Sep 18, 2021 03:09 UTC
  • Jumamosi, 18 Septemba 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 11 Mfunguo Tano Safar 1443 Hijria, ambayo inasadifiana na tarehe 18 Septemba 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 942 iliyopita Jaafar bin Hussein bin Ahmad mashuhuri kwa jina la Siraj, alifariki dunia katika mji wa Sur (Tyre) kusini mwa Lebanon. Jaafar bin Hussein bin Ahmad alikuwa miongoni mwa mafaqihi, wapokeaji hadithi na maqarii wakubwa wa karne ya sita. Siraj alizaliwa mwaka 419 Hijria na kupata elimu mbalimbali kama hadithi, qiraa na fasihi ya lugha. Aidha alisafiri katika nchi mbalimbali kama Misri na eneo la Sham kwa ajili ya kuzidisha elimu na maarifa. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu mbalimbali na miongoni mwake ni kile alichokipa jina la Nidhamul Manasik. ***

Jaafar bin Hussein bin Ahmad mashuhuri kwa jina la Siraj,

 

Katika siku kama ya leo miaka 312 iliyopita, alizaliwa Samuel Johnson mwandishi wa drama, malenga na mwandishi wa visa wa Kiingereza. Alianza shughuli zake za fasihi sambamba na ukosoaji wake katika taaluma hiyo. Baada ya muda mwanatamthilia huyo aliingia katika uga wa utunzi wa mashairi. Samuel Johnson aliaga dunia mwaka 1784. ***

Samuel Johnson

 

Siku kama ya leo miaka 203 iliyopita, nchi ya Chile ilipata uhuru. Mwaka 1536 Chile ilidhibitiwa na Hispania. Sehemu kubwa ya kukoloniwa Chile, nchi hiyo ilikuwa sehemu ya utawala wa Naibu Mfalme wa Uhispania nchini Peru. ***

Bendera ya Chile

 

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita yaani tarehe 18 Septemba mwaka 1961 aliaga dunia Dag Hammarskjold mwanasiasa na Katibu Mkuu wa Pili wa Umoja wa Mataifa. Mwanasiasa huyo wa nchini Sweden alifariki dunia baada ya ndege iliyokuwa imembeba wakati wa safari yake katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanguka. Hammarskjold alikuwa Congo kwa lengo la kufanya mazungumzo na pande husika ili kumaliza vita vya ndani nchini humo. Mwanasiasa huyo alizaliwa mwaka 1905 na alihesabiwa katika zama zake kuwa mmoja kati ya waandishi stadi nchini Sweden. Mwaka 1952, Dag Hammarskjold alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobeli kutokana na harakati zake za kuimarisha amani duniani. ***

Dag Hammarskjold

 

Na miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 27 Shahrivar mwaka 1367 Hijria Shamsia, aliaga dunia, Ustadh Muhammad Hussein Shahriyar mshairi mashuhuri wa Kiirani. Alizaliwa mjini Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran na baada  ya kumaliza masomo yake ya sekondari katika Chuo cha Dar al-Funun mjini Tehran alijiunga na chuo cha tiba. Hata hivyo baada ya miaka michache aliacha masomo na kurejea katika kijiji alichozaliwa. Ustadh Shahariyar alitoa mashairi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 23. Sambamba na kushadidi harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini, Shahriyar aliungana na wimbi hilo kwa kutumia mashairi yake. Vilevile alikuwa mashuhuri sana kwa kumpenda Mtume wa Ahlubaiti zake na mapenzi hayo yalidhihiri katika tungo na mashairi yake. ***

Ustadh Muhammad Hussein Shahriyar mshairi mashuhuri wa Kiirani

 

Tags