Oct 21, 2022 22:53 UTC
  • Jumamosi, 22 Oktoba, 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 25 Mfunguo Sita Rabiu Awwall 1444 Hijria sawa na tarehe 22 Oktoba 2022 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 1008 iliyopita sawa na tarehe 25 Rabiul Awwal mwaka 436 Hijiria alifariki dunia Sayyid Murtadha Alamul Huda mwanafunzi mashuhuri wa Sheikh Mufid. Alizaliwa mwaka 355 Hijiria huko Baghdad na alijifunza elimu za zama zake. Baadaye alianzisha kituo cha elimu ambacho kilikuwa kikihudhuriwa na watu wenye itikadi na mielekeo tofauti. Sayyid Murtadha ameacha vitabu vingi na miongoni mwa vitabu hivyo ni Tanzihil Anbiyah, Taqribul Usul pamoja na kitabu cha maashairi chenya beti elfu 20. ***

Sayyid Murtadha Alamul-Huda

 

Katika siku kama ya leo miaka 116 iliyopita, Paul Cezanne mchoraji maarufu wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 67. Alikuwa na shauku na mapenzi makubwa na fani ya uchoraji tangu akiwa mdogo, lakini kutokana na msisitizo wa baba yake aliingia Chuo Kikuu na kusoma taaluma ya sharia. Hatimaye akiwa na umri wa miaka 24, baba yake alimruhusu kuendelea na masomo katika taaluma ya uchoraji. Mwanzoni mabango ya uchoraji ya Paul Cezanne hayakupata wafuasi wengi na athari zake za uchoraji zilikabiliwa na ukosoaji mkubwa. Mwenendo huo uliendelea hadi alipofikisha umri wa miaka 50 ambapo hatua kwa hatua alianza kupata umashuhuri kutokana na kuuza mabango yake ya uchoraji. ***

Paul Cezanne mchoraji maarufu wa Ufaransa

 

Tarehe 30 Mehr miaka 70 iliyopita, Dakta Hussein Fatimi, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Dakta Musadiq, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Iran wakati huo alitangaza habari ya kukatwa uhusiano wa kisiasa kati ya Iran na Uingereza. Uamuzi huo ulikabidhiwa kwa balozi mdogo wa Uingereza mjini Tehran, baada ya kuidhinishwa na baraza la mawaziri. Dakta Fatimi alisema Tehran imeamua kukata uhusiano na Uingereza kutokana na upuuzaji wa serikali ya London kwa matakwa ya wananchi wa Iran ya kujipatia haki zao, hususan katika uwanja wa kutaifisha sekta ya mafuta. Dakta Fatimi aliwataka viongozi wa London wabadili siasa zao kuhusiana na Iran. ***

Dakta Hussein Fatimi

 

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, aliaga dunia Arnold Joseph Toynbee mwanahistoria mtajika wa Uingereza. Alizaliwa mwaka 1889. Toynbee alikuwa akifundisha taaluma ya Historia ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha London. Msomi huyo ameandika vitabu vingi katika uga wa historia na baadhi ya vitabu vyake ni A Study of History, Change and Habit, Choose Life na Civilization on Trial. ***

Arnold Joseph Toynbee

 

Miaka 11 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sultan bin Abdul-Aziz Aal Saud aliyekuwa mrithi wa kiti cha Ufalme wa Saudia. Sultani alikuwa mtoto wa 15 wa kiume wa Mfalme Abdul-Aziz na mama yake ni Hussa Bint Ahmed Al-Sudairi. Vyombo vya Saudi vilitangaza kuwa, mwanamfalme Sultan bin Abdul-Aziz Aal Saud aliaga duniia katika moja ya hospitali mjini New York Marekani. Sultan bin Abdul-Aziz aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 85 baada ya maradhi ya saratani kuenea katika mwili wake wote. ***

Sultan bin Abdul-Aziz Aal Saud

 

Na tarehe 22 Oktoba ni siku ya kitaifa ya Vatican, inayohesabiwa kuwa nchi ndogo zaidi duniani. Vatican ina ukubwa wa chini ya nusu kilomita mraba, na jamii ya watu karibu elfu moja huko kusini mwa bara Ulaya. Nchi hiyo iko eneo la magharibi ndani ya mji mkuu wa Italia, Roma. Lugha rasmi ya Vatican ni Kitaliano. Wakazi wa Vatican ni wafuasi wa madhehebu ya Katoliki na wanatumia sarafu ya Yuro. Nchi hiyo ndogo ya Vatican inatawaliwa na serikali ya kidini ambayo inaongozwa na Papa wa Kanisa Katoliki. Vatican inatajwa kuwa kituo kikuu cha kupanga mikakati ya madhehebu ya Katoliki katika maeneo mbalimbali duniani. Nchi ya Vatican ilijitenga na Italia mwaka 1929 na tarehe 22 Oktoba ya kila mwaka ambayo kwa hakika ni siku ya kuchaguliwa Papa John Paul wa Pili hapo mwaka 1978, imetangazwa kuwa ni Siku ya Kitaifa ya Vatican. ***

Bendera ya Vatican