Burkina Faso yavunja vyama vyote vya siasa, yasema vimechochea migawanyiko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136058-burkina_faso_yavunja_vyama_vyote_vya_siasa_yasema_vimechochea_migawanyiko
Serikali ya Burkina Faso inayoongozwa na jeshi imetoa amri ya kuvunjwa vyama vyote vya siasa ambavyo kabla ya hapo vilikuwa tayari vimelazimishwa kusimamisha shughuli zao kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini humo miaka minne iliyopita.
(last modified 2026-01-30T09:12:34+00:00 )
Jan 30, 2026 07:46 UTC
  • Burkina Faso yavunja vyama vyote vya siasa, yasema vimechochea migawanyiko

Serikali ya Burkina Faso inayoongozwa na jeshi imetoa amri ya kuvunjwa vyama vyote vya siasa ambavyo kabla ya hapo vilikuwa tayari vimelazimishwa kusimamisha shughuli zao kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini humo miaka minne iliyopita.

Baraza la mawaziri la taifa hilo la Afrika Magharibi lilipitisha amri hiyo jana Alkhamisi huku serikali hiyo ya kijeshi ikijitahidi kudhibiti uasi unaohusishwa na makundi ya kigaidi ya al-Qaeda na ISIL (ISIS).

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burkina Faso, Emile Zerbo, amesema, uamuzi huo ulikuwa sehemu ya juhudi kubwa zaidi za "kujenga upya nchi" baada ya utumiaji mbaya na ufanisi mbovu uliodaiwa kuwepo katika mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini humo.

Zerbo amebainisha kuwa ukaguzi wa serikali uligundua kwamba kuongezeka kwa vyama vya siasa kumechochea mgawanyiko na kudhoofisha mshikamano wa kijamii.

Amri hiyo ya serikali inavunja vyama vyote vya siasa na uundaji wa vyama, huku mali zote za vyama hivyo zikitarajiwa kuhamishiwa serikalini.

Kabla ya mapinduzi ya kijeshi, Burkina Faso ilikuwa na zaidi ya vyama 100 vya siasa vilivyosajiliwa, huku 15 vikiwakilishwa bungeni baada ya uchaguzi mkuu wa 2020.

Burkina Faso inaongozwa na Kapteni Ibrahim Traore, ambaye alichukua madaraka katika mapinduzi ya Septemba 2022, miezi minane baada ya mapinduzi ya awali ya kijeshi kumpindua Rais Roch Marc Kabore aliyechaguliwa kidemokrasia.

Viongozi wa kijeshi wa nchi hiyo wamekata uhusiano na mkoloni wa zamani Ufaransa na kuigeukia Russia kwa ajili ya msaada wa kiusalama.../