Ijumaa, Oktoba 28, 2022
Leo ni Ijumaa tarehe Pili Mfunguo Saba Rabiuthani 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 28 Oktoba 2022 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita Imam Ruhullah Khomeini alipinga vikali mpango wa Fahd bin Abdulaziz kuhusu mapatano ya Palestina na Israel. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na baada ya kutiwa saini mkataba wa Camp David baina ya serikali ya Misri na utawala ghasibu wa Israel chini ya upatanishi wa Marekani, tawala vibara za Kiarabu zilifuata nyayo za utawala wa Misri katika suala hilo. Wakati huo Fahd bin Abdulaziz aliyekuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, alitoa pendekezo la kutambuliwa rasmi utawala vamizi wa Israel, suala ambalo lilikabiliwa na upinzani mkali wa Waislamu kote duniani. Kwa msingi huo katika siku kama hii ya leo Imam Ruhullah Khomeini alitoa hotuba akisema: "Ni wajibu kwetu sisi na kwa kila Mwislamu kupinga mipango kama ule uliopendekezwa na Fahd. Tunawajibika kulaani mipango kama hii isiyokuwa na faida kwa watu wanaodhulumiwa. Jambo hatari sana kwa sasa ni makubaliano ya Camp David na mpango wa Fahd ambayo inaimarisha zaidi Israel na kudumisha jiani zake." Upinzani huo wa wazi wa Imam Khomeini na uungaji mkono wa Waislamu kote dunia kwa misimamo hiyo ya Imam ilikuwa sababu ya kukataliwa na kupingwa pendekezo hilo katika nchi nyingine.
Miaka 49 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Taha Hussein mwandishi mahiri na stadi wa Kimisri. Alizaliwa mwaka 1889 katika moja ya vijiji vya Misri. Taha Hussein ambaye alikuwa mtoto wa saba katika familia yake, alipofuka na kupoteza uwezo wa kuona akiwa na umri wa miaka mitatu. Hata hivyo Mwenyezi Mungu alimjaalia kipaji cha hali ya juu. Taha Hussein alifanikiwa kuhafidhi Qur’ani yote katika kipindi kifupi. Akiwa na umri wa miaka 14 alifaulu mtihani wa watahaniwa wa kuingia Chuo Kikuu cha al-Azhar na akiwa pamoja na kaka yake, alijishughulisha na kusoma masomo ya dini pamoja na lugha ya kigeni. Mwaka 1914 Taha Hussein alihitimu kwa alama nzuri na kutunukiwa shahada ya uzamivu yaani PhD. Wakati huo Chuo Kikuu cha Taifa cha Misri kilichukua uamuzi wa kuipeleka timu ya wahadhiri nchini Ufaransa kwa ajili ya kufundisha historia ya Mashariki. Akiwa ahuko alijifunza histotia ya Ugiriki na Roma ya kale pamoja na lugha ya Kigiriki. Mwaka 1959 mwandishi huyo mahiri wa Kimsri alinutukiwa tuzo ya Nobel kutokana na mchango wake katika uga wa fasihi. Taha Husserin ameandika vitabu vingi katika taaluma za fasihi, sayansi ya siasa na historia.
Tarehe 28 Oktoba miaka 74 iliyopita wakati wa vita vya kwanza kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Waarabu, wanajeshi wa utawala huo waliwaua kwa umati wakazi wa kijiji cha al Dawayima huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wazayuni hao walivamia msikiti wa kijiji hicho na kuwauwa shahidi Waislamu 75 raia wa Palestina waliokuwa wakiswali. Vilevile waliwaua kwa umati watu wa familia 35 waliokuwa wamekimbilia hifadhi katika pango moja nje ya kijiji hicho. Askari jeshi wa utawala haramu wa Israel walikisawazisha na ardhi kijiji hicho baada ya kuwaua kwa umati wakazi wake wote.
Tarehe 28 Oktoba mwaka 1962 yaani siku kama hii ya leo miaka 60 iliyopita, ulihitimishwa mgogoro wa makombora wa Cuba baada ya kiongozi wa wakati huo wa Urusi, Nikita Khrushchev kuamuru kurejeshwa nyumbani meli zilizokuwa na makombora ya nyuklia. Hatua ya Urusi ya kujenga vituo kadhaa vya makombora ya nyuklia nchini Cuba katika umbali wa kilomita 90 kutoka Marekani ilizusha mgogoro mkubwa wa makombora uliokaribia kuitumbukiza dunia katika vita vya nyuklia. Wakati huo Marekani na Russia zilitishia kushambuliana kwa makombora ya nyuklia na kuzusha hofu kubwa hususan kwa watu wa Marekani, Russia na nchi za Ulaya. Hatimaye tarehe 28 Oktoba mwaka 1962 Nikita Khrushchev alitoa amri ya kurejea nchini meli zote zilizokuwa na makombora ya nyuklia na kufungwa vituo vya makombora vya Urusi nchini Cuba.
Katika siku kama ya leo miaka 82 iliyopita wanajeshi laki mbili wa Italia waliishambulia Ugiriki kwa amri ya Musolini, kiongozi wa serikali ya kifashisti ya nchi hiyo. Mashambulizi hayo yalifanywa wakati Vita vya Pili vya Dunia vilipokuwa vimepamba moto kwa kuchochewa na Ujerumani ya Kinazi, nchi muitifaki wa Italia huko Ulaya.
Na siku kama ya leo miaka 6 iliopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Taqi Tabatabai Qumi mmoja wa Marajii Taklidi wa Kishia. Ayatullah Taqi Tabatabai Qumi ambaye ni mashuhuri zaidi kwa jina la Haji Agha Taqi Qumi alizaliwa mwaka 1301 Hijria Shamsia katika mji wa Mash’had. Baba yake ni Sayyid Hussein Tabatabai Qumi aliyekuwa mmoja wa Marajii wakubwa wa Taklidi ambaye kutokana na kupinga amri ya Reza Shah mfalme wa wakati huo wa Iran ya kuondolewa hijabu kwa nguvu, alilazimika kuhama Iran na kuelekea Iraq. Sayyid Taqi alisoma masomo ya awali na ya utangulizi kwa baba yake na alipoelekea Iraq alisoma kwa walimu mahiri wa zama hizo kama Sayyid Muhammad Hadi Milani, Sayyid Abdul-Hadi Shirazi, Hussein Hilli, Muhammad Kadhim Shirazi na wengineo.