Jumatatu tarehe 24 Oktoba 2022
Leo ni Jumatatu tarehe 27 Rabiul Awwal 1444 Hijria sawa na tarehe 24 Oktoba 2022.
Tarehe 27 Rabiul Awwal miaka 1081 iliyopita alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiarabu Abul Alaa al Maarry katika mji wa Maarrat al-Nu'man nchini Syria. Abul Alaa alifariki dunia mwaka 449 Hijria katika mji huo huo ulioko umbali wa kilomita 33 kusini mwa Halab (Aleppo). Baadaye alielekea Baghdad kwa ajili ya kukamilisha elimu ya juu. Licha ya kuwa kipofu tangu utotoni, lakini Abul Alaa alitokea kuwa mshairi mashuhuri na hodari wa zama zake. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri la "Risalatul Ghufran" na "al Aamali."
Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita sawa na tarehe Pili mwezi Aban mwaka 1307 Hijria Shamsia, Ayatullah Dakta Sayyid Muhammad Husseini Beheshti mwanafikra na mwanamapinduzi wa Iran alizaliwa huko Isfahan, moja kati ya miji ya katikati mwa Iran. Ayatullah Beheshti alilelewa katika familia ya kidini na alianza kujifunza masomo ya kidini akiwa kijana mdogo. Akiwa na umri wa miaka 18, alielekea katika mji wa kidini wa Qum nchini Iran na kusoma kwa maulamaa wakubwa wa mji huo akiwemo Imam Khomeini (RA). Wakati huo huo, Dakta Beheshti alitumia kipawa chake kikubwa na kuamua kuendelea pia na masomo ya Chuo Kikuu na kufanikiwa kupata shahada ya udaktari katika falsafa. Dakta Beheshti aliuawa shahidi akiwa na viongozi na shakhsiya wengine 72 wa Iran katika mkutano mwezi Tiir mwaka 1360 Hijria Shamsia baada kundi la kigaidi la Munafiqin kuripua bomu katika mkutano huo.
Tarehe 24 Oktoba miaka 93 iliyopita ulianza mgogoro mkubwa wa kiuchumi wa Marekani unaojulikana kwa jina la Wall Street. Kimsingi Wall Street ni mtaa mashuhuri mjini New York ambao kutokana na kuwa na taasisi nyingi kubwa za kifedha na kibenki unatambuliwa kuwa kituo muhimu sana cha kiuchumi cha Marekani. Kituo hicho cha kiuchumi kilikumbwa na mgogoro mkubwa wa kifedha wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia na baada yake. Oktoba 24 mwaka 1929 janga kubwa la kifedha liligubika makao ya hisa ya Marekani huko Wall Street na kupelekea kukosa kazi zaidi ya wafanyakazi milioni 13 wa Marekani, njaa kali, kufilisika kwa viwanda na mabenki na mamilioni ya watu kupoteza makazi na nyumba zao.

Katika siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, uliundwa Umoja wa Mataifa na kuchukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa. Wawakilishi wa mataifa yaliyoafikiana katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, yaani Marekani, Urusi, Uingereza na Ufaransa, waliandaa mazingira ya kuundwa umoja huo; na hatimaye katika mkutano uliofanyika San Francisco, Marekani, wawakilishi kutoka nchi 50 duniani walipitisha sheria za kuundwa umoja huo. Ijapokuwa umoja huo umefanikiwa katika baadhi ya mambo, lakini kuwepo haki ya veto kwa baadhi ya nchi ambazo ni Marekani, Russia, Uingereza, Ufaransa, na China kunalifanya Baraza la Usalama la umoja huo kufuata kibubusa siasa za nchi zenye haki ya kupiga kura ya turufu, na hasa Marekani.
Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, Iran ilifanikiwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa hati ya Umoja wa Mataifa, mlango wa kujiunga na umoja huo uko wazi kwa mataifa yote yanayopenda amani na ambayo yanakubaliana na sheria na maaamuzi ya taasisi hiyo. Nchini Iran, Umoja wa Mataifa una jumla ya ofisi 14 za uwakilishi na utendaji.
Siku kama ya leo Miaka 54 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa kituo cha kidini cha Najaf aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92. Baada ya kuaga dunia Ayatullah Burujerdi ambaye alikuwa mar'ja' mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, Ayatulah Hakim alichukua nafasi yake na kufuatwa na Waislamu wengi na hasa wa Iraq, kuhusiana na masuala ya kifik'hi. Alipambana vikali na kila kundi au watu waliojaribu kuharibu jina la Uislamu. Fatua yake mashuhuri ya kupinga fikra ya ukomunisti dhidi ya mafundisho ya dini ilileta mabadiliko makubwa nchin Iraq. Fatua hiyo pia ilimpelekea kutoa amri ya kupigana jihadi dhidi ya utawala haramu wa Israel. Ujenzi wa maktaba, shule na vituo vya kidini na kiutamaduni pamoja na uandishi wa vitabu kama vile Mustamsak Urwat al-Wuthqah na Nahjul Faqaha ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vilivyoandikwa na mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu.
Na miaka 48 iliyopita katika siku kama ya leo, vita vya nne baina ya Waarabu na Israel vilivyojulikana kwa jina la Vita vya Ramadhani vilifikia tamati. Tarehe 6 Oktoba 1973 Anwar Sadat Rais wa wakati huo wa Misri akiwa na lengo la kufidia kushindwa katika vita vya Waarabu na Israel mwaka 1967, alifanya mashambulio ya kushtukiza katika ngome za Israel katika Kanali ya Suez. Muda mchache baada ya mashambulio hayo, wanajeshi wa Syria nao walifanya mashambulio katika miinuko ya Golan ambayo ilikaliwa kwa mabavu na Israel katika vita vya mwaka 1967 na kufanikiwa kuwatimua wanajeshi wote wa utawala huo haramu kutoka katika maeneo waliokuwa wakiyadhibiti.