Aug 15, 2021 02:28 UTC
  • Jumapili tarehe 15 Agosti 2021

Leo ni Jumapili tarehe sita Muharram 1443 Hijria Qamaria sawa na 24 Mordad mwaka 1400 Hijria Shamsiya inayosadifiana na Agosti 15 mwaka 2021.

Tarehe sita Muharram mwaka 61 Hijria yaani miaka 1382 iliyopita mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (as) aliyekuwa Karbala alimwandikia barua fupi lakini muhimu sana ndugu yake, Muhammad bin Hanafiyya na wafuasi wake kadhaa wa mjini Madina. "Barua hiyo ilisema: Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu. Hakika anayejiunga nami atapata daraja ya kuuawa shahidi, na ambaye hatajiunga hatapata ushindi." Barua hii ilikuwa na ujumbe kadhaa, miongoni mwa ujumbe hizo ni kwamba, Imam Hussein alikuwa akijua kuwa, atauawa shahidi yeye na masahaba zake katika mapambano yake na mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya. Pili ni kwamba aliweka wazi hatima ya wale wote watakaofuatana naye katika mapambano ya Karbala na kwamba wote watauawa na kwamba mtu mwenye malengo mengine bora arejee Madina.

Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita, Habib Bin Madhahir, mmoja wa masahaba wa Mtume Muhammad (saw) na mfuasi wa kweli wa Imam Hussein (as), aliwalingania watu wa kabila la Bani Asad kwa ajili ya kwenda kumsaidia mjukuu huyo wa Nabii wa Allah. Katika siku hiyo, sahaba huyo wa Mtume aliomba idhini kwa Imam Hussein (as) kwa kusema: “Ewe mjukuu wa Mtume, katika maeneo haya jirani wanaishi watu wa kabila la Bani Asad, ikiwa utaniruhusu nitaenda kwao nikawalinganie, huenda Mwenyezi Mungu akakuokoa kutokana na shari ya watu hawa makatili kupitia uwepo wa watu wa kabila la Bani Asad.” Imam Hussein alimruhusu Habib Bin Madhahir ambaye alitoka majira ya usiku kwenda kwa watu wa kabila hilo akiwataka wamsaidie mjukuu huyo wa Mtume. Akiwa katika linganio hilo, sahaba huyo wa Mtume alisema: “Kwa kuwa nyinyi ni watu wa ukoo na kabila langu, ninakulinganieni kufuata njia hii, leo ninakuombeni msikie usia wangu na mfanye haraka kwenda kumsaidia Imam Hussein (as) ili mpate utukufu wa dunia na Akhera.” Kutokana na wito huo, watu wachache kutoka kabila hilo wanaokadiriwa kufikia 90 walisimama na kwenda kumsaidia mjukuu huyo wa Nabii wa Allah. Hata hivyo baadaye walitoroka na kurejea makwao baada ya kufahamu kwamba jeshi la Omar Bin Sa’ad lilifahamu nia yao, hivyo walihofia kuuawa na jeshi hilo. Baada ya Imam Hussein kusikia habari hiyo, alisema: “Laa haula walaa quwwatan illa Billah.”

Kaburi la Habib Bin Madhahir

 

Siku kama ya leo miaka 1037 iliyopita inayosadifiana na tarehe 6 Muharram mwaka 406 Hijria, alifariki dunia Sayyid Muhammad Hussein Musawi Baghdadi, msomi mashuhuri, mwanafikra na mshairi wa Kiislamu. Aalim huyo pia alijulikana kwa jina la Sayyid Radhi. Alipata elimu za wakati huo katika kipindi cha ujana wake akiwa pamoja na ndugu yake, Sayyid Murtadha, ambaye pia alikuwa msomi mtajika. Sayyid Radhi aliinukia kuwa msomi mkubwa katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur'ani Tukufu na elimu nyingine za Kiislamu. Msomi huyo alikuwa wa kwanza kuasisi chuo kikuu kwa mtindo wa kisasa na ameandika zaidi ya vitabu 20 katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur'ani, historia na fasihi ya Kiarabu. Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni Nahjul Balagha ambacho kinakusanya semi, hotuba, amri, barua na mawaidha ya Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as).

