Jumatano tarehe 16 Novemba 2022
Leo ni Jumatano tarehe 21 Mfunguo Saba Rabiuthani 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 16 Novemba 2022.
Miaka 42 iliyopita katika siku kama leo mji wa mpakani wa Susangerd huko kusini magharibi mwa Iran ulishuhudia mapambano kati ya wapiganaji wa Kiislamu na wanajeshi vamizi wa utawala wa zamani wa Iraq. Oparesheni hiyo ya kujihami ilifanywa na wapiganaji shupavu 200 wa Iran waliojumuisha wanajeshi wa ulinzi, wanamgambo wa kujitolea na idadi ya kadhaa ya wenyeji wa mji huo waliokuwa wakitumia silaha nyepesi dhidi ya jeshi vamizi la Saddam. Katika operesheni hiyo wapiganaji shupavu wa Iran chini ya uongozi wa shahidi Dakta Mustafa Chamran, walipambana vikali na kufanikiwa kuukomboa mji wa Susangerd.
Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, Allama Muhammad Taqi Jaafari, mwanafalsafa na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1304 Hijria Shamsia katika mji wa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran. Kipaji chake kilidhihiri na kuchomoza tangu akiwa katika kipindi cha kuinukia kwake ambapo kabla ya kuanza shule ya msingi tayari alikuwa amejifunza Qur'ani. Akiwa shule alionekkana mwenye kipaji mno. Hata hivyo umasikini ulimfanya aache shule na kuanza kufanya kazi. Pamoja na kufanya kazi aliutumia muda wake wa ziada kusoma masomo ya dini. Allama Muhammad Taqi Jaafari ameandika vitabu vingi ambapo Tarjuma na Tafsiri ya Nahajul Balagha ndio kitabu muhimu zaidi cha mwanazuoni huyo.
Na miaka 22 iliyopita sawa na tarehe 25 Aban 1379 Hijria Shamsia, aliaga dunia Hujjatul Islam, Dakta Muhammad Hadi Amini Najafi, mmoja wa maulama na waandishi mahiri wa Kiirani. Alizaliwa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran, na katika kipindi cha ujana wake alielekea huko Najaf, Iraq akiwa pamoja na baba yake, Allama Amini, mwandishi wa kitabu mashuhuri cha al-Ghadir. Msomi huyo alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar nchini Misri. Mwaka 1350 Hijria Shamsia Dakta Muhammad Hadi Amini Najafi alirejea nchini Iran na kuanza kufanya kazi ya uandishi, kufundisha na kufanya uhakiki.