Jun 19, 2022 02:21 UTC
  • Jumapili, Juni 19, 2022

Leo ni Jumapili mwezi 19 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah mwaka 1443 Hijria, mwafaka na tarehe 19 Juni mwaka 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 725 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Kamaldeen Farsi mwanahisabati mashuhuri wa Kiirani.  Kamaldeen Farsi aliyekuwa amebobea pia katika elimu ya fizikia alifanya safari wakati wa ujana wake katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Licha ya kuwa umri wake hapa duniani ulikuwa mfupi, lakini ameacha athari zenye thamani kubwa katika elimu ya hisabati na utamabuzi wa nuru. Kitabu cha Tadhkirat al-Ahbab ndio kitabu muhimu zaidi cha msomi huyo wa Kiislamu. 

Kamaldeen Farsi

##########

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, sawa na tarehe 29 Khordad 1356 Hijria Shamsia, alifariki dunia Dakta Ali Shariati mwandishi na msomi wa zama hizi wa Kiirani mjini London, Uingereza. Dakta Shariati alipata elimu yake ya juu katika taaluma ya fasihi sambamba na kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya utawala wa mfalme hapa nchini. Dakta Shariati alikuwa bega kwa bega na Shahidi Mutahhari na Shahidi Bahonar, katika kuanzisha Husseiniya ya Ershad mjini Tehran kwa shabaha ya kuzikomaza fikra za tabaka la vijana. Ameandika zaidi ya vitabu 200 na miongoni mwao ni 'Uislamu na Mwanadamu', 'Historia ya Ustaarabu' na 'Fatima ni Fatima'.

Dakta Ali Shariati

 

##########

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita nchi ya Kuwait iliyoko katika eneo la Ghuba ya Uajemi ilijipatia uhuru baada ya kufutwa makubaliano ya ukoloni ya mwaka 1899 kati ya Uingereza na Kuwait. Katikati ya karne 18, iliasisiwa silsila ya al Swabah nchini humo na ilipofikia mwishoni mwa karne ya 19, Kuwait iliomba uungaji mkono wa Uingereza kwa shabaha ya kukabiliana na dola la Othmaniya. Mwaka 1899, Uingereza na Kuwait zilifanya makubaliano ambayo yaliiweka Kuwait chini ya ukoloni wa Uingereza.

Bendera ya Kuwait

 

##########

Na siku kama ya leo miaka 155 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Juni 1867, Maximilian mwana wa mfalme wa Austria ambaye aliikalia kwa mabavu Mexico, alinyongwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo. Baada ya Benito Juarez kujinyakulia urais wa Mexico mwaka 1855, aliwakata mikono wazungu na kupunguza nguvu za Kanisa nchini Mexico. Hatua hiyo iliwakasirisha mno wazungu na wakoloni wa Ulaya waliokuwa wakiongozwa na Ufaransa, na kulazimika kutuma jeshi nchini Mexico kwa shabaha ya kulihami Kanisa pamoja na wawekezaji nchini humo.

Maximilian

 

Tags