Jumamosi, Pili Oktoba, 2021
Leo Jumamosi tarehe 25 Mfunguo Tano Safar 1443 Hijria ambayuo inasadifiana na tarehe Pili Oktoba 2021.
Siku kama ya leo miaka 834 iliyopita, mji wa Baitul-Muqaddas ulikombolewa na Salahuddin Ayyubi kamanda mwanamapambano wa Kiislamu. Awamu ya kwanza ya vita vya Msalaba baina ya Wakristo na Waislamu vilianza 1096 ambapo miaka minne baadaye majeshi ya msalaba Mwekundu yalishambulia mji wa Baitul-Muqaddas na kuukalia kwa mabavu. Wanajeshi wao wa Msalaba walifanya uporaji na kuwauwa kikatili maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wasio na hatia wa ardhi hiyo. Hata hivyo mnamo mwaka 1187, baada ya Salahuddin Ayyubi kudhibiti Syria, Lebanon na Misri, aliuzingira mji wa Baitul-Muqaddas. Awali aliwatumia ujumbe wavamizi akiwaeleza heshima maalumu aliyonayo kwa mji huo na kutotaka kufanya umwagaji damu katika eneo hilo na kuwataka wavamizi hao waondoke katika mji huo na hata akawadhaminia usalama wa mali zao. Hata hivyo watu wa msalaba walikataa na hivyo kupelekea kuibuka vita na mji huo kukombolewwa na Waislamu katika siku kama ya leo wakiongozwa na kamanda Salahuddin Ayyubi.***
Miaka 152 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Mahatma Gandhi, kiongozi wa harakati ya kupigania uhuru nchini India katika moja ya vijiji vya jimbo la Gujarat. Mwaka 1891 Miladia Gandhi alirejea kutoka nchini Uingereza na kuishi mjini Mumbai. Mwaka 1893 Miladia Mahatma Gandhi alielekea mjini KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini. Akiwa nchini humo alishuhudia ubaguzi wa rangi wa jamii ya wachache ndani ya taifa hilo. Mwaka 1917 Miladia na baada ya kurejea nchini kwake alipata umashuhuri mkubwa. Na miaka michache baada ya Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia yaani akiwa na umri wa miaka 33 aliongoza mapambano kwa ajili ya kuwaokoa watu wake sanjari na kupigania uhuru wa India kutoka mikononi mwa Waingereza ambapo hatimaye na baada ya kuvumilia matatizo mengi akiwa na shakhsia tofauti kama vile Jawaharlal Nehru akafanikiwa kulipatia uhuru taifa hilo hapo mwaka 1947 Miladia. ***
Tarehe Pili Oktoba miaka 117 iliyopita alizaliwa Graham Greene mwandishi wa Uingereza. Mwandishi huyo aliakisi matendo mema na mabaya katika athari zake na aliandika kwenye kitabu chake kinachoitwa 'Nguvu na Utukufu' kwamba subira, uvumilivu na mateso ni njia ya wokovu. Graham Greene ameacha vitabu vingi na baadhi ni 'Mtu wa Tatu', 'Utawala Unaotisha' na Muuaji wa Kukodishwa'. Mwandishi huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1991.***
Na katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita inayosadifiana na tarehe Pili Oktoba 1958, nchi ya Guinea Conakry ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wareno walianza kumiminika nchini Guinea mwishoni mwa karne ya 15, na mwanzoni mwa karne ya 19, Wafaransa walipata satua zaidi nchini humo. Mwaka 1849 nchi hiyo ilikoloniwa rasmi na Ufaransa. Guinea Conakry inapakana na nchi za Senegal, Mali, Ivory Coast, Liberia, Sierra Leone na Guinea Bissau.***