Alkhamisi tarehe 20 Agosti mwaka 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 30 Dhulhija 1441 Hijria sawa na Agosti 20 mwaka 2020.
Siku kama ya leo yaani tarehe 30 Mordad katika kalenda ya mwaka wa Kiirani ni siku ya kumuenzi na kumkumbuka Allamah Muhammad Baqir Majlisi, mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu. Baba yake Allamah Majlisi alipata elimu kwa msomi mkubwa wa Kiislamu Sheikh Bahai. Umahiri wa Sheikh Majlisi ulianza kuonekana akiwa bado kijana na alipata ijaza au ruhusa ya kunukuu hadithi kutoka kwa msomi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kiislamu Mulla Sadra akiwa na umri wa miaka 14 tu. Allamah Majlisi ameandika vitabu vingi wakati wa uhai wake ambavyo hii leo ni marejeo ya Waislamu. Katika kipindi cha uhai wake Allamah Muhammad Baqir Majlisi alifanya hima kubwa kuhakikisha kuwa Swala za Ijumaa na jamaa zinatekelezwa. Vilevile alifanya juhudi za kuasisi shule za masomo ya kidini na kueneza hadithi za Mtume wa Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu. Idadi ya vitabu vilivyoandika na Allamah Muhammad Baqir Majlisi imetajwa kuwa zaidi ya 600 na umashuhuri zaidi ni kile kinachojulikana kwa jina la Biharul Anwar. Vitabu vingine mashuhuri vya msomi huyo ni Hayatul Quluub, Ainul Hayat na Zadul Maad.

Miaka 505 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitokea mapigano ya kihistoria ya Chaldoran kati ya Iran na dola la Othmania katika eneo la bonde lililoko kati ya Tabriz na Khoui, kaskazini magharibi mwa Iran. Mapigano hayo yalikuwa kati ya wapiganaji wa Shah Ismail Swafawi na vikosi vya Sultan Salim Othmani.

Siku kama hii ya leo miaka 28 iliyopita, Estonia ambayo ni miongoni mwa nchi za Baltic huko magharibi mwa Urusi ya zamani ilijitangazia uhuru. Estonia ilikuwa chini ya satwa ya Urusi ya zamani kufuatia makubaliano ya siri yaliyofikiwa mwaka 1939 Miladia kati ya Hitler na Stalin. Mwaka 1991, karibu asilimia 80 ya wananchi wa Estonia walishiriki kwenye kura ya maoni na kupelekea kutangazwa uhuru wa nchi hiyo katika siku kama hii.

Siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, yaani Agosti 20 mwaka 1998 Marekani ilizishambulia kwa makombora ya masafa marefu nchi za Sudan na Afghanistan. Serikali ya Washington ilidai kwamba, watu walioshiriki katika kulipua kwa mabomu balozi za Marekani mjini Dar es Salaam, Tanzania na Nairobi, Kenya wiki mbili kabla, walikuwa na uhusiano na nchi hizo. Washington pia ilidai kuwa ilikishambulia kwa mabomu kiwanda cha kuzalisha madawa cha ash-Shifaa nchini Sudan kwa sababu eti kilikuwa kikitengeneza mada za kemikali. Hata hivyo weledi wa masuala ya kisiasa walisema kwamba, sababu ya Marekani kufanya mashambulio ya mabomu dhidi ya Sudan na Afghanistan ilikuwa ni kujaribu kufunika fedheha ya kimaadili iliyokuwa ikimkabili Rais wa nchi hiyo Bill Clinton. Kwa sababu hiyo mashambulizi hayo yaliamsha hasira za fikra za walio wengi na serikali nyingi duniani dhidi ya siasa za kutumia mabavu na kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani.