Mar 17, 2020 01:42 UTC
  • Jumanne tarehe 17 Machi 2020

Leo ni Jumanne tarehe 22 Rajab 1441 Hijria inayosadifiana na tarehe 17 Machi mwaka 2020.

Miaka 1384 iliyopita inayosadiafina na leo, ardhi ya Baitul Muqaddas huko Palestina ilikombolewa na Waislamu. Vita vya kwanza kati ya Waislamu na Warumi vilijiri huko kaskazini mwa Bahari Nyekundu baada ya kudhihiri Uislamu. Jeshi la Waislamu lilitoa pigo kwa Warumi na eneo la kusini mwa Palestina likakombolewa katika zama za utawala wa Umar bin Khattab. Baada ya kushindwa huko, mfalme wa Roma alituma jeshi kubwa katika ardhi za Palestina. Warumi walishindwa vibaya na jeshi la Kiislamu katika vita vilivyojiri huko Palestina na mwishoni mwa mapigano hayo, kamanda wa jeshi la Roma aliuawa na Damascus ikadhibitiwa na Waislamu.

Baitul Muqaddas

Siku kama ya leo miaka 223 iliyopita, inayosadifiana na 22 Rajab 1228 Hijria, alifariki dunia Allamah Sheikh Jaafar Kaashiful Ghitwa, mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu mjini Najaf, Iraq. Allamah Kashiful Ghitwa alikuwa mwanachuoni aliyebobea kwenye taaluma mbalimbali za kielimu kama fiqhi, usulul fiqh, tafsiir ya Qur'ani na Hadith. Mwanachuoni huyo ameandika vitabu vingi vikiwemo, Kashful Ghitwaa na al A'qaaidul Jaafariyya.

Allamah Sheikh Jaafar Kaashiful Ghitwa

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, wawakilishi wa nchi za Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi na Luxembourg, walitia saini mkataba  wa ushirikiano mjini Brussels, Ubelgiji. Katika mkataba huo uliojulikana kwa jina la "Mkataba wa Brussels", nchi hizo zilikubaliana kuanzisha mfumo wa ulinzi wa pamoja na kupanua uhusiano wao wa kiuchumi na kiutamaduni.  Mkataba huo pia ndio uliokuwa chachu ya kuanzishwa kwa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO. Kwani ni baada ya hapo ndipo yalipofanyika mazungumzo kati ya Marekani, Canada na baadhi ya nchi wanachama wa Mkataba wa Brussels huko Washington, Marekani ambapo baadaye kuliundwa Shirika hilo la NATO mwezi Aprili 1949.

NATO