Nguvu za kijeshi za Iran hazijaathiriwa na shambulio la Israel
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Kitaifa la Iran (SNSC) Ali Akbar Ahmadian amesema hujuma ya hivi karibuni za Israel haijapunguza hata kidogo nguvu za kijeshi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Akizungumza Jumatatu alipotembelea Ofisi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, jijini Tehran, Ahmadian alisema: "Operesheni hiyo ya Israel haikuwa na athari hata kidogo kwa nguvu ya kijeshi ya Iran,"
Utawala wa Israel ulishambulia vituo kadhaa vya kijeshi vya Iran mapema Jumamosi, na kuua maafisa wanne wa Jeshi la Iran na raia mmoja.
Kituo cha Ulinzi wa Anga cha Iran kilisema uharibifu mdogo ulisababishwa katika baadhi ya maeneo, na kwamba uchunguzi kuhusu yaliyojiri unaendelea.
Iran imesisitiza kuwa haitaki vita lakini haitaacha haki yake ya kutoa jibu linalofaa na thabiti kwa kitendo cha hivi karibuni cha uchokozi cha Israel.
Katika barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Pascale Christine Baeriswyl siku ya Jumapili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alitoa wito wa kufanyika kwa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani shambulio la Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.