Nov 11, 2022 22:57 UTC
  • Jumamosi 12 Novemba, 2022 Miladia

Leo ni Jumamosi tarehe 17 Mfunguo Saba Rabiu Thani wwal 1444 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 12 Novemba 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 125 iliyopita alizaliwa Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yushij, mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran. Isfandyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yushij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi. Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi mapya ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh". ***

Nima Yushij

 

Miaka 110 iliyopita katika siku kama hii ya leo Ayatullah Sheikh Muhammad Ali Nakhjavani mmoja wa maulama watajika na wapokezi wakubwa wa hadithi aliaga dunia huko Karbala nchini Iraq. Alikuwa mtu wa Nakhjavan katika Azerbaijan ya leo na alijifunza Qur'ani Tukufu akiwa na umri wa miaka 11. Baadaye alijifunza elimu za zama hizo kwa wanazuoni wakubwa. Mwanazuoni huyo alifanikiwa kufikiwa daraja ya Ijitihad na kuwa Marjaa Taqlidi wa Waislamu hususan wa eneo la Caucasia. Ayatullah Nakhjavani ameandika vitabu kadhaa vikiwemo vya Sherhe ya Rasaail na Makasib. Alizikwa katika Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika mji wa Najaf. ***

Ayatullah Sheikh Muhammad Ali Nakhjavani

 

Katika siku kama ya leo miaka 104 iliyopita yaani Novemba 12 mwaka 1918, utawala wa kifalme ulikomeshwa nchini Austria na kuanza kipindi cha utawala wa Jamhuri baada ya kushindwa utawala wa Austria na Hungary katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutengana nchi hizo mbili. Mfalme wa mwisho wa Austria, Charles wa Kwanza ambaye alitawazwa kuwa mfalme wa nchi hiyo tarehe 21 Novemba mwaka 1916, alijiuzulu uongozi siku moja tu baada ya kutiwa saini makubaliano ya kusimamisha Vita vya Kwanza vya Dunia hapo tarehe 11 Novemba mwaka 1918 na kuomba hifadhi nchini Uswisi. ***

Ramani ya utawala wa Austria kabla ya kugawanywa

 

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, vita vya kihistoria vilivyopewa jina la al-Alamein vilimalizika katika mji wenye jina kama hilo huko kaskazini mwa Misri kati ya wanajeshi wa Uingereza na jeshi la Manazi wa Ujerumani. Vita hivyo vilimalizika baada ya kushindwa jeshi la Ujerumani, japokuwa mapigano kati ya pande hizo mbili yaliendelea katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Afrika. Amani kamili ilipatikana katika maeneo hayo baada ya kushindwa kikamilifu jeshi la Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. ***

Vita vya al-Alamein

 

Miaka 66 iliyopita, askari wa utawala haramu wa Israel walifanya mauaji mengine ya umati dhidi ya Wapalestina wasio na hatia katika kambi kubwa ya Wapalestina mjini Rafah huko katika Ukanda wa Gaza. Jinai hiyo ilifanyika siku chache tu baada ya kutangazwa usitishaji vita baina ya Israel, Ufaransa na Uingereza dhidi ya Misri. Hujuma hiyo ya kinyama ilisababisha mauaji ya Wapalestina 110, wakiwemo wanawake na watoto na kujeruhi wengine 1,000. ***

Katika siku kama ya leo miaka 5 iliyopita ulitokea mtetemeko wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 7 kwa kipimo cha Rishta katika mkoa wa Kermanshah huko magharibi mwa Iran na maeneo ya kandokando yake huko mashariki mwa Iraq. Kituo kikuu cha mtetemeko huo wa ardhi kilikuwa umbali wa kilomita 5 kutoka mji wa Ezgeleh na kilomita 11 chini ya ardhi. Mtetemeko huo ulihisika pia katika nchi za Uturuki, Kuwait na Saudi Arabia. Karibu watu 574 waliaga dunia kutokana na mtetemeko huo wa ardhi na wengine elfu 9,388 walijeruhiwa. Watu wengine elfu sabini walipoteza makazi yao. Idadi kubwa zaidi ya watu walipoteza maisha katika miji ya Qasr-e Shirin, Sarpol-e Zahab na Salas-e Babajani. ***

Tetemeko la ardhi katika mkoa wa Kermanshah magharibi mwa Iran