Jun 20, 2020 04:27 UTC
  • Jumamosi tarehe 20 Juni 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 28 Shawwal 1441 Hijria sawa na Juni 20 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 968 iliyopita alizaliwa Majdud ibn Ādam mashuhuri kwa jina la Sanai Ghaznavi, malenga, tabibu na mwanairfani mkubwa wa Iran mjini Ghazni. Ghaznavi alianza kusoma mashairi ya kuwasifu watawala akiwa bado kijana mdogo. Hata hivyo muda mfupi baadaye aliachana na mwenendo huo na kuanza kusomea elimu ya irfan (ya kumjua Mwenyezi Mungu). Kuanzia wakati huo alianza kuishi maisha ya kuwatumikia wananchi sambamba na kusoma mashairi ya kuwakosoa watawala dhalimu na mafisadi. Alianzisha pia mfumo wa aina yake katika usomaji wa mashairi. Miongoni mwa athari za Sanai Ghaznavi ni pamoja na kitabu cha 'Hadiqatul-Haqiqah' ambacho kina muundo wa mashairi na ndani ya kitabu hicho malenga huyo mkubwa ameweka wazi fikra zake za kimaadili na irfani. Vitabu vya 'Elahi Nameh' 'Karnameh Balkh' na 'Twariqut-Tahqiq,' ni miongoni mwa athari za Sanai Ghaznavi.

Sanai Ghaznavi

Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita inayosadifiana na hii ya leo yaani tarehe 20 mwezi Juni mwaka 1875, kisiwa cha Okinawa kinachopatikana katika Bahari ya Pacific huko Japan kilidhibitiwa na jeshi la nchi hiyo. Hata hivyo mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia kisiwa hicho cha kistratijia chenye ukubwa wa kilomita mraba 1250 kilikaliwa kwa mabavu na majeshi ya Marekani licha ya mapambano makali ya jeshi la Japan. Jeshi la Marekani liliondoka Japan mwaka 1958 lakini kisiwa cha Okinawa kiliendelea kudhibitiwa na Wamarekani. Mwaka 1972 vikosi vya Marekani vilisitisha ukaliaji wa mabavu wa kisiwa hicho kufuatia mazungumzo marefu kati ya Washington na Tokyo.

Kisiwa cha Okinawa, Japan

Miaka 108 iliyopita katika siku kama ya leo msomi wa Poland kwa jina la Casimir Funk kwa mara ya kwanza kabisa alifanikiwa kugundua vitamin au virutubisho. Baada ya uhakiki mwingi Dakta Casimir Funk aligundua kwamba vyakula vinavyotumiwa na mwanadamu vina baadhi ya virutubisho (vitamins) ambavyo japokuwa ni vichache sana lakini vina udharura mkubwa katika ukuaji na usalama wa mwili na akaamua kuvipa jina la Vitamini. Kuna aina mbalimbali za vitamin kama A, B, C, D na E, na kila moja ina sifa za kipekee na matumizi ya aina yake katika mwili.

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita inayosadifiana na tarehe 31 Khordad 1360 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 21 Juni mwaka 1981, aliuawa shahidi Dakta Mustafa Chamran, msomi na kamanda shujaa wa vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Dakta Chamran alifanikiwa kupata shahada katika fani ya elektroniki na kisha alielekea Marekani ambako alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu. Kwa miaka kadhaa Dakta Chamran alikuwa nchini Lebanon kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo waliokuwa wakipambana na utawala wa Kizayuni wa Israel. Mara baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Dakta Chamran alichaguliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na kisha akawa mbunge wa Tehran.

Dakta Mustafa Chamran

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, inayosadifiana na 31 Khordad 1369 Hijria Shamsia, mikoa ya Gilan na Zanjan iliyoko kaskazini na kaskazini magharibi mwa Iran ilikumbwa na mtetemeko mkubwa wa ardhi wenye ukubwa wa 7.3 kwa kipimo cha rishta, na kuleta maafa makubwa. Zaidi ya watu elfu hamsini walifariki dunia na wengine zaidi ya elfu sitini kujeruhiwa, na laki tano kukosa makaazi. Mtetemeko huo licha ya kuleta maafa kwa binadamu, ulisababisha hasara kubwa ya kiuchumi kwa wananchi na serikali, na hasa kwenye miundombinu.