Jumapili, Oktoba 30, 2022
Leo ni Jumapili tarehe Nne Mfunguo Saba Rabiuthani 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 30 Oktoba 2022 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1271 iliyopita, alizaliwa Sayyid Abdul Adhim al Hassani aliyekuwa mmoja wa wajukuu wa Imam Hassan al Mujtaba (a.s) huko katika mji wa Madina. Sayyid Abdul Adhim alikuwa mmoja kati ya shakhsiya walioaminiwa na Imam al Hadi (as) na alinukuu hadithi moja kwa moja kutoka kwa maimamu watukufu kama vile Ridha, Jawad na al Hadi (as). Sayyid Abdul Adhim alihamia Iran kutokana na pendekezo la Imam al Hadi (as) kwa ajili ya kuwaongoza Waislamu na akaishi katika mji wa Rei karibu na Tehran ya sasa. Sayyid Abdul Adhim aliuawa shahidi mwezi Shawwal mwaka 250 Hijria. Kaburi la mtukufu huyo liko katika eneo la Rei na ni miongoni mwa maeneo yanayotembelewa na Waislamu kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Siku kama ya leo, miaka 931 iliyopita alizaliwa mjini Baghdad Abubakr Muhammad Anbari, faqihi, mtaalamu wa hadithi na lugha. Anbari alipata kusoma elimu ya dini, nahwu na lugha akiwa kijana mdogo kutoka kwa baba yake. Baada ya kuhitimu masomo yake katika nyanja tofauti, alianza kufundisha na kulea wanafunzi wengi. Alitokea kuwa faqihi mkubwa na kutabahari katika elimu ya lugha ya Kiarabu. Msomi huyo ameandika vitabu vingi maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha ‘Manshurul-Fawaaid.’

Miaka 112 iliyopita katika siku kkama ya leo ya tarehe 30 Oktoba 1910 alifariki dunia Henry Dunant, mwasisi wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu. Dunant alizaliwa Geneva, Uswisi na mwaka 1828, aliamua kuanzisha Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu kwa shabaha ya kuokoa maisha ya majeruhi wa vita. Kutokana na hatua yake hiyo ya kibinadamu, Henri Dunant alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1901, na alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82.
Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Aban 1359 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Muhammad Hussein Fahmideh, kijana shujaa wa Kiirani kwenye vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Shahidi Fahmideh alielekea kwenye medani ya vita akiwa na umri wa miaka 13 tu, ikiwa imepita miezi michache tu baada ya kuanza kwa vita hivyo. Shahidi Fahmideh alijitolea mhanga kwa kujifunga kiunoni maguruneti na kujilaza mahala kilipokuwa kikipita kifaru cha adui na kuwatia kiwewe na hatimaye kuwalazimisha wavamizi kukimbia. Hatua hiyo ilipongezwa na Imam Khomeini ambaye alimtaja kijana huyo kuwa ni kiongozi na kigezo cha kuigwa. ***
Na miaka 132 iliyopita katika siku hii ya nne ya Rabi al-Thani, 1312 AH,
"Syed Ali Muhammad bin Sultan Ulama", anayejulikana kama "Taj Ulama", mmoja wa wanazuoni maarufu wa India, alikufa akiwa na umri wa miaka 52.
Alizaliwa mwaka 1262 Hijria katika mji wa Lucknow Kaskazini mwa India na akajifunza masomo ya kidini kutoka kwa baba yake na wanazuoni wengine wa mji wake. Taj al-Ulama alikuwa mwanachuoni msomi, mwanatheolojia, na mwanachuoni wa hadithi. Pia alikuwa na ujuzi mpana wa dini mbalimbali, hivyo akawa anajadiliana na wataalamu na wazee wa kila dini. Msomi huyu mwenye kuona mbali pia aliamini ulazima wa mapambano dhidi ya ukoloni wa Waingereza. Kuna vitabu visivyohesabika vilivyoachwa na Taj Ulama, kati ya hivyo tunaweza kutaja "Ahsan al-Qasas" katika tafsiri ya Surah Yusuf na "Ghohar Shab Chirag" kusu fadhila za Sala.