Kaburi la Sayyid Radhi

 

Miaka 73 iliyopita India ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza, baada ya miaka mingi ya mapambano ya kupigania uhuru. India ina historia kongwe na watawala mbalimbali wa ndani na nje wamewahi kutawala nchini humo. Mapambano ya wananchi wa India dhidi ya mkoloni Muingereza yalipamba moto zaidi baada ya kuasisiwa Chama cha Congress ya Kitaifa na kujiunga na chama hicho Mahatma Gandhi.

Miaka 619 iliyopita katika siku kama hii ya leo nchi ya Jamhuri ya Congo Brazzaville ilipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Huko nyuma Congo Brazzaville ilikuwa sehemu ya ardhi ya Congo katika Afrika Magharibi iliyojumuisha Zaire ya zamani na Angola.  Kongo Brazzaville iligunduliwa na Wareno katika karne ya 15 na baadaye ilikaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kifaransa kwa miaka kadhaa mfululizo. Kongo Brazaville iko magharibi mwa Afrika ikipakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cameroon, Gabon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Angola. 

 

Katika siku kama ya leo miaka 51 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allamah Agha Bozorge Tehrani. Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Bozorge Tehrani alikwea kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za maeneo mengi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia". Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia katika mji mtakatifu wa Najaf na kuzikwa katika maktaba yake kama alivyokuwa ameusia. 

 

Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, mfereji wa Panama ulifunguliwa rasmi kufuatia kupita meli ya kwanza katika kanali hiyo. Ujenzi wa kanali hiyo ulianzishwa na wahandisi wa Kifaransa na baadaye serikali ya Marekani ilinunua kampuni ya Ufaransa iliyokuwa ikijenga mfereji huo na kukamilisha ujenzi wake. Kujengwa mfereji huo wenye urefu wa zaidi ya kilomita 60 kuliunganisha bahari mbili za Pacifi na Atlantic.

Mfereji wa Panama

 

Miaka 31 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 24 Mordad 1369 Hijria Shamsia, Saddam Hussein Rais wa zamani wa Iraq alimtumia barua Hujjatul Islam Walmuslimin Hashemi Rafsanjani aliyekuwa Rais wa Iran wakati huo, akimjulisha kwamba amekubali kikamilifu vipengee vya makubaliano ya mpaka yaliyotiwa saini 1975 nchini Algeria. Hata hivyo, tarehe 27 Shahrivar 1359 Hijria Shamsia, Saddam Hussein baada ya kushawishiwa na madola ya kibeberu ya Magharibi, alijitokeza kwenye televisheni ya Iraq na kuuchanachana mkataba huo, na baada ya siku chache, alianza kuivamia ardhi ya Iran. Saddam Hussein na waitifaki wake walidhani kwamba, muda mfupi tu baada ya kuivamia ardhi ya Iran wangeliweza kuuangusha mfumo mchanga wa Kiislamu hapa nchini. Hata hivyo kusimama kidete wananchi na mapambano ya wapiganaji shupavu wa Kiislamu wa Iran yalibatilisha njama zao na jeshi vamizi la Iraq likalazimika kurejea nje ya mipaka ya Iran baada ya kushindwa mtawalia. 

 

Miaka 73 iliyopita, sawa na tarehe 15 Agosti 1948 nchi ya Korea ya Kusini iliundwa baada ya kujitokeza mgawanyiko wa visiwa vya Korea. Visiwa vya Korea vilikabiliwa na uvamizi na kukaliwa kwa mabavu wa madola yenye nguvu katika eneo hilo kama vile China na Japan tokea nusu ya kwanza ya karne ya ishirini.

Bendera ya Korea Kusini

 

Miaka 16 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 15 Agosti 2005 Miladia, utawala wa Kizayuni wa Israel ulilazimika kuondoka katika maeneo ya Ukanda wa Gaza, magharibi mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Eneo hilo lilikaliwa kwa mabavu na Wazayuni mwaka 1967, baada ya kutokea vita vya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel. Lakini pamoja na hayo utawala huo katili hutekeleza mashambulio ya mara kwa mara dhidi ya Gaza na kuwaua Wapalestina wengi hasa  wanawake na watoto.

Askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakiondoka Gaza kwa madhila

 

Tags