya kuuawa kiongozi wa nchi hiyo. Saadat aliuawa kwa kumiminiwa risasi na Khalid Islanbuli kutokana na kutia saini makubaliano ya Camp David na utawala ghasibu wa Israel na kusaliti malengo ya taifa la Palestina. Baada ya kushika madaraka Mubarak alifuata nyayo za Saadat na hadi anang'olewa madarakani alikuwa kibaraka na mtekelezaji mkubwa wa siasa za Marekani na waitifaki wake katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika.

Tags