Sep 02, 2022 02:26 UTC
  • Ijumaa, 02 Septemba, 2022

Leo ni Ijumaa Mwezi Tano Mfunguo Tano Safar, 1444 Hijria sawa na tarehe Pili Septemba 2022 Miladia

Miaka 1383 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani mwezi tano Safar mwaka 61 Hijria, Ruqayya, binti mdogo wa Imam Hussein (AS) alikufa shahidi katika mji wa Sham. Ruqayya Khatun au Fatima bintul-Hussein (AS), maarufu kama Fatima Saghira, ni binti wa Imam Hussein (AS) na mama yake alikuwa akiitwa Ummu Is-haq bint Talha. Inaelezwa kwamba wakati alipokufa shahidi, Ruqayya alikuwa na umri wa miaka mitatu, minne au saba. Imam Hussein (AS) alikuwa akimhurumia sana binti yake huyo na yeye Ruqayya pia alikuwa akimpenda sana baba yake. Aliandamana na baba yake, kaka zake, ami zake pamoja na watu wengine wa ukoo wa Mtume SAW kuelekea Karbala. Baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein pamoja na masahaba zake, watu wa nyumba ya Mtume SAW waligeuzwa mateka, wakachukuliwa na watu wa Kufa na kupelekwa mjini Sham. Alipofika Sham, Ruqayya Khatun alikuwa usiku na mchana akimlilia na kumtaka baba yake. Kauli yenye nguvu ni kwamba wakati wakiwa kwenye magofu ya Sham, alipokiona kichwa kilichokatwa cha baba yake, akasemezana nacho kwa huzuni na majonzi makubwa, kisha akaweka mdomo wake karibu na mdomo wa baba yake, alilia sana mpaka akazirai. Alipotikiswa, ilibainika kuwa ameshaaga dunia. Ziara la Ruqayyah (as), ambalo ni moja ya maziara wanayoyazuru Waislamu wa Kishia, liko katika mji mkuu wa Syria Damascus, umbali wa mita 300 kaskazini mashariki ya msikiti maarufu wa Umawiyah.

Ziara la Ruqayya (as)

 

Miaka 893 iliyopita katika siku kama hii ya leo, mwezi 5 Safar mwaka 551 Hijria alizaliwa Kamal al-Din Abu Imran, maarufu kama "Ibn Yunus", faqihi, tabibu na mwanahisabati, katika mji wa Mosul kaskazini mwa Iraqi. Baada ya kumaliza masomo ya msingi ya dini, alijifunza hisabati na baada ya kupata ujuzi katika fani hiyo, akaanza kufundisha somo hilo. Ibn Yunus alihesabika kuwa miongoni mwa wanasayansi watajika wa zama zake. Alikuwa gwiji katika fani ya fiqhi za madhehebu mbalimbali za Kiislamu na dini nyinginezo za tauhidi, kiasi kwamba hata Mayahudi na Wakristo walikuwa wakimwendea kwa ajili ya kutafsiriwa Taurati na Injili. Faqihi na mwanahisabati huyo Muislamu alikuwa na kipaji maalum pia katika uga wa fasihi na akisanifu mashairi. Miongoni mwa athari alizoacha Ibn Yunus, ni pamoja na vitabu vya "Asraru-Sultaniyya" cha elimu ya nyota na "Sharh al-Amal al-Handasiyyah" kinachohusiana na hisabati.

Kamal al-Din Abu Imran, maarufu kama "Ibn Yunus"

 

Miaka 221 iliyopita katika siku kama ya leo mnamo Septemba 2, 1801, baada ya mapigano kadhaa kati ya majeshi ya utawala wa Othmaniyya yakishirikiana na jeshi la Uingereza kwa upande mmoja dhidi ya majeshi ya Ufaransa katika upande mwingine, hatimaye Wafaransa walishindwa na kuondoka Misri moja kwa moja. Ikumbukwe kuwa, baada ya Napoleon kuikalia kwa mabavu ardhi ya Misri, Uingereza, ambayo wakati huo ilikuwa mpinzani na mshindani mkuu wa Ufaransa katika nyanja za kiuchumi na kijeshi, ilihisi maslahi yake yako hatarini. Kwa sababu hiyo, na ili kuwatimua Wafaransa Misri na kulizuia jeshi lao lisisonge mbele zaidi, Uingereza iliamua kushirikiana na dola la Othmaniyya. Baada ya Napoleon kurejea Ufaransa na majeshi yake kubaki bila uongozi wake yalianza taratibu kupoteza uwezo wake huko Misri; na kutokana na kudhoofika kulikosababishwa na mashambulizi ya mfululizo ya Waothmania na Waingereza, hatimaye majeshi ya Ufaransa yalilazimika kuondoka nchini Misri.

Bendera ya Misri

 

Miaka 85 iliyopita mnamo Septemba Pili, 1937 aliaga dunia Pierre de Coubertin, mwanahistoria wa Ufaransa na mwanzilishi wa Michezo ya Olimpiki ya kisasa. Alizaliwa mwaka 1863; na baada ya kuhitimu masomo yake akafanya kazi ya ualimu. Kutokana na kutalii katika uwanja wa historia na kupendezwa na Michezo ya Olimpiki iliyokuwa ikifanyika Ugiriki ya Kale, Coubertin alitia nia ya kuifufua michezo hiyo. Kwa sababu hiyo, akaitaka serikali ya Ufaransa ianzishe tena michezo hiyo na yeye mwenyewe akaandika hati ya kanuni zitakazotumika. Mnamo mwaka 1896, Coubertin aliitisha Kongamano la kwanza la Kimataifa la Olimpiki nchini Ufaransa na kusisitiza kuwa michezo hiyo inalenga kuinua hadhi ya binadamu na kuleta suluhu na amani baina ya mataifa. Kuanzia mwaka 1898, Mashindano ya Olimpiki yalifanyika rasmi kwa kutumia sheria mpya na katika michezo mipya mbalimbali; na ndoto aliyokuwa nayo Coubertin ikatimia. Coubertin aliendelea kuwa mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki hadi mwaka 1925.

Pierre de Coubertin

 

Na miaka 60 iliyopita kulingana na kalenda ya hijria shamsia, yaani tarehe 11 Shahrivar 1341 tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.2 kwa kipimo cha rishta lilitikisa mji wa Buin Zahra kaskazini magharibi mwa Iran. Katika tetemeko hilo la kutisha, zaidi ya watu elfu 20 waliuawa na maelfu ya wengine walijeruhiwa. Kutokea kwa tetemeko hilo nyakati za usiku kuliwafanya watu wachache tu waweze kunusuru maisha yao. Katika tetemeko la ardhi la Bouin Zahra, vijiji 120 viliteketea kikamilifu na mamia ya nyumba ziliharibiwa vibaya. Baada ya tukio hili, bila kupoteza muda, watu wa Iran walipeleka misaada yao katika eneo hilo na kukimbilia kuwasaidia wananchi wenzao waliojeruhiwa. Buin Zahra ni la matetemeko ya ardhi kwani mwaka 2013 lilipatwa na zilzala nyingine iliyoua watu wapatao 300.

Tetemeko la ardhi katika mji wa Buin Zahra kaskazini magharibi mwa Iran

 

 

Tags