Alkhamisi tarehe 17 Machi 2022
Leo ni Alkhamisi tarehe 14 Shaaban 1443 Hijria sawa na tarehe 17 Machi 2022.
Miaka 1386 iliyopita katika siku kama hii ya leo, ardhi ya Baitul Muqaddas huko Palestina ilikombolewa na Waislamu. Vita vya kwanza kati ya Waislamu na Warumi vilijiri huko kaskazini mwa Bahari Nyekundu baada ya kudhihiri Uislamu. Jeshi la Waislamu lilitoa pigo kwa Warumi na eneo la kusini mwa Palestina likakombolewa katika zama za utawala wa Umar bin Khattab. Baada ya kushindwa huko, mfalme wa Roma alituma jeshi kubwa katika ardhi za Palestina. Warumi walishindwa vibaya na jeshi la Kiislamu katika vita vilivyojiri huko Palestina na mwishoni mwa mapigano hayo, kamanda wa jeshi la Roma aliuawa na Damascus ikadhibitiwa na Waislamu.
Miaka 804 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 14 Shaaban mwaka 639 Hijria, alifariki dunia Ibn Yunus, faqihi, tabibu na mwanahesabati mashuhuri wa Kiislamu. Msomi huyo wa Kiislamu alitumia sehemu kubwa ya umri wake kujifunza elimu kutoka kwa baba yake na wanazuoni wengine wa zama hizo. Baada ya kustafidi na elimu katika zama ambazo wasomi wa Kiislamu walitia fora katika elimu ya sayansi na sanaa, Ibn Yunus alianza kufunza katika vyuo mbali mbali mjini Cairo nchini Misri. Mbali na kutabahari katika nyuga za fiqhi, sayansi na utabibu, msomi huyo wa Kiislamu alikuwa mtaalamu wa muziki. Miongoni mwa athari muhimu za mwanazuoni huyo wa Kiislamu, ni kitabu alichokipa jina la "Al-Asraaru Sultaniya" kinachozungumzia masuala ya unajimu.
Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, wawakilishi wa nchi za Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi na Luxembourg, walitia saini mkataba wa ushirikiano mjini Brussels, Ubelgiji. Katika mkataba huo uliojulikana kwa jina la "Mkataba wa Brussels", nchi hizo zilikubaliana kuanzisha mfumo wa ulinzi wa pamoja na kupanua uhusiano wao wa kiuchumi na kiutamaduni. Mkataba huo pia ndio uliokuwa chachu ya kuanzishwa kwa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO. Kwani ni baada ya hapo ndipo yalipofanyika mazungumzo kati ya Marekani, Canada na baadhi ya nchi wanachama wa Mkataba wa Brussels huko Washington, Marekani ambapo baadaye kuliundwa Shirika hilo la NATO mwezi Aprili 1949.
Na katika siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, sawa na tarehe 26 mwezi Esfand mwaka 1373 Hijria Shamsiya aliaga dunia Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ahmad Khomeini, mwana wa Imam Ruhullah Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sayyid Ahmad Khomeini alizaliwa mwaka 1324 Hijria Shamsiya katika mji mtukufu wa Qum nchini Iran na kuanza kujifunza elimu ya kidini kwa baba yake. Sayyid Ahmad Khomeini alikuwa na nafasi muhimu katika kuwaunganisha wanamapinduzi na Imam Khomeini wakati wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.