Nov 02, 2022 22:52 UTC
  • Alkhamisi, Novemba 3, 2022

Leo ni Alkhamisi tarehe 8 Mfunguo Saba Rabiuthani 1444 Hijria sawa na Novemba 3 mwaka 2022 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1212 iliyopita alizaliwa Imam Hassan Askari (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Madina. Imam Askari alilazimishwa na watawala wa Bani Abbas kwenda uhamishoni huko Samurra akiwa pamoja na baba yake na kufaidika na elimu ya Imam Hadi kwa kipindi cha miaka 13. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu kwa kipindi cha karibu miaka sita baada ya kuuawa shahidi baba yake. Sehemu ya umri wake wa miaka 28 iliishia katika jela za watawala madhalimu wa Bani Abbas au akiwa uhamishoni na chini ya udhibiti wa watawala hao. Hata hivyo mtukufu huyo hakuacha kueneza maarifa sahihi ya Uislamu na kulea kizazi cha wanazuoni hodari.

Katika siku kama ya leo miaka 1087 iliyopita yaani mwaka 357 Hijria, aliaga dunia Abu Firas al-Hamdani malenga na mwandishi mahiri wa Kiarabu. Mbali na kuandika mashairi, Abu Firas al-Hamdani alikuwa mpiganaji na miongoni mwa watu wa karibu kwa Seif ad-Dawlah mtawala wa Halab na alikuwa miongoni mwa makamanda wake.

Abu Firas al-Hamdani

Miaka 176 iliyopita yaani mwaka 1268 Hijria, alizaliwa Sayyid Murtadha Kashmiri, mmoja wa maulama na maurafaa mahiri. Alimu huyo alizaliwa katika familia iliyokuwa ikiheshimika. Akiwa kijana mdogo alianza kusoma elimu za Kiislamu kwa baba yake na kwa maulama wengine wa eneo hilo. Akiwa na umri wa miaka 16 Murtadha Kashmiri alifunga safari na kuelekea Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu pia katika maudhui mbalimbali.

Miaka 105 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria aliaga dunia Sheikh al-Shari'a Isfahani mwalimu mkubwa wa Chuo Kikuu cha Kidini cha mjini Najaf Iraq. Alizaliwa mwaka 1266 Hijria katika mji wa Isfahan nchini Iran. Mwaka 1295 Hijria alielekea Najaf Iraq kwa lengo la kujiendeleza zaidi kimasomo na kufanikiwa kuhudhuria masomo na darsa za wanazuoni mahiri wa zama hizo kama Mullah Ahmad Sabzawar, Muhammad Hussein Kadhmeini, na Mirza Habibullah Rashti. Miongoni mwa wanafunzi wake ni Muhammad Taqi Khonsari, Abdul Karim Hairi na Muhammad Hussein Borujerdi. Sheil al-Shar'ia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 73 na amezikwa katika haram ya Imam Ali bin Abi Talib mjini Najaf Iraq.

Sheikh al-Shari'a Isfahani

Katika siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, wakati wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Misri, askari wa utawala huo waliwaua kwa umati Wapalestina katika mji wa Khan Yunis uliopo katika Ukanda wa Gaza. Baada ya kuingia katika mji huo askari hao wa Kizayuni waliwaua askari 25 wa Misri na baadaye wakavamia hospitali na kuwaua wagonjwa na wauguzi waliokuwa humo. Baadaye askari hao katili wa utawala wa Kizayuni walishambulia kwa mabomu na kuteketeza kambi ya wakimbizi ya mji wa Khan Yunis ambako makumi ya wanawake na watoto wadogo walikuwa wakiishi.

Khan Yinus, Ghaza

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 12 Aban 1352 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul Hussein Sha'arani arifu, faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 71. Msomi huyo alibobea katika elimu mbalimbali za kidini na alikuwa mahiri katika lugha kadhaa za kigeni. Ayatullah Mirza Abul Hussein Sha'arani ameandika vitabu vingi na alikuwa mahiri katika elimu za mujumu na nyota.

Ayatullah Mirza Abul Hussein Sha'arani

Na miaka 26 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 3 Novemba 1996, alifariki dunia Jenerali Jean-Bedel Bokassa dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Jean-Bedel Bokassa anayejulikana pia kama Bokassa I (wa kwanza) alichukua madaraka mwaka 1921 kupitia mapinduzi ya kijeshi, baada ya kuiondoa madarakani serikali ya Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Afrika ya Kati David Dacko. Bokassa alifanya mapinduzi hayo kwa uungaji mkono wa Ufaransa. Katika miaka 14 ya utawala wake, kiongozi huyo alitenda jinai na mauaji mbalimbali na kujilimbikizia mali nyingi. ***