Mar 10, 2021 02:18 UTC
  • Jumatano tarehe 10 Machi mwaka 2021

Leo ni Jumatano tarehe 26 Rajab 1442 Hijria sawa na tarehe 10 Machi mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 1445 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Abu Twalib ami ya Mtume Muhammad (SAW) na baba wa Imam Ali (A.S) alifariki dunia wakati Waislamu walipokuwa chini ya mzingiro wa washirikina wa Makka. Abu Twalib alikuwa pamoja na Waislamu wengine huko katika Shiibi Abi Twalib akimlinda na kumhami mtukufu huyo mbele ya adha za washirikina. Mtume Muhammad (SAW) alikuwa chini ya uangalizi wa Abu Twalib tangu alipokuwa na umri wa miaka minane, baada ya kuaga dunia babu yake Abdul Muttalib. Abu Twalib alisilimu baada ya kubaathiwa Mtume na alikuwa muungaji mkono na mtetezi mkubwa wa Mtume Mtukufu dhidi ya washirikina wa Kikuraishi.

Baada ya kupewa Utume Nabii Muhammad (saw), Abu Talib hakumwacha mkono mtukufu huyo na alisimama imara kukabiliana na washirikina wa Kikureishi. Baada ya kufariki dunia Abu Talib, washirikina walizidisha maudhi na manyanyaso dhidi ya Bwana Mtume (saw), kiasi kwamba kutokana na hali ngumu mno iliyomkabili, hatimaye kwa amri ya Mwenyezi Mungu, mtukufu huyo alihama kutoka Makka kwenda Madina ambako aliasisi utawala wa kwanza wa Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita mvumbuzi wa Scotland, Alexander Graham Bell alivumbua simu na siku hiyo hiyo akafanya mazungumzo ya kwanza ya majaribio ya simu na msaidizi wake, Thomas Watson. Uvumbuzi huo wa simu ulileta mabadiliko makubwa katika vyombo vya mawasiliano. Bell alifaidika na uzoefu na majaribio ya wahakiki na wavumbizi wengine katika kutengeneza chombo hicho cha mawasiliano ya haraka. Baada ya hapo chombo cha simu kiliboreshwa na kufikia kiwango cha sasa kwa kukamilishwa kazi iliyofanywa na Alexander Graham Bell.

Alexander Graham Bell

Katika siku kama ya leo miaka 76 iliyopita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ndege za kivita za Marekani zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya mji mkuu wa Japan, Tokyo. Mashambulizi hayo makubwa yalishirikisha mamia ya ndege kubwa za kurusha mabomu za Marekani zilizomimina mabomu kwa mara kadhaa katika mji mkuu wa Japan. Karibu raia laki moja wa nchi hiyo waliuawa katika mashambulizi hayo. Hata hivyo Japan haikusalimu amri hadi Mwezi Agosti mwaka huo huo wa 1945 wakati Marekani iliposhambulia kwa mabomu ya nyuklia miji ya Hiroshima na Nagasaki na kuua maelfu ya raia wasio na hatia.

Mlipukko wa bomu la nyuklia 

Miaka 31 iliyopita mwaka 1368 Hijiria Shamsia, Dakta Abdul Hamid Irfani, mshairi wa Pakistan alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 80. Alikuwa mwingi wa kuhuisha tamaduni za Kiislamu na kupambana na tamaduni za Wamagharibi. Pia alikuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa na wanafunzi maarufu wa wanafalsafa na mshairi maarufu wa Lahore, Pakistan, Muhammad Iqbal. Dakta Irfani ameandika vitabu 40 katika taaluma mbalimbali, vitabu ambavyo baadhi vimepata kuchapwa nchini Iran.