Nov 05, 2022 22:45 UTC
  • Jumapili tarehe 6 Novemba, 2022

Leo ni Jumapili tarehe 11 Rabiuthani 1444 Hijria sawa na Novemba 6 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1224 iliyopita, alifariki dunia Abu Ali Khayyat, mnajimu na mtaalamu wa hesabati wa Kiislamu. Abu Ali ni mmoja wa shakhsia aliyekuwa na nafasi kubwa wakati wake huku jina lake likiwekwa mstari wa mbele katika kitabu cha majina ya wasomi wakubwa na mashuhuri wa dunia. Msomi huyo ameandika vitabu vingi maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha 'Mawaalid' na 'Siyarul-A'amaal.' Vitabu vingi vya Abu Ali Khayyat vimetarjumiwa kwa lugha ya Kilatini.

Siku kama ya leo miaka 836 iliyopita, alizawa mjini Mosul, moja ya miji mashuhuri ya Iraq, Ibn Khallikan, kadhi, mwanahistoria na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu. Akiwa kijana alisoma elimu za awali katika mji alikozaliwa na kisha kufanya safari mbalimbali na kukutana na wanasheria wa Kiislamu na wanahistoria wakubwa sanjari na kustafidi na elimu kutoka kwao. Kwa muda mrefu Ibn Khallikan alikuwa kadhi mjini Damascus, Syria ya leo huku akiwa mtaalamu pia katika elimu za historia, fasihi ya Kiarabu na mashairi. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwezi wa Rajab mwaka 681 Hijiria baada ya kuugua na kuzikwa chini ya mlima Qasioun ulio Damascus ambako pia wamezikwa wasomi wengi. Kitabu muhimuz aidi cha Ibn Khallekan ni Wafayatul A'yan.

Ibn Khallikan

Miaka 390 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Gustav wa Pili, mfalme wa Sweden. Alizaliwa mwaka 1594 na alikalia kiti cha ufalme alipokuwa na umri wa miaka 17. Umaarufu wake ulitokana na kushinda kwake katika vita vya kidini vya miaka 30 kati ya Waprotestant na Wakatoliki vya mwaka 1618 hadi 1648.

Gustav wa Pili

Siku kama ya leo miaka 209 iliyopita vita vya kwanza vya Simon Bolivar, shujaa wa uhuru wa mataifa ya Amerika ya Latini vya kukomboa nchi ya Venezuela kutoka kwa wakoloni wa Kihispania vilimalizika kwa ushindi. Katika vita hivyo askari 6500 wa Simon Bolivar waliwashinda askari elfu 13 wa Uhispania. Hatimaye shujaa huyo wa Amerika ya Latini aliikomboa Venezuela kutoka utawala wa kikoloni wa Uhispania na kisha akashiriki katika mapambano ya kupigania uhuru ya nchi nyingine kadhaa za kusini mwa Amerika.

Simon Bolivar

Miaka 162 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Novemba 1860 Abraham Lincoln aliyekuwa mpinzani wa utumwa nchini Marekani, alishika madaraka na kuwa rais wa nchi hiyo. Katika kipindi cha uongozi wake vita kadhaa vilitokea nchini Marekani na kupelekea kushindwa waliokuwa wakiunga mkono utumwa. Abraham Lincoln aliuawa mwaka 1865 na mmoja wa wapinzani wa harakati za kupinga utumwa nchini Marekani.

Abraham Lincoln

Na siku kama ya leo miaka 44 iliyopita wafanyakazi wa redio na televisheni ya Iran walianza mgomo wakipinga utawala wa Shah. Mgomo huo ulifanyika kwa shabaha ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya utawala wa Shah na kuharakisha mwenendo wa kuipindua serikali yake. Siku hiyo hiyo maafisa wa jeshi la Shah walishambulia taasisi za magazeti na vyombo vya habari na kuwatia nguvuni waandishi kadhaa. Hatua hiyo ilipelekea kusitishwa uchapishaji wa magazeti yaliyokuwa yakichapishwa kwa wingi nchini.

Mgomo wa wafanyakazi wa redio na televisheni ya Iran