Dec 18, 2021 03:02 UTC
  • Jumamosi, 18 Desemba, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 13 Mfunguo Nane Jamadil-Awwal 1443 Hijria mwafaka na tarehe 18 Desemba 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1432 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, Bibi Fatma Zahra binti wa Mtume Muhammad SAW alikufa shahidi baada ya kuishi maisha mafupi lakini yaliyojaa baraka tele. Baba yake ni Mtume Muhammad SAW na mama yake ni Bibi Khadija binti Khuwaylid AS. Bibi Fatma alishiriki katika medani mbalimbali za kipindi cha mwanzo wa Uislamu akiwa bega kwa bega na Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) na Imam Ali bin Abi Talib AS na alilea watoto wema, kama Imam Hassan na Hussein AS ambao Mtume (saw) amesema kuwa ni viongozi wa mabarobaro wa peponi. Bibi Fatma alisifika mno kwa tabia njema, uchamungu na elimu, na alikuwa mfano na kiigizo chema cha Waislamu. ***

 

Miaka 107 iliyopita katika siku kama ya leo, Uingereza iliikoloni rasmi Misri. Inafaa kukumbusha kwamba, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa Othmania ulikuwa mwitifaki wa madola yaliyokuwa yakiipinga Uingereza yaani Ujerumani na Austria. Uingereza nayo ikiwa na lengo la kukabiliana na kitendo hicho, iliikalia kwa mabavu Misri, ambayo hadi katika kipindi hicho ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Othmania. Harakati za ukombozi za wananchi wa Misri dhidi ya mkoloni Mwingereza zilizaa matunda mwaka 1922, ambapo nchi hiyo ilijitangazia uhuru wake. ***

Bendera ya Misri

 

Katika siku kama ya leo miaka 83 iliyopita msomi wa Ujerumani, Otto Hahn, alifanikiwa kupasua kiini cha atomu, hatua ambayo ilikuwa mwanzo wa zama za atomu. Mtaalamu huyo wa kemia alizaliwa mwaka 1879 huko Frankfurt na kupata shahada ya uzamivu katika taaluma ya kemia. Tangu wakati huo alijishughulisha na utafiti katika taaluma ya fizikia. Baada ya utafiti mkubwa na katika siku kama hii ya leo Otto Hahn alifanikiwa kupasua kiini cha atomu. Hatua hiyo iliibua nishati kubwa ambayo baadaye ilianza kutumika katika vinu na mabomu ya nyuklia. Mwaka 1944 Otto Hahn alitunikiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya kemia. ***

Otto Hahn,

 

Na tarehe 18 Disemba miaka 42 iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha makubaliano ya kufuta aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake. Makubaliano hayo yana lengo la kuondoa dhulma zinazofanywa dhidi ya wanawake duniani. Hata hivyo makubaliano hayo, kama yalivyo mengine mengi ya kimataifa, yanatawaliwa na mitazamo ya kimaada ya Magharibi inayosisitiza usawa wa jinsia mbili za mwanamke na mwanaume katika kila kitu. Hii ni katika hali ambayo mwanamke na mwanaume wanatofautiana kimwili na kiroho. Kwa sababu hiyo dini za Mwenyezi Mungu hususan Uislamu zinasisitiza kuwa njia ya kuwakomboa wanawake ni kuwatayarishia mazingira ya uadilifu kwa kutilia maanani uwezo wao wa kimwili na kiroho. ***

Makubaliano ya kufuta aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake

 

Tags