Ijumaa tarehe 14 Oktoba 2022
Leo ni Ijumaa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 14 Oktoba 2022.
Siku kama ya leo miaka 1497 iliyopita kwa mujibu wa nukuu za maulama wengi wa Kiislamu, alizaliwa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Makka. Baba yake, Abdullah alifariki dunia kabla ya kuzaliwa Mtume na mama yake, Amina binti Wahab, alifariki dunia mtukufu huyo akiwa na umri wa miaka sita. Katika kipindi cha mwanzoni mwa ujana wake, Muhammad alikuwa akijitenga na jamii ya kijahilia ya watu wa Makka na kwenda kwenye pango la Hiraa lililoko karibu na mji wa Makka na kuketi huko kwa masaa kadhaa akitafakari katika maumbile ya dunia na kufanya ibada. Alipotimiza umri wa miaka 40, Malaika Jibrilu alimteremkia mtukufu huyo akiwa katika pango hilo na kumpa ujumbe wa Mola Muumba. Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) alikumbana na mashaka mengi katika jitihada zake za kufuta ibada ya masanamu na kueneza imani ya Tauhidi na kumwabudu Mungu Mmoja.

Siku kama hii ya terehe 17 Rabiul Awwal miaka 1361 iliyopita pia alizaliwa mjukuu wa mtukufu huyo Imam Ja'far Swadiq (as) katika mji mtakatifu wa Madina. Kipindi cha maisha yake kilikuwa zama za kuchanua elimu na maarifa, tafsiri ya Qur'ani na kusambaa elimu mbalimbali. Imam Sadiq (as) alitumia fursa hiyo ambayo ilisadifiana na kuanza kuporomoka utawala wa Bani Umayyah na kuchukua madaraka utawala wa Bani Abbas, kwa ajili ya kueneza maarifa asili ya Kiislamu na kulea kizazi cha wasomi na maulama katika nyanja mbalimbali. Kwa minasaba hii adhimu Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran inatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote duniani.

Siku kama ya leo miaka 208 iliyopita, mkutano wa kihistoria wa Vienna ulifanyika kwa lengo la kujadili “Ulaya baada ya Napoleon Bonaparte”. Baada ya kujiuzulu na kubaidishwa Bonaparte mwezi Aprili mwaka 1814, mkutano wa kihistoria wa Vienna ulianza kufanyika katika siku kama ya leo katika mji mkuu wa Austria Vienna ili kuchukua maamuzi kuhusu ardhi zilizokaliwa kwa mabavu na Ufaransa katika kipindi cha vita vya Bonaparte. Wakati wa kuendelea mkutano huo, Napoleone Bonaparte alikimbia kutoka mahala alipokuwa amebaidishiwa na mwishoni mwa mwezi Februari mwaka 1815 kwa mara nyingine tena akashika hatamu za uongozi kwa muda mfupi, kipindi ambacho kiliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la “Utawala wa Siku 100”. Aliposhika tena hatamu za uongozi alijianda kuwashambulia maadui zake.
Siku kama ya leo miaka 89 iliyopita, kwa amri ya Adolf Hitler Kansela wa wakati huo wa Ujerumani, nchi hiyo ilijitoa katika Jumuiya ya Kimataifa. Kuingia madarakani Adolf Hitler akiwa Kansela wa Ujerumani kulizushha wasiwasi mkubwa katika kila kona ya Ulaya kutokana na mipango yake ya kijeshi. Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutiwa saini mkataba wa amani wa Warsaw ambao ulidhibiti sana zana za kijeshi za Ujerumani, Hitler na viongozi wengine wa Kinazi walikasirishwa mno na hatua hiyo.
Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, Wazayuni wa Israel walivamia kijiji cha Qibya kilichoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kufanya jinai kubwa za kutisha. Katika mashambulizi na uvamizi huo ulioendelea katika kijiji hicho kwa muda wa siku mbili, Wazayuni walitekeleza mauaji na ukatili mkubwa dhidi ya raia wa Kipalestina wasio na hatia. Mbali na Wazayuni hao kuwaua na kuwajeruhi kwa umati raia wa Kipalestina zaidi ya 42, askari wa Israel waliokuwa wakiongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ariel Sharon, walibomoa makumi ya nyumba na shule za kijiji hicho. Mauaji hayo ya halaiki ni miongoni mwa mifano ya ugaidi wa utawala ghasibu wa Israel hususan wa Waziri Mkuu wa zamani wa utawala huo, Ariel Sharon.
Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, yaani tarehe 14 Oktoba mwaka 1964 Nikita Khrushchev, Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti cha Umoja wa Sovieti aliuzuliwa kutoka katika wadhifa wake huo. Nikita Khrushchev alifanikiwa kuwa mwanachama wa ofisi ya kisiasa ya Chama cha Kikomonisti mwaka 1939 na baada ya kufariki dunia Joseph Stalin mwaka 1953, Nikita alijitokeza kuwa shakhsia aliyekuwa na nguvu katika umoja wa Sovieti na kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti na baadaye Waziri Mkuu wa shirikisho hilo.
Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 89 Ayatullah Muhammad Baqir Muhsini Malayeri, faqihi mkubwa wa Iran. Ayatullah Malayeri aliyekuwa mashuhuri katika hawza ya kielimu ya mjini Qum, Iran alizaliwa mjini Najaf, Iraq na katika familia ya kielimu, hapo mwaka 1285 Hijiria Shamsia. Akiwa kijana mdogo alielekea mjini Malayer, ambao ni makao makuu ya mkoa wa Hamadan nchini hapa akiwa pamoja na baba yake na baada ya kuhitimu masomo ya msingi alielekea mjini Mash'had kwa ajili ya kuendelea na masomo ya hawza. Wakati wa kuasisiwa hawza ya kielimu ya Qum, Ayatullah Muhammad Baqir Muhsini Malayeri naye alielekea mji huo na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo akiwemo Abdul-Karim Haeri Yazdi na Seyyed Hussein Borujerdi na kufikia daraja za juu za kielimu. Aidha Ayatullah Malayeri alitambuliwa kwa uchaji-Mungu mkubwa katika zama zake.
Na katika siku kama ya leo miaka 23 iliyopita alifariki dunia kiongozi wa zamani wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Nyerere Alizaliwa Butiama huko Mara mwaka 1922. Mwaka 1955 aliingia katika ulingo wa siasa huku akiongoza chama cha (Tanganyika Africa Nation Union) TANU. Mwaka 1961 Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na mwaka mmoja baadaye akawa rais wa nchi hiyo. Kutokana na juhudi zake mwaka 1964 ziliungana Tanganyika na Zanzibar na kuunda nchi moja ya Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania. Nyerere aliendelea kuongoza nchi hiyo hadi mwaka 1985 ambapo aliachia hatamu za uongozi. Licha ya hayo, lakini Nyerere aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Tanzania hadi alipofariki dunia.