Araqchi: Vikosi vya Jeshi la Iran vinashikilia kitufe cha kufyatua risasi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araqchi, ameandika kwenye chaneli ya X, akijibu vitisho vya hivi karibuni vya Rais Donald Trump wa Marekani kwamba: "Vikosi vyetu vya jeshi vimeshikilia kitufe cha kufyatua risasi na viko tayari kujibu haraka na kwa kina uchokozi wowote dhidi ya ardhi, anga na maji ya nchi hii."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Silaha za nyuklia hazina nafasi katika hesabu za usalama za Tehran, na hatujawahi kutaka kupata silaha hizo."
Sayyid Abbas Araqchi ameongeza kuwa: "Masomo muhimu tuliyojifunza kutokana na Vita vya Siku 12 yametupa uwezo wa kujibu kwa nguvu, kasi, na shadidi zaidi."
Ameendelea kuandika: "Wakati huo huo, Iran imekuwa ikikaribisha makubaliano ya nyuklia ya haki, ya uadilifu na yenye manufaa kwa pande zote; makubaliano ambayo yatategemea usawa na yasiyo na shuruti, vitisho au kulazimishwa."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Tehran inataka mkataba unaohakikisha haki za Iran za teknolojia ya nyuklia ya amani na kuhakikisha kwamba haitatengeneza silaha za nyuklia.
Awali Sayyid Abbas Araqchi alikuwa ameonya kwamba, kutwisha diplomasia kupitia vitisho vya kijeshi hakuwezi kuwa na ufanisi au tija, akisema kwamba hakuna uamuzi wowote ambao umefanywa na Tehran juu ya kufanya mazungumzo na Marekani.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amepinga utumiaji wa nguvu kama njia ya kufikia malengo ya kisiasa, akisema mbinu kama hiyo haiwezi kutafsiriwa kama diplomasia.