Sep 16, 2021 02:22 UTC
  • Alkhamisi tarehe 16 Septemba 2021

Leo ni Alkhamisi tarehe 9 Safar 1443 Hijria sawa na Septemba 16 mwaka 2021.

Katika siku kama ya leo miaka 1406 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, aliuawa shahidi Ammar bin Yassir, sahaba mkubwa wa Mtume Muhammad (saw) na msaidizi wa karibu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Ammar bin Yasir aliuawa katika vita vya Siffin vilivyojiri kati ya majeshi ya Imam Ali (as) na Muawiya bin Abi Sufian. Ammar alizaliwa miaka 57 kabla ya Hijra ya Mtukufu Mtume na wazazi wake wawili, yaani Yassir na Sumayyah, ndio waliokuwa mashahidi wa kwanza katika Uislamu. Sahaba huyu mtukufu alisimama imara dhidi ya maudhi ya makafiri na alishiriki katika vita mbalimbali pamoja na Bwana Mtume (SAW). Wakati mmoja Mtume alimwambia: "Ewe Ammar! Baada yangu kutatokea fitina, na katika hali hiyo mfuate Ali bin Abi Twalib na kundi lake, kwani Ali yuko pamoja na haki na haki iko pamoja na Ali.

Siku kama ya leo miaka 1022 iliyopita, alifariki dunia Abu Ali Maskawayh, mtaalamu, mwanahistoria na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu. Miskawayh alizaliwa mwaka 320 katika mji wa Rei ulio karibu na mji mkuu wa Iran ya sasa. Miskawayh alikuwa mwalimu katika elimu za zama zake sambamba na kufanya utafiti katika elimu ya tiba, kemia, historia na falsala. Miongoni mwa athari zilizobakia za Abu Ali Miskawayh ni pamoja na kitabu kiitwacho "Tahdhibul-Akhlaq", "Tajaaribul-Umam" na "Jaavidaane Kherad."

Tarehe 9 Safar miaka 848 iliyopita yaani tarehe tisa Safar mwaka 595 Hijria, alifariki dunia Ibn Rushd Andalusi, msomi mkubwa wa falsafa wa Kiislamu. Abul-Walid Muhammad Bin Ahmad Bin Rushd, ambaye alikuwa miongoni mwa wasomi wakubwa wa elimu ya falsafa wa Kiislamu katika karne ya 6 Hijiria, alikuwa pia mtaalamu katika elimu za fiqhi, hadithi, fasihi, mantiki na elimu nyingine za wakati huo. Ibn Rushd aliyekuwa akiishi Andalusia (Uhispania ya leo) alikuwa mtu wa karibu kwa mfalme na miongoni mwa makadhi wa eneo moja la utawala wa kifalme. mwanafalsafa huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi kikiwemo cha 'Bidaayatul-Mujtahid' 'Falsafatu Ibn Rushdi' na 'al-Kulliyaat'.

Ibn Rushd Andalusi

Miaka 285 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Daniel Gabriel Fahrenheit mwanahesabati na mwanafizikia wa Kijerumani aliyevumbua kipimajoto yaani thermometer, akiwa na umri wa miaka 50. Fahrenheit alikuwa na fikra ya kubuni kifaa ambacho kingekuwa na uwezo wa kupima kiwango cha joto na mwaka 1724 mwanafizikia huyo Mjerumani akafanikiwa kutengeneza kipimajoto hicho. Kifaa hicho ambacho kimepewa jina la msomi huyo mwenyewe yaani Fahreinheit, bado kinatumika hadi leo.

Daniel Gabriel Fahrenheit

Miaka 90 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, aliuawa Omar al Mukhtar kiongozi wa taifa la Libya katika mapambano ya ukombozi dhidi ya wakoloni wa Italia. Omar Mukhtar aliyekuwa kiongozi wa kidini alizaliwa mwaka 1859. Mwaka 1895 alielekea Sudan na kushiriki katika harakati za kupambana na ukoloni wa Uingereza. Baada ya kushindwa kwa harakati hizo, Omar Mukhtar alirejea nchini Libya. Mwaka 1911 Wataliano waliivamia Libya kwa lengo la kuitawala nchi hiyo. Kiongozi huyo wa kidini aliwahimiza wapiganaji wa makabila ya Libya kusimama kidete na kupambana dhidi ya wavamizi wa Kitaliano na kuwasababishia hasara kubwa. Hata hivyo kwa kutumia askari wengi zaidi na silaha za kisasa wavamizi hao walimzingira Omar Mukhtar na wenzake na kumkamata na kisha wakamnyonga katika siku kama ya leo.

Omar al Mukhtar

Siku kama ya leo miaka 89 iliyopita Sir Ronald Ross daktari mashuhuri wa Kiingereza na mvumbuzi wa chanzo cha ugonjwa wa Malaria alifariki dunia. Alizaliwa Mei 13 mwaka 1857 katika mji wa Almora huko India. Alielekea Uingereza akiwa mdogo na alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu PhD katika taaluma ya tiba. Uvumbuzi wake wa chanzo cha Malaria ulikuwa na nafasi muhimu sana kwani uliandaa uwanja wa namna ya kukabiliana na maradhi hayo. Mwaka 1902 Dakta Ronald Ross alitunukiwa tuzo ya Nobel. Hatimaye Daktari Ronald Ross aliaga dunia katika siku kama ya leo baada ya kuishi kwa muda wa miaka 75.

Sir Ronald Ross

Tarehe 16 Septemba miaka 82 iliyopita Warsaw mji mkuu wa Poland ulizingirwa na Wajerumani, katika mwezi wa kwanza wa Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulio ya wanajeshi wa Kinazi wa Ujerumani huko Poland yalianza siku 15 kabla ya kuanza vita hivyo.

Warsaw mji mkuu wa Poland

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita utawala wa kidikteta wa Reza Khan nchini Iran uliangushwa na kukaanza kipindi cha utawala wa mwanawe yaani Muhammad Reza Pahlavi. Baada ya mashambulio ya Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti upande wa kaskazini na jeshi la Uingereza upande wa magharibi na kusini mwa Iran na kukaliwa kijeshi Iran wakati wa kujiri Vita vya Pili vya Dunia, Reza Khan alilazimika kujiuzulu katika siku kama ya leo baada ya kutawala kidikteta nchini Iran kwa muda wa miaka 15. Baada ya kubaidishwa Reza Khan, mwanawe yaani Muhammad Reza Pahlavi aliingia madarakani kwa ushirikiano na Waingereza. Baada ya kubaidishwa kwa muda katika kisiwa cha Mauritius hatimaye alipelekwa Johannesburg Afrika Kusini. Aliishi huko hadi alipofariki dunia tarehe 26 Julai 1944.

Kuanza kwa utawala wa Muhammad Reza Pahlavi

Na siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, zilzala iliyokuwa na ukubwa wa 7.7 kwa kipimo cha rishta ililitikisa eneo la kaskazini mashariki mwa Iran na kuuharibu mji wa Tabas na vijiji vya kando kando yake. Watu zaidi ya elfu 25 waliuawa na makumi ya maelfu kujeruhiwa katika mtetemeko huo mkubwa wa ardhi. Zilzala ya Tabas ilitokea sambamba na kupamba moto mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah.

آغاز سلطنت محمدرضا پهلوی

 

Na leo tarehe 16 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya Kulindwa Tabaka la Ozoni. Siku hii haina hestoria ndefu ikilinganishwa na matukio mengine ya kimataifa. Siku hii iliainishwa mwaka 1994 wakati nchi wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa zilipokubaliana kutenga siku maalumu ya kulindwa tabaka la Ozoni. Tangu wakati huo nchi zote ziliahidi kuanza kuzalisha na kutumia nyenzo na vitu ambavyo havina madhara kwa tabaka hilo. Lengo la maadhimisho ya Siku ya Kimatafaifa ya Ozoni ni kuhamasisha kulindwa tabaka hilo muhimu sana linalowalinda viumbe hai ardhini wasiathiriwe na mionzi hatari ya Kikiuka Urujuani (Ultraviolet).