Mar 04, 2020 02:48 UTC
  • Jumatano tarehe 4 Machi 2020

Leo ni Jumatano tarehe 9 Rajab 1441 Hijria saw ana tarehe 4 Machi mwaka 2020.

Katika siku kama ya leo miaka 53 iliyopita sawa na tarehe 14 Esfand mwaka 1346 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, alifariki dunia Dakta Muhammad Musaddiq, Waziri Mkuu na mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa Iran. Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1261 Hijria Shamsia. Mwaka 1299 Hijria Shamsia ikiwa ni baada ya kuhudumu kama Waziri wa Fedha na Waziri wa Mambo ya Nje, Musaddiq alichaguliwa kuwa mwakilishi wa watu wa Tehran bungeni. Alifanya jitihada kubwa za kutaifishwa sekta ya mafuta nchini Iran na mwaka 1329 Hijria Shamsia alifanikiwa kupasisha kanuni ya kutaifishwa mafuta bungeni kwa himaya ya makundi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Ayatullah Kashani. Baadaye aliondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyoongozwa na Marekani tarehe 28 Mordad mwaka 1332 Hijria na kufungwa jela miaka mitatu. Baada ya kutumikia kifungu hicho Musaddiq alibaidishiwa katika kijiji kimoja huko magharibi mwa Tehran na alifariki dunia miaka kadhaa baadaye katika siku kama ya leo.

Dakta Muhammad Musaddiq

Siku kama ya leo miaka 133 iliyopita, alifariki dunia msomi mkubwa na mujtahidi wa Kishia Ayatullah Muhammad Hassan Aal Yaasin Kadhimi. Ayatullah Aal Yaasin alizaliwa mwaka 1220 Hijiria mjini Kadhimiya, Iraq. Masomo yake ya awali alisoma katika mji alikozaliwa na baada ya hapo alifanya safari nchini Iran na kisha Karbala na kusoma kwa maulama wakubwa akiwemo Sheikh Muhammad mwandishi wa vitabu vya Fusuul. Baadaye alielekea mjini Najaf na kusoma pia kwa maulama wakubwa akiwemo Sheikh Muhammad Hassan Najafi mwandishi wa kitabu cha Jawaahir na wengineo. Baada ya hapo Ayatullah Muhammad Hassan Aal Yaasin alichukua uongozi wa chuo cha Kadhimiya na kujishughulisha na kazi ya kutoa elimu na kulea wanafunzi. Vitabu vya 'Asraarul-Faqahah', 'Hashiyatul-Fusuul' na 'ufafanuzi wa kitabu cha Fawaaidul-Usuul' ni miongoni mwa athari za msomi huyo.

Siku kama ya leo miaka 172 iliyopita, yalianza mapambano ya wapigania uhuru wa Hungary dhidi ya serikali ya Austria. Siasa za kibeberu za Klemens Metternich, Kansela wa wakati huo wa Austria zilisababisha mapinduzi mwaka 1848 katika ardhi zisizo za Ujerumani zilizokuwa chini ya himaya ya Austria, ikiwemo Hungary. Uasi wa wananchi wa Hungary ulioibuka kutokana na dhulma ya Waaustria, ulienea kwa kasi kote nchini humo. Licha ya kutishiwa na serikali kuu, wanamapinduzi walitangaza nchi hiyo kuwa jamhuri tarehe 4 mwezi Aprili mwaka 1849 baada ya kushtadi harakati zao huko Hungary. Hata hivyo kwa msaada wa utawala wa Tsar wa Urusi, ufalme wa Austria uliyakandamiza mapinduzi hayo na kuwanyonga viongozi wake.

Tarehe 4 Machi miaka 197 iliyopita, vikosi vya jeshi la Ugiriki vilifanya mauaji makubwa dhidi ya Waislamu wa ufalme wa Othmania kwa kuwaua kwa halaiki Waislamu elfu 12 katika mji wa Tripolitsa. Makundi ya Wagiriki waliokuwa wakiungwa mkono na nchi kadhaa za Ulaya, yaliungana na kutekeleza mauaji hayo katika muongo wa mwanzoni mwa karne ya 19, yaani mwaka 1822. Kufuatia mauaji hayo mwezi Novemba mwaka 1824 majeshi ya Kiislamu yaliamua kulipiza kisasi dhidi ya Wagiriki.

Siku kama ya leo miaka 478 iliyopita aliaga shahidi Izzud-Din Sayyid Hussein, mmoja wa maulama wa karne ya 10 Hijiria. Sayyid Hussein alizaliwa mwaka 906 Hijiria katika moja ya vijiji vya mji wa Jabal Amel nchini Lebanon na kuanza kusoma elimu za wakati huo ambapo alifanikiwa kufikia daraja za juu katika elimu ya Irfan. Hatimaye watu wenye chuki ambao hawakuvumilia kuona shakhsia tukufu ya kimaanawi na kidini ya msomi huyo walimuua kwa sumu katika siku kama ya leo.

Siku kama ya leo miaka 520 iliyopita, alizaliwa Abdi Bik Shirazi, mtaalamu mkubwa wa historia wa Iran maarufu kwa jina la Navidi, huko mjini Shirazi. Abdi Bik Shirazi alikuwa miongoni mwa waandishi wa historia ya Tahmasp Safavid, huku akiwa na utaalamu pia katika elimu ya fasihi. Athari kubwa ya mwanahistoria huyo ni kitabu kinachozungumzia silsila ya utawala wa Safavid nchini Iran. Katika kitabu hicho Abdi Bik Shirazi alifafanua habari za utawala huo kuanzia mwaka 978 Hijiria.