Jumapili tarehe 23 Oktoba 2022
Leo ni Jumapili tarehe 26 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1444 Hijria sawa na Oktoba 23 mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 1100 iliyopita yaani tarehe 26 Rabiul Awwal mwaka 344 Hijiria alifariki dunia Ibn Sammak, mtaalamu mkubwa wa masuala ya itikadi ya Kiislamu huko Baghdad. Historia haijaweka wazi tarehe na mahala alipozaliwa msomi huyo, lakini ripoti zinasema kwamba aliishi mjini Baghdadi, Iraq na kupata elimu na maarifa kwa wasomi wa mji huo. Vilevile historia inasema Ibn Sammak alilea wasomi wengine mashuhuri akiwemo Haakim Nishaburi. Miongoni mwa vitabu vya Ibn Sammak ni kile cha "al Aamali" na vitabu vingine kadhaa kuhusu fadhila na matukufu ya Ahlulbait wa Mtume Muhammad (saw).

Miaka 150 iliyopita, aliaga dunia Theophile Gautier, malenga na mwandishi wa Kifaransa. Gautier alizaliwa mwaka 1811 na kuhitimu masomo yake huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa. Theophile Gautier kwa muda fulani alikuwa mwandishi wa gazeti na alikuwa na hamu kubwa ya kuwa mchoraji au mwanamuziki. Lakini hatimaye alijifunza fasihi hususan mashairi na kuacha athari maarufu katika uwanja huo.
Siku kama ya leo miaka 114 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani, alimu na msomi mkubwa wa Kiislamu. Abul-Makaarim Zanjani alizaliwa mwaka 1255 Hijiria mjini Zanjani, kaskazini magharibi mwa Iran ambapo baada ya kuhitimu masomo yake ya awali alielekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo ya hawza mjini hapo. Akiwa mjini Najaf, Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani alipata kusoma kwa maulama wakubwa kama vile Morteza Ansari. Aidha baada ya kufariki dunia baba yake, Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani alichukua jukumu la umarjaa wa masuala ya kidini na sheria za Kiislamu hususan mjini Zanjani. Katika kipindi cha mapinduzi ya kikatiba, msomi huyo na kama walivyokuwa wasomi wengine, alisimama kupambana na udikteta wa wakati huo hapa nchini Iran. Vitabu vya 'Makhaarijur-Rahman' na 'Miftaahud-Dhafar' ni miongoni mwa athari za Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani.
Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, vita vya kihistoria vilivyopewa jina la al-Alamein vilitokea katika mji wenye jina kama hilo huko kaskazini mwa Misri kati ya wanajeshi wa Uingereza na jeshi la Manazi wa Ujerumani. Vita hivyo vilimalizika baada ya kushindwa jeshi la Ujerumani, japokuwa mapigano kati ya pande hizo mbili yaliendelea katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Afrika. Amani kamili ilipatikana katika maeneo hayo baada ya kushindwa kikamilifu jeshi la Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Na miaka 45 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Sayyid Mustafa Khomeini, mtoto wa Imam Ruhullah Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa shahidi kufuatia njama ilizofanywa na askari usalama wa utawala wa Shah akiwa nyumbani kwake huko Najaf, moja kati ya miji mitukufu ya Iraq. Al Haj Mustafa Khomeini alizaliwa mwaka 1309 Hijria Shamsiya katika mji mtakatifu wa Qum na baadaye akajiunga na chuo cha elimu ya dini cha mji huo kwa ajili ya masomo ya juu baada ya kuhitimu elimu ya msingi. Alikuwa hodari mno na alifikia daraja ya juu ya kielimu ya Ijtihadi akiwa na umri wa miaka 27. Ayatullah Mustafa Khomeini alikuwa pamoja na baba yake Imam Khomeini katika kipindi chote cha mapambano dhidi ya utawala wa Shah.