Jumatatu tarehe 7 Juni 2021
Leo ni Jumatatu tarehe 26 Shawwal 1442 Hijriia sawa na tarehe 7 Juni mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 173 iliyopita Paul Gauguin, mchoraji mashuhuri wa Kifaransa alizaliwa mjini Paris. Alipata hamu ya uchoraji kutoka kwa mke wake ambaye alikuwa mwalimu wa uchoraji. Hatimaye aliamua kusafiri hadi katika kisiwa cha Tahiti kilichoko katika bahari ya Pacific ili kuendeleza sanaa hiyo. Akiwa katika kisiwa hicho alichora picha za kuvutia kuhusiana na mazingira na pia maisha ya watu wa kisiwa hicho hadi alipofariki dunia mwaka 1903.
Siku kama hii ya leo miaka 142 iliyopita, yaani tarehe 7 Juni 1879 vilianza vita vilivyochukua muda wa miaka mitano kati ya nchi za Peru, Chile na Bolivia. Vita hivyo vilianza baada ya serikali ya Bolivia kutiliana saini na shirika moja la Chile na kisha kukiuka makubaliano ya mkataba huo, na suala hilo liliifanya Chile iishambulie kijeshi Bolivia. Hatimaye Chile ilijipatia ushindi kwenye vita hivyo na kutiliana saini makubaliano mapya na nchi za Bolivia na Peru. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, ufukwe wote wa Bolivia na sehemu ndogo ya ardhi ya Peru ilichukuliwa na Chile.
Katika siku kama ya leo miaka 54 iliyopita na kufuatia kushindwa Waarabu katika vita na utawala haramu wa Israel, askari wa utawala huo waliingia katika mji wa kihistoria na kidini wa Baitul Muqaddas. Waislamu wanaupa utukufu maalumu mji huo kutokana na kuwa Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa ambacho ni kibla cha kwanza cha Waislamu unapatikana humo na pia kutokana na kuwa ni sehemu ambayo Mtume Mtukufu (saw) alipaa kuelekea mbinguni katika tukio la Mi'raaj kutokea hapo. Tangu utawala ghasibu wa Israel uzikalie kwa mabavu ardhi za Wapalestina, umekuwa ukitekeleza njama hatari za kuuharibu msikiti huo na badala yake kujenga hapo hekalu bandia la Nabii Suleiman (as). Utawala huo vilevile unatekeleza siasa hatari ya kuvuruga muundo wa jamii asili ya wakazi wa mji wa Baitul Muqaddas kwa kuwafukuza Wapalestina katika ardhi zao na kujenga hapo vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi na Kizayuni. Walowezi hao wa Kizayuni wanafanya njama kubwa ya kufuta kabisa nembo na alama za Wapalestina na Waislamu katika mji huo mtukufu wa Baitul Muqaddas.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Juni 1980, ndege za kijeshi za utawala wa Kizayuni wa Israel zilishambulia na kukiharibu kituo cha nyuklia cha Tamouz kilichoko karibu na Baghdad, mji mkuu wa Iraq. Licha ya shambulizi hilo kuharibu kikamilifu kituo hicho cha nyuklia na kuzikasirisha fikra za waliowengi duniani na vilevile kulaaniwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini hakuna hatua yoyote ya kivitendo ilizochukuliwa dhidi ya utawala wa Israel. Hivi sasa utawala huo ghasibu unamiliki zaidi ya vichwa 200 vya makombora ya nyuklia, na umekuwa ukikataa kuwaruhusu wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuikagua mitambo na vinu vyake vya nyuklia.