May 04, 2022 02:34 UTC
  • Jumatano tarehe 4 Mei 2022

Leo ni Jumatano tarehe 2 Shawwal 1443 Hijria iinayosadifiana na tarehe 4 Mei 2022.

Katika siku kama ya leo miaka 1016 iliyopita alizaliwa malenga na arif mkubwa wa Kiislamu wa karne ya tano Hijria Khaja Abdullah Ansari katika mji wa Herat nchini Afghanistan. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat. Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi na nudhumu, mashuhuri zaidi vikiwa ni "Munajat Nameh", "Mohabbat Nameh" na "Zadul Arifin". Vilevile ameandika tafsiri ya Qur'ani Tukufu aliyoipa jina la "Kashful Asrar."

Khaja Abdullah Ansari

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita chama cha National Socialism cha Ujerumani mashuhuri kwa jina la chama cha Nazi, kilivunjwa rasmi nchini humo. Kwa utaratibu huo kipindi cha utawala wa kidikteta, ukandamizaji na mabavu cha chama hicho ambacho kiliingia madarakani tangu mwaka 1932 nchini Ujerumani, kilifikia ukingoni. Si vibaya kuashiria hapa kuwa, chama cha Nazi kiliundwa mwezi Oktoba mwaka 1920 baada ya kuongezeka harakati ya kisiasa za Munich. Hadi mwaka 1929 chama hicho kilikuwa na wanachama laki moja na 76 elfu tu lakini mwaka 1933 idadi hiyo iliongezeka na kufikia milioni mbili na kuongezeka zaidi hadi kufikia milioni sita katika miaka iliyofuata. Inaelezwa kuwa, chama hicho kilikuwa na lengo la kuyaunganisha mataifa yanayozungumza Kijerumani na kuanzisha dola moja lenye nguvu ambalo lingeweza kupanua mipaka yake. Hata hivyo baada ya kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia chama hicho cha Nazi kilisambaratika na kutoweka.

Tarehe 4 Mei miaka 52 iliyopita wanafunzi wanne wa Chuo Kikuu cha serikali cha Kent katika jimbo la Uhio nchini Marekani waliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Gadi ya Taifa na wengine kadha wakajeruhiwa katika maandamano ya Wamarekani ya kupinga vita vya Vietnam. Kuanza mwaka 1969 Wamarekani hususan vijana walizidusha upinzani na maandamano ya kupinga vita na uvamizi wa nchi hiyo dhidi ya Vietnam. Maandamano hayo yalishadidi baada ya kufichuliwa habari ya mauaji ya mamia ya Wavietnam katika kijiji cha My Lai (My Lai massacre) na vilevile mwaka 1970 baada ya kuchapishwa habari ya kupanuka zaidi vita vya Vietnam na kuingia Cambodia.

Mauaji ya Chuo Kikuu cha Kent

Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, Josip Broz Tito, kiongozi wa Yugoslavia na mmoja wa waasisi wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM alifariki dunia. Wakati wa kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1915, Tito aliyekuwa akipigana dhidi ya Russia alitiwa mbaroni na baada ya kuachiliwa huru akiwa na Wakomonisti alipigana vita dhidi ya utawala wa Tzar. Kwa muda fulani, Tito alikuwa na nafasi muhimu kkatika Chama cha Kikomonisti cha Yugoslavia na alifungwa jela miaka 6 kwa kosa hilo. Tito aliiongoza Yugoslavia kwa muda wa miaka 35. Josip Broz Tito aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 88 baada ya kuugua kwa muda mrefu. 

Josip Broz Tito

Na siku kama ya leo miaka 41 iliyopita ndege iliyokuwa imembeba waziri wa mambo ya nchi za nje wa Algeria Bin Yahya ilitunguliwa na ndege za kivita za utawala wa Saddam Hussein wa Iraq baada ya kutembelea Iran. Baada ya tukio hilo mjumbe maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiongoza jumbe kadhaa alikwenda kukagua eneo la tukio hilo. Maafisa wa Iran walitangaza kuwa, nyaraka zilizopatikana zilionyesha kuwa, ndege za kivita za Iraq zilikuwa zikiifuatilia ndege hiyo ya Bin Yahya. Shambulizi la ndege za kivita za Iraq dhidi ya ndege iliyokuwa imembeba waziri wa mambo ya nje wa Algeria liliichafua sana sura ya Iraq katika macho ya walimwengu.

Bin Yahya

 

Tags