Aug 20, 2022 02:42 UTC
  • Jumamosi, 20 Agosti, 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 22 Muharram 1444 Hijria sawa na tarehe 20 Agosti 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 984 iliyopita alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Muhammad bin Hassan Tusi, ambaye ni mashuhuri kwa jina la Sheikhul Twaaifa. Sheikh Tusi alizaliwa katika mji wa Tus kaskazini mwa Iran na akaelekea Iraq kwa ajili ya kutafuta elimu ya juu baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa Iraq na miaka kadhaa baadaye akaweka msingi wa chuo kikuu cha kidini cha Najaf. Kituo hicho cha kidini kina historia ya miaka elfu moja na ni moja ya vituo muhimu mno vya elimu ya Kiislamu. Sheikh Tusi ameandika vitabu vingi sana katika taaluma mbalimbali. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni tafsiri ya Qur'ani tukufu ya al Tibyan na vitabu vya hadithi na fiqhi vya al Istibsar na al Tahdhiib. ***

Sheikh Muhammad bin Hassan Tusi

 

Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, mji mkuu wa Ubelgiji Brussels ulidhibitiwa na vikosi vya Ujerumani. Huu ulikuwa mji mku wa kwanza kukaliwa kwa mabavu na Ujerumani wakati wa kujiri vita vikuu vya kwanza vya dunia. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 34 iliyopita Marekani ilikiri kwamba ilifanya makosa kuishambulia ndege ya abiria ya Iran hapo tarehe 3 Julai mwaka 1988. Siku hiyo ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege ya Iran iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas kusini mwa Iran na kuelekea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, ilishambuliwa kwa makombora mawili kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi. Manowari ya kijeshi ya Marekani, USS Vincennes, ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi watu 298 waliokuwemo. Shambulio hilo lilionyesha wazi unyama wa serikali ya Marekani na ukatili wake hata kwa wanawake na watoto wadogo waliokuwemo ndani ya ndege hiyo. Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho kilichoonekana na serikali ya Washington kuwa eti ni cha kishujaa. ***

 

Na miaka 30 iliyopita, Estonia ambayo ni miongoni mwa nchi za Baltic huko magharibi mwa Urusi ya zamani ilijitangazia uhuru. Estonia ilikuwa chini ya satwa ya Urusi ya zamani kufuatia makubaliano ya siri yaliyofikiwa mwaka 1939 Miladia kati ya Hitler na Stalin. Mwaka 1991, karibu asilimia 80 ya wananchi wa Estonia walishiriki kwenye kura ya maoni na kupelekea kutangazwa uhuru wa nchi hiyo katika siku kama hii. ***

Estonia