Qalibaf: Iran haipingi mazungumzo, inataka diplomasia ichukue mkondo wake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136050-qalibaf_iran_haipingi_mazungumzo_inataka_diplomasia_ichukue_mkondo_wake
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa Tehran haipingi msingi wa mazungumzo na diplomasia ambao lazima uwe wa aina yake na wenye mlingano kwa mujibu wa kuheshimiana pande mbili.
(last modified 2026-01-30T03:12:48+00:00 )
Jan 30, 2026 03:12 UTC
  • Qalibaf: Iran haipingi mazungumzo, inataka diplomasia ichukue mkondo wake

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa Tehran haipingi msingi wa mazungumzo na diplomasia ambao lazima uwe wa aina yake na wenye mlingano kwa mujibu wa kuheshimiana pande mbili.

Katika mahojiano yake na televisheni ya CNN, Mohamamd Baqer Qalibaf amesema kuwa mazungumzo chini ya kivuli cha vita yanachochea mivutano na ukosefu wa usalama, na kwamba: Iran iko tayari kwa mazungumzo ya dhati kwa mujibu wa sheria na kanuni za kimataifa.

Spika wa Bunge la Iran amesisitiza kuwa Rais Donald Trump wa Marekani hadi sasa amethibitisha kwamba anataka kutwisha mitazamo yake ya kisiasa kupitia vitisho vya kuanzisha vita.

Katika mahojiano hayo na televisheni ya CNN, Mohammad Baqer Qalibaf ameashiria pia mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran mwezi Juni mwaka jana na kusema, Marekani ilitekeleza hujuma hiyo siku mbili kabla ya kufanyika durua ya sita ya mauzngumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Washington na Tehran. 

Spika Qalibaf ameongeza kuwa "Maadamu hakuna dhamana yoyote kwa haki za taifa la Iran, maslahi ya kiuchumi ya taifa la Iran yanakabiliwa na vitisho na hadhi ya taifa haiheshimiwi, kwa kawaida hakuwezi kufanyika mazungumzo, kwa sababu hatutambui amri, hatua za mabavu au kusalimu amri  kuwa ni mazungumzo."

Amesema Trump lazima achukue hatua za kufikia "amani ya kweli" ikiwa kweli anatafuka amani na kudai anastahili Tuzo ya Amani ya Nobel.

Matamshi hayo yanakuja huku Trump akiendelea kutoa vitisho vya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran. Washington imetuma meli ya kivita ya USS Abraham Lincoln na kundi la meli kadhaa za kivita eneo la Asia Magharibi karibu na Iran.