Oct 27, 2024 02:21 UTC
  • Jumapili, 27 Oktoba, 2024

Leo ni Jumapili 23 Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria mwafaka na 27 Oktoba 2024.

Tarehe 23 Rabiuthani miaka 201 iliyopita alifariki dunia faqihi, mwanachuoni wa Hadithi na malenga mashuhuri wa Kiislamu, Allamah Ahmad Naraqi. Mwanazuoni huyo alizaliwa mwaka 1185 Hijria na kukulia katika mji wa Kashan katikati mwa Iran ambako alipata elimu kwa baba yake, Mullah Mahdi Naraqi. Miaka kadhaa baadaye alihamia katika mji mtakatifu wa Najaf, nchini Iraq na kupata elimu ya juu kwa maulamaa wakubwa wa mji huo. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vya "Miirajus Saada" na "Asrarur Hajj."

 

Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita, nchi ya Norway ilivunja muungano wake na Sweden na kujitangazia uhuru. Kabla ya karne ya 14 Norway ilikuwa nchi yenye ushawishi na moja ya madola vamizi. Hata hivyo mnamo mwaka 1380 ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Denmark na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo kwa muda wa karne 4.

 

Katika siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, baada ya Japan kupigana vita na nchi mbili za China na Russia kwa miaka kadhaa na kupata ushindi katika vita hivyo, iliunganisha rasmi ardhi ya Korea na ardhi yake. Korea iliendelea kuwa chini ya udhibiti wa Japan hadi mwaka 1945 wakati Japan iliposhindwa katika Vita vya Pili vya Dunia. 

 

Katika siku kama ya leo miaka 66 iliyopita katika siku kama ya leo, Jenerali Muhammad Ayub Khan alifanya mapinduzi nchini Pakistan na kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Tukio hilo lilitokea miaka 11 baada ya Pakistan kupata uhuru, ambapo Jenerali Muhammad Ayub Khan aliyekuwa mmoja wa makamanda wa jeshi alichukua hatamu za uongozi baada ya kufanya mapinduzi ambayo hayakuwa na umwagaji damu.  Kufuatia mapinduzi hayo, Iskander Mirza aliyekuwa Rais wa kwanza wa Pakistan akalazimika kuondoka madarakani. Baada ya mapinduzi hayo, Muhammad Ayub Khan ambaye alichukua nyadhifa za Urais na Waziri Mkuu alitangaza serikali ya kijeshi nchini humo. Hata kama baada ya miaka 7 Ayub Khan aliibuka mshindi katika uchaguzi wa Rais uliofanyika nchini humo mwaka 1965, lakini alianza kukabiliwa na mashinikizo baada ya kuongezeka matatizo ya kiuchumi na kisiasa. Hatimaye mwaka 1969, Ayub Khan aliachia ngazi na kukabidhi uongozi wa nchi kwa Jenerali Yahya Khan  aliyekuwa mkwewe.

Jenerali Muhammad Ayub Khan

 

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita Imam Ruhullah Khomeini alipinga vikali mpango wa Fahd bin Abdulaziz kuhusu mapatano ya Palestina na Israel. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na baada ya kutiwa saini mkataba wa Camp David baina ya serikali ya Misri na utawala ghasibu wa Israel chini ya upatanishi wa Marekani, tawala vibara za Kiarabu zilifuata nyayo za utawala wa Misri katika suala hilo. Wakati huo Fahd bin Abdulaziz aliyekuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, alitoa pendekezo la kutambuliwa rasmi utawala vamizi wa Israel, suala ambalo lilikabiliwa na upinzani mkali wa Waislamu kote duniani. Kwa msingi huo katika siku kama hii ya leo Imam Ruhullah Khomeini alitoa hotuba akisema: "Ni wajibu kwetu sisi na kwa kila Mwislamu kupinga mipango kama ule uliopendekezwa na Fahd. Tunawajibika kulaani mipango kama hii isiyokuwa na faida kwa watu wanaodhulumiwa. Jambo hatari sana kwa sasa ni makubaliano ya Camp David na mpango wa Fahd ambayo inaimarisha zaidi Israel na kudumisha jiani zake." Upinzani huo wa wazi wa Imam Khomeini na uungaji mkono wa Waislamu kote dunia kwa misimamo hiyo ya Imam ilikuwa sababu ya kukataliwa na kupingwa pendekezo hilo katika nchi nyingine. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 8 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Taqi Tabatabai Qumi mmoja wa Marajii Taqlidi wa Kishia. Ayatullah Taqi Tabatabai Qumi ambaye ni mashuhuri zaidi kwa jina la Haji Agha Taqi Qumi alizaliwa mwaka 1301 Hijria Shamsia katika mji wa Mash’had. Baba yake ni Sayyid Hussein Tabatabai Qumi aliyekuwa mmoja wa Marajii wakubwa wa Taklidi ambaye kutokana na kupinga amri ya Reza Shah mfalme wa wakati huo wa Iran ya kuondolewa hijabu kwa nguvu, alilazimika kuhama Iran na kuelekea Iraq. Sayyid Taqi alisoma masomo ya awali na ya utangulizi kwa baba yake na alipoelekea Iraq alisoma kwa walimu mahiri wa zama hizo kama Sayyid Muhammad Hadi Milani, Sayyid Abdul-Hadi Shirazi, Hussein Hilli, Muhammad Kadhim Shirazi na wengineo. ***

 

Tags