Ijumaa, 30 Aprili, 2021
Leo ni Ijumaa tarehe 17 Ramadhani 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 30 Aprili mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 1443 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia Mtume Mtukufu Muhammad SAW alisafiri kutoka Makka hadi Baitul Muqaddas na kupaa mbinguni kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Aya ya kwanza ya Sura ya al Israa inatoa maelezo kuhusu muujiza huo mkubwa ikisema. "Ametakasika aliyemchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyouzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya ishara zetu. Hakika yeye ni mwenye kusikia na mwenye kuona." Kwa kuzingatia aya hiyo na hadithi za Mtume Muhammad SAW, wakati mtukufu huyo alipokuwa katika safari ya Miiraji alionyeshwa siri nyingi za Mwenyezi Mungu SW, viumbe vyake Jalali na hatima ya wanadamu katika ulimwengu wa Akhera. Tukio hilo ni miongoni mwa miujiza mikubwa ya Mtume Muhammad SAW na linadhihirisha nafasi ya juu ya mtukufu huyo.

Tarehe 17 Ramadhani miaka 1440 iliyopita, vita vya Badr, moja kati ya vita maarufu vya Mtume Muhammad SAW, vilitokea katika eneo lililoko kati ya Makka na Madina. Badr ni jina la kisima kilichoko umbali wa kilomita 120 kusini magharibi mwa mji wa Madina, ambako kulipiganwa vita vya kwanza kati ya Waislamu na washirikina. Vita vya Badr vilitokea huku washirikina wakiwa na wapiganaji wengi waliokaribia 920 na jeshi la Kiislamu likiwa na wapiganaji 313 na silaha chache. Hata hivyo imani thabiti ya Waislamu iliwafanya washinde vita hivyo.

Tarehe 10 Ordebehesht kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani sawa na tarehe 30 Aprili, inafahamika kuwa siku ya kitaifa ya Ghuba ya Uajemi. Siku hii iliitwa siku ya kitaifa ya Ghuba ya Uajemi kutokana na baadhi ya pande zenye chuki dhidi ya Iran, kufanya njama za kutaka kupotosha historia, kwa kuiita kwa majina mengine yasiyo na msingi Ghuba ya Uajemi. Jina la kihistoria la Ghuba ya Uajemi limetafsiriwa katika lugha mbalimbali kwa jina hilo au kwa jina la Bahari ya Pars. Inafaa kuashiria hapa kuwa, Ghuba ya Uajemi ni ya tatu kwa ukubwa duniani baada ya Ghuba ya Mexico na Ghuba ya Hudson. Kutokana na kuwa na vyanzo vingi vya utajiri yakiwemo mafuta na gesi, Ghuba ya Uajemi na pwani yake inahesabika kimataifa kuwa sehemu yenye umuhimu mkubwa na wa kistratijia. Kwa kuzingatia utambulisho wa kiutamaduni na kihistoria wa taifa la Iran, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Utamaduni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, liliitangaza siku ya leo ambayo inakumbusha tukio la kuwaondoa Wareno kutoka lango la Hormuz, kuwa siku ya kitaifa ya Ghuba ya Uajemi.

Siku kama ya leo miaka 244 iliyopita, alizaliwa Carl Friedrich Gauss mwanahisabati na mnajimu mashuhuri wa Kijerumani. Mama yake Gauss ndiye aliyemshawishi mno mwanawe ajikite zaidi katika somo la hisabati, na hatimaye mtoto huyo alitabahari kwenye fani hiyo. Msomi huyo wa hisabati na mnajimu mashuhuri wa Kijerumani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 78.

Tarehe 30 Aprili mwaka 1945 dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolf Hitler alijiua akiwa mafichoni chini ya ardhi baada na kufeli ndoto yake ya kutawala dunia nzima. Hitler alizaliwa mwaka 1889 nchini Austria na alipigana Vita vya Kwanza vya Dunia katika safu za kwanza za askari wa Ujerumani. Adolf Hitler alianzisha chama cha National Socialist German Workers baada ya kuchanganya itikadi za kisoshalisti na mitazamo mikali ya utaifa. Na ulipotimia mwaka 1939 alianzisha Vita vya Pili vya Dunia.

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita alifariki dunia malenga, mwandishi na msanii wa uchoraji wa zama hizi wa Iran, Ustadh Ismail Ashtiyani. Baada ya masomo ya msingi na upili, Ustadh Ashtiyani alijifunza sanaa ya kuchora kwa msanii mashuhuri wa zama hizo Kamalul Mulk. Mwaka 1307 Hijria Shamsia alishika wadhifa wa mkuu wa Chuo cha Sanaa cha Darul Funun. Miongoni mwa vitabu vyake ni pamoja na diwani ya mashairi, Kumbukumbu ya Ulaya na Historia ya Kamalul Mulk.

Tarehe 10 Ordibehesht miaka 42 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikata uhusiano wake na Misri. Amri ya kukatwa uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Misri ilitolewa na hayati Imam Ruhullah Khomeini baada ya Rais wa wakati huo wa Misri, Anwar Saadat kutia saini makubaliano ya aibu na fedheha ya Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusaliti malengo ya Wapalestina. Kutiwa saini makubaliano hayo ilikuwa hatua ya kuhalalisha uvamizi wa Wazayuni dhidi ya Palestina na kusaliti haki za Wapalestina waliokuwa wakipambana na utawala haramu wa Israel na vilevile kupuuza maslahi ya Umma wa Kiislamu. Baadaye kiongozi huyo wa Misri alitiwa adabu na shujaa, Khalid Islambuli aliyemmiminia risasi na kumuua kutokana na usaliti huo.
