Jumanne tarehe 27 Julai 2021
Leo ni Jumanne tarehe 16 Dhulhija 1442 Hijria sawa na Julai 27 mwaka 2021.
Miaka 249 iliyopita, katika siku kama ya leo ulitiwa saini mkataba wa kwanza wa kuigawa Poland kati ya madola matatu makubwa ya Ulaya katika karne ya 18. Poland ambayo hii leo ni moja ya nchi zilizo huru za mashariki mwa Ulaya, iligawanywa baina ya nchi tatu za Urusi, Austria na Prusssia kwa kutiwa saini makubaliano yaliyotajwa. Ni muhimu kuashiria hapap kwamba hadi sasa Poland imeshawahi kugawanywa mara nne kati ya nchi tofauti.
Miaka 197 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, alizaliwa mwandishi maarufu wa Kifaransa Alexandre Dumas. Dumas aliandika riwaya nyingi kuhusiana na mapinduzi na historia ya Ufaransa kwa kustafidi na hadithi alizosimuliwa na baba yake ambaye alikuwa jenerali wa jeshi pamoja na kumbukumbu binafsi za wananchi kuhusu mapinduzi yalitokea nchini Ufaransa.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 5 Mordad mwaka 1358 Hijria Shamsiya, Swala ya kwanza ya Ijumaa katika mji wa Tehran baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ilisaliwa katika Chuo Kikuu cha Tehran ikiongozwa na marehemu Ayatullah Sayyid Mahmoud Talaqani, mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kiislamu, kufuatia agizo la Imam Ruhullah Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, Swala ya Ijumaa haikuwa ikifanyika kutokana na kuweko anga ya udhibiti na ukandamizaji wa serikali ya Shah.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, Muhammad Reza Pahlavi mfalme wa mwisho wa Iran aliaga dunia huko Cairo, Misri. Aliingia madarakani baada ya baba yake yaani Rezakhan kuondolewa kwenye uongozi na kubaidishwa na Waingereza. Kama alivyokuwa baba yake, Muhammad Reza Pahlavi alikuwa na uhusiano mkubwa na Uingereza na ndio maana akafanya jitihada za kulinda maslahi haramu ya nchi hiyo nchini Iran. Hata hivyo baada ya harakati za wananchi na kushinda harakati ya kuitaifisha sekta ya mafuta, maslahi ya Waingereza nchini Iran yalifikia tamati. Shah aliwakandamiza wananchi wa Iran kwa ngumi ya chuma na alikuwa kibaraka mkubwa wa Marekani. Suala hilo lilizidisha kasi ya harakati za Mapinduzi ya Kiislamu zilizoongozwa na hayati Imam Khomeini na mwaka 1357 Mapinduzi ya Kiislamu yalihitimisha utawala dhalimu wa Shah ambaye alikimbilia nje ya nchi na kufia Misri katika siku kama hii ya leo.
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, ilianza operesheni kubwa ya kijeshi iliyopewa jina la "Mirsad" huko magharibi mwa Iran kwa lengo la kuwasambaratisha vibaraka wa kundi la kigaidi la Munafiqin. Kundi la Munafiqin ambalo lilikuwa limekusanya magaidi katika mpaka wa Iran na Iraq wakiwa na silaha nzito kutoka kwa utawala wa zamani wa Baghdad lilianza kuishambulia ardhi ya Iran siku mbili kabla ya kuanza operesheni hiyo. Kiongozi wa Munafiqin alidhani kuwa magaidi hao wangeweza kuvuka barabara kuu za Iran bila ya kizuizi na tabu yoyote na kufika haraka mjini Tehran. Hata hivyo wanajeshi wa Iran wakishirikiana na wananchi waliojitolea katika operesheni hiyo ya Mirsad waliwazingira vibaraka hao wa Munafiqin huko magharibi mwa nchi na kuwasambaratisha magaidi hao walio na uhusiano mkubwa na nchi za kigeni.